Dk. Slaa aweka serikali njiapanda


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 June 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi

SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iko njiapanda. Kambi ya upinzani bungeni imeonya kuwa isipopewa majibu sahihi kwa hoja zake, itaifikisha serikali "kizimbani".

Akiwasilisha maoni ya upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Kiongozi wa Upinzani, Dk. Willibrod Slaa amesema, upinzani utaishitaki serikali kwa wananchi ambao wana uwezo wa kuihukumu.

Serikali haijaeleza imechukua hatua gani za kuridhisha dhidi ya wahusika katika wizi wa mabilioni uliohusisha makampuni ya ndani na nje kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ameeleza.

Upinzani unataka serikali ieleze kinagaubaga ukweli wa tuhuma zinazohusisha ubia wa BoT, benki ya Afrika Kusini – NEDBANK – na kampuni ya Deep Green Finance iliyosajiliwa nchini katika mazingira ya kutatanisha.

Makampuni hayo na mengine ya Tangold na Meremeta yamekuwa yakihusishwa na uchotaji wa mabilioni na wakati mwingine kubadilishana malipo kwa njia za kutilia mashaka.

Maoni ya upinzani yaliwasilishwa bungeni juzi, Jumatatu mara baada ya hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Zaidi ya Sh. 50 bilioni zinakadiriwa kupitia mikononi mwa makampuni haya bila maelezo yalitolewa kwa misingi ipi, kwa kazi ipi na katika taratibu zipi za utawala wa fedha.

Dk. Slaa alisema serikali imekuwa ikikwepa kuzungumzia tuhuma hizo kwa umakini kwa kipindi cha miaka mitatu sasa, jambo alilosema ni ishara ya udhaifu mkubwa na mwenendo wa ndumilakuwili kwa upande wa serikali.

Kuhusu NEDBANK, Dk. Slaa anajenga mashaka iwapo kweli ni benki yenyewe au matapeli. Aliuliza kama walioshiriki wizi ni maofisa wa benki, kwa nini benki hiyo yenye heshima kubwa duniani na historia ya zaidi ya miaka 100, haijatoa msimamo wake.

Alisema, “Kambi ya Upinzani inatoa ilani kuwa sasa baada ya jitihada za miaka takriban mitatu, tutafanya kampeni ya dunia nzima kuomba benki hiyo iliyoshiriki kwenye ufisadi ifungiwe kwa vile haiaminiki tena.”

Dk. Slaa aligusia ufisadi wa Deep Green Finance Company Ltd kwa kuitumia benki ya NEDBANK sambamba na ufisadi uliofanyika ndani ya BoT kupitia makampuni ya Tangold na Meremeta.

Amesema tuhuma za ufisadi unaohusisha makampuni hayo hazijapata kuelezwa kwa ufasaha na serikali, na upinzani unaona hakuna tena nafasi ya kuvumilia.

“Tunahitaji kuelezwa kinagaubaga masuala haya. Kwanini Serikali yetu inafanya kazi kwa “Double Standard? Hii ni hali ya hatari,” alisema.

Amesema inashangaza Waziri Mkuu kuwa mkali kuhusu mwenendo wa DECI iliyofanya kazi kwa miaka miwili tu huku akiwa kimya kwa Tangold iliyofanya kazi nchini kwa miaka minne bila ya kusajiliwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Jaji Bomani iliyochunguza Tangold na makampuni ya Meremeta na Deep Green Finance, Tangold ni mali ya watu binafsi lakini serikali imekuwa ikisema inaimiliki kwa asilimia 100.

Dk. Slaa pia anataka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa anayetajwa kuhusika na kujibinafsishia mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, kwa kutumia kampuni binafsi aliyoianzisha wakati akiwa bado ikulu.

Amesema kuna uthibitisho wa kutosha kuwa Mkapa alianzisha kampuni binafsi na kampuni hiyo, ikishirikiana na makampuni mengine, yakabinafsishiwa Kiwira.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 46(3) inaeleza, rais mstaafu ana kinga kwa jambo lile tu ambalo akiwa madarakani kama rais alilifanya au alikosa kulifanya.

Hii ina maana kwamba “rais mstaafu anakosa kinga kwa jambo alolifanya kama raia binafsi (mjasiriamali) akiwa madarakani,” alisema.

Katika hatua nyingine, serikali imetakiwa kufanya ukaguzi mahsusi kwenye mashirika yake yakiwemo Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kutokana na kugubikwa na matumizi mabaya ya mabilioni ya shilingi.

Dk. Slaa amesema ndani ya TBC, hakuna maelezo ya mali za kudumu za iliyokuwa Radio Tanzania (RTD) wakati hakuna nyaraka zinazoonyesha salio katika akaunti ya RTD.

“Ni udhaifu mkubwa sana katika usimamizi wa mali ya umma, na isipoangaliwa inaweza (kuleta) upotevu na au wizi wa mali hizo,” alisema.

Kadhalika, amesema manunuzi ya zaidi ya Sh. 2.4 bilioni (sawa na zaidi ya asilimia 49 ya manunuzi yote ya RTD) yalifanywa nje ya wigo wa matumizi halali kulingana na tangazo la serikali Na. 97 na 98.

Manunuzi yenye thamani ya zaidi ya Sh. 178 bilioni nayo hayakuwa na idhini ya Bodi ya Zabuni, alisema akirejelea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kuhusu TANAPA, Dk. Slaa amesema taarifa ya CAG ya hesabu za 2007/08 inaonyesha ubadhirifu wa amana zenye thamani ya Sh. 7.360 bilioni (dola 4,088,801).

Taarifa ya CAG inaonyesha hakuna mikataba inayothibitisha malipo yaliyofanywa kwa Shirika la Habari la Kimarekani la CNN lililorusha matangazo ya TANAPA; hivyo kuna shaka kama matangazo yalitolewa kwa kiwango na mfumo uliotakiwa.

“Hatima ya mikataba hii na usalama wa fedha zetu haifahamiki, ikiwamo thamani ya fedha kwa huduma iliyotolewa,” alisema na kutahadharisha kuwa shirika hilo lina hali mbaya ya kifedha kiasi cha kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.

Dk. Slaa anakomalia kasma mpya katika bajeti itakayogharimu serikali Sh. 19 bilioni (Sh. 19,963,429,490) akisema kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya matumizi ya chakula na viburudisho kwa viongozi waandamizi wa wizara wawapo ofisini.

Amesema fedha nyingi zinazotumika kwa njia hii zingeweza kuziba pengo katika maeneo kadhaa na kupunguza mzigo kwa wananchi.

0
Your rating: None Average: 3 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: