Dk. Slaa, Kikwete uso kwa uso


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinakusudia kumshitaki Rais Jakaya Kikwete kwa umma, iwapo atagoma kukutana nao, imeleezwa.

Taarifa kutoka ndani ya CHADEMA zinasema, mkakati wa CHADEMA kumpeleka Kikwete kwenye mahakama ya umma ulifikiwa kwenye kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, ambapo wajumbe kwa kauli moja walikubaliana chama kilifikishe suala la katiba kwa wananchi.

“Pale kwenye kikao cha Kamati Kuu (CC), tulikubaliana kulipeleka suala hilo kwa wananchi. Lakini tumeamua kwa sasa, kumpa fursa Kikwete ya kukutana na chama chetu,” ameeleza Tundu Lissu mwanasheria wa chama hicho.

Alisema, “Tutakwenda kwa wananchi kuwambia ukweli wa kilichotokea. Katika hilo, hatutaogopa polisi wala jeshi. Tutakwenda kijiji kwa kijiji, nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa, kueleza madhara ya hiki ambacho CCM wamekipitisha na hatua ambazo wamepitia kuunda muswaada wa katiba mpya,” ameeleza Lissu.

Hata hivyo, akijibu maswali ya waandishi wa habari, makao makuu ya CHADEMA, juzi Jumatatu, mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe aligoma kuzungumzia suala hilo kwa undani.

Badala yake, Mbowe alisema, “Kwa nini unataka tuvuke mto, wakati hatujafika kwenye daraja.” Mbowe kujibu swali lililotaka msimamo wa chama iwapo Kikwete atagoma kukutana nao.

Alisema baada ya kukutana na Rais Kikwete na kumweleza ushauri wao, watamsikiliza atakachowaeleza; iwapo atapuuza madai yao, watalazimika kuchukua uamuzi mmoja tu: Kwenda kwa wananchi. Hakufafanua.

Katika mkutano wa CC, CHADEMA kimeamua kuunda kamati ya watu sita itakayoongozwa na Mbowe na katibu mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa kukutana na serikali kwa lengo la kutafuta kile walichoita, “Mwafaka wa kitaifa.”

Wajumbe wengine wa kamati hiyo, ni makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara, Said Arfi, makamu mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohammed, wajumbe wa Kamati, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari. Mjumbe mwingine, ni mkurugenzi wa sheria wa chama hicho, Tundu Lissu.

Iwapo dhamira ya CHADEMA kukutana na Kikwete itafanikiwa, hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Dk. Slaa kukutana na Kikwete, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambapo Slaa alitoa ushindani mkubwa kwa kiongozi huyo wa nchi.

Mbowe amesema wanataka kumweleza rais ukweli wanaouamini kwamba kiongozi huyo amepotoshwa na wasaidizi wake serikalini na vilevile katika chama kuhusu suala hilo na umuhimu wa kusikiliza mapendekezo ya CHADEMA ili kurekebisha mchakato katika njia nzuri.

“CHADEMA kinaamini kuwa Rais Kikwete amempotosha na wasaidizi wake, naye ameendelea kupotosha Watanzania. Lakini bado tunaamini katika kutumia fursa za kisiasa na kijamii katika kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya haja, nia, mchakato na misingi ya katiba inayotakiwa na wananchi,” ameeleza Mbowe.

Mbowe ambaye ni kiongozi wa upinzani bungeni amesema, “Ushiriki wa CHADEMA katika mchakato mzima wa kupata katiba mpya uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utategemea utayari wa serikali ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika sheria iliyopitishwa kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo.”

“Hotuba ya rais Kikwete imezidi kuwagawa Watanzania kwa misingi ya ushabiki wa vyama badala ya kuwaunganisha katika suala hili muhimu kwa mustakabali wao na taifa lao. Nia ya chama chetu ni kuelekeza njia nzuri ya kupatikana kwa mwafaka ili kuepusha katiba mpya kupatikana kwa mapambano,” ameeleza.

Amesema chama chake kinaamini kuwa sheria iliyopitishwa na Bunge ina upungufu katika maeneo mengi na ya kimsingi na hivyo kuleta kasoro kubwa.

Aidha, Mbowe ametuhumu viongozi na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wenzao kutoka Chama cha Wananchi (CUF), kwamba wamewadanganya wananchi kwa maslahi binafsi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: