Dk. Slaa chaguo sahihi, kwa wakati sahihi


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version

CHAMA kilichopo ikulu, kinatetemeka. Kinafikiri jinsi Dk. Willibrod Slaa atakavyoingia madarakani na kuunda serikali itakayoleta mabadiliko.

Haya yanapokuja, watawala wamejikuta hawana mbinu nyingine, badala yake wanatupa ngumi gizani wakiamini kuwa wananchi watawaogopa. Hizi ni mbinu za miaka mingi za Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Wananchi wamefikia mahali wameuona ukweli kuwa kuendelea kuwa na utawala wa CCM kama alivyosema Dk. Slaa, “ni maafa kwa taifa.”

Dk. Willibrod Slaa na ujumbe wake wa mabadiliko wanawakilisha katika taifa nafasi pekee ambayo wiki chache zilizopita haikuwa inawezekana.

Nafasi ya wananchi kufanya mabadiliko makubwa ya kuindoa serikali iliyoko madarakani na kuleta serikali mpya yenye kujali kweli maslahi ya nchi.

Wakati wananchi wanajiuliza ni mgombea yupi wamchague katika nafasi ya urais, naomba nipendekeze kuwa kati ya wagombea wote wa nafasi hiyo, hakuna mgombea anayeahidi mabadiliko makubwa, ya kina na ya lazima kama Dk. Slaa.

Dk. Slaa na chama chake wamekuja mbele ya taifa letu na pendekezo la wazi kabisa ambalo haliitaji kutanguliwa na vikosi vya gwaride ili watu waweze kulipokea.

Hatuwezi kuendelea na kufanikiwa kama taifa hili litaendelea kubaki mikononi mwa CCM.

Bila wananchi ambao kimsingi ndio wenye uamuzi wa mwisho kuhusu nchi yao, basi ni wazi kuwa kizazi kingine kitaendelea kukaa katika hali ya kusubiri kudra wakati kundi la watu wachache likijilimbikizia madaraka.

Dk. Slaa na wenzake wanapendekeza kufanya mabadiliko makubwa kuanzia katika vyombo mbalimbali vya utawala hadi kufikia kwenye katiba.

Mabadiliko ambayo Dk. Slaa na timu yake wanayapendekeza, ni mabadiliko ya kutaka kuona kuwa hatimaye taifa la kisasa linaanza kujengwa katika nchi yetu.

Kuanzia mabadiliko ya mfumo wa elimu, vyombo vya ulinzi na usalama na hasa katika muundo wa utawala, vyote vina lengo moja tu: Nalo ni kusahihisha makosa ya miaka arobaini na tisa ya utawala wa CCM.

Makosa haya ikiwemo kukosa mwelekeo wa taifa na kupotea kwa uongozi bora kumeligharimu kwa kiasi kikubwa taifa hili.

Kwa mfano, leo hii tunapoangalia katika ahadi zake kubwa zote ambazo mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete amezitoa kuanzia kule Karagwe alipoanza kampeni hadi Mwembeyanga alipokuwa majuzi, karibu asilimia 99 zinanogeshwa na kupatikana kwa wafadhili.

Kuanzia ujenzi wa barabara kule Bukoba hadi ujenzi wa hospitali ya magonjwa ya Moyo jijini Dar es Salaam, zote kwa kiasi kikubwa zinategemea misaada ya wafadhili.

Haijulikani iwapo wafadhiri wanaotegemewa wakijiondoa, fedha ya kuendesha miradi hiyo zitatoka wapi?

Hii ni tofauti na Dk. Slaa ambaye ahadi zake nyingi ikiwamo ile iliyonivutia ya kuleta nidhamu katika matumizi ya serikali, haihitaji fedha kutoka nje.

Ahadi hii itaokoa mabilioni ya shilingi ambayo yataweza kutumiwa katika mambo mengine.

Ahadi nyingine ambayo Dk. Slaa ameitoa na ambayo imenivutia, ni uthabiti wake wa kutokuwavumilia viongozi wabovu kama inavyofanywa sasa chini ya utawala wa CCM.

Yote haya mawili ni sawa kabisa na kufungua dirisha ili hewa safi iweze kuingia.

Ndugu zangu, tunapoandika kuhusu hili watu wengine wanaweza kuamini kuwa tunaandika tukiwa na chuki na serikali.

Lakini serikali ni chombo cha wananchi na ni kama gari ambalo dereva wake akiliendesha vibaya kunaweza kutokea ajali.

Hivyo, watu wanapotaka mabadiliko kwa kiasi kikubwa wanabadilisha dereva badala ya gari lenyewe.

Uchaguzi huu ni nafasi ya Watanzania kuamua kwa hiari yao kumuondoa dereva mbovu (CCM) na kumuingiza dereva mpya kwenye gari lao (yaani serikali yao).

Wazo hili la CCM kukataliwa na wananchi linawasumbua na linawatisha mno chama hicho kwa kuwa wananufaika wa mfumo wa utawala kuliko kitu kingine.

Kwamba upo uwezekano wa Dk. Slaa kushinda na kumuwezesha kuunda serikali mpya yenye mwamko mpya ikihusisha watu makini na wasioyumbishwa na watuhumiwa wakuu wa ufisadi.

Niliandika hivi miaka mitatu iliyopita: “Kuanguka kwa CCM, unabii utatimia.” Ukweli ni kuwa unabii huu unaendelea kutimizwa kila dakika na watu wasije kushtuka wakiamka tarehe 1 Novemba 2010 na kuikuta CCM haina tena kucha zake.

Nina uhakika wa asilimia 100 kuwa serikali itakayoundwa na Dk Slaa ndiyo itakuwa chachu kubwa ya mabadiliko kwa taifa na ambayo itatupa nafasi ya kuanza kujenga taifa la kisasa.

Hata katika maandiko matakatifu si wana Israeli wote waliokuwa tayari kutoka Misri na wengine kwa hakika safari ya kwenda nchi ya ahadi ilikuwa ni ngumu.

Wapo ambao baada tu ya kufurahia kuvuka Bahari ya Shamu walijikuta wanapata njaa ya ghafla na kuanza kuyakumbuka “matikiti maji na vitunguu saumu vya Misri.”

Dk. Slaa na wenzake wamewaita wananchi watoke katika nchi ya Misri na kuachana na fahari ya Farao ili waweze kujijengea taifa lao la kisasa.

Tunajua kuwa si wote wanafurahia ujumbe huu na si wote wako tayari kuona mabadiliko kutoka kile walichokizoea.

Lakini hivi sasa hakuna utata tena kuwa Dk. Slaa anawakilisha kipindi cha mabadiliko na ndiye chaguo sahihi katika wakati huu wa kihistoria.

Wananchi watakapoenda kupiga kura kesho Jumapili watambue kuwa hawapigi kura kuchagua maisha ya anasa, ufahari na umangimeza.

Bali, wanakwenda kupigakura ili kuamua kama miaka mitano ijayo, watakula nyama watakazowinda, vitunguu saumu na matiki kutoka mashamba yao na kuuza mengine wakitaka.

Lakini siyo wao tu, uchaguzi huu unauliza swali moja la msingi: Je, Watanzania wanataka kuwarithisha watoto wao taifa la namna gani?

Ninaamini baada ya kusikiliza kampeni, kuwafuatilia wagombea, tumepata fursa ya kujiuliza: Tunataka tuwaache tena watawala walioshindwa wajaribu tena kwa miaka mingine mitano, ama sasa yametosha?

Katika hili kusiwe na utata. Ni lazima tutalipa tutakachokipanda. Tunaowajibu kama taifa wa kuhakikisha kuwa tunaitumia nafasi hii ya kujenga taifa kwa umakini.

Naam! Hakuna lolote ambalo wahusika wanaweza kututisha kwani kama ilivyoandikwa, “Hawa Wamisri mliowaona leo, hamtawaona Milele.”

Kimsingi utawala wa CCM unakaribia kuachwa kwenye jumba la makumbusho.

Na kwa vile historia imekuita kufanya uamuzi kwa ajili ya watoto wako na watoto wa watoto wake, nawe itika. Dk. Slaa na CHADEMA wametubipu, tuwapigie kura.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: