Dk. Slaa kweli aweza kumshinda Kikwete?


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Dk. Willibrod Slaa

JAWABU la swali hilo hapo juu linalobeba kichwa cha habari, kwa hakika, linategemea ni nani unamuuliza.

Ukimuuliza mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jibu lake halitachelewa; Dk. Slaa hawezi kabisa kumshinda Kikwete. Atasema kwa sababu “Kikwete anakubalika, sera za CCM zinakubalika na Kikwete mwenyewe amefanya mengi katika uongozi wake.”

Lakini ukimuuliza mfuasi au mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jibu lake naye halitakuwa gumu; atasema “Bila ya shaka, Dk. Slaa anakubalika kwani ameonesha ujasiri usio kifani katika kuwashughulikia mafisadi, amesimama kidete kupigania maslahi ya taifa na kwa miaka 15 ameendelea kuchaguliwa kama mbunge wa chama chake kutoka Karatu ambako historia ya uongozi wake inaonesha ni jinsi gani ni mtu wa watu”.

Swali hilo hilo ukimuuliza mtu ambaye hana chama, jibu lake linaweza kuwa na utata wa aina fulani. Yeye ataanza kwa kusema “anaweza” na halafu papo hapo ataongeza na “lakini”.

Anaposema “anaweza” mtu huyo anakiri kuwa kama hali fulani fulani zikitimia au mazingira fulani yakiwa sawasawa basi Dk. Slaa anaweza kuishangaza Tanzania na dunia na kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu licha ya kuungwa mkono kukubwa na kubebwa ambako Rais Kikwete anafanyiwa.

Na anaposema “lakini” anakiri kuwa yumkini hata Dk. Slaa na CHADEMA wajitahidi vipi tayari ushindi umeshaamriwa kuwa Kikwete na CCM lazima washinde na kilichobakia ni kukamilisha taratibu tu.

Na lipo kundi jingine ambalo jibu lake ni “hatujui”. Kundi hili la tatu ndilo kundi litakaloamua nani anashinda uchaguzi mkuu mwaka huu. Kundi hili linaweza kujumuisha mashabiki wa vyama vingine na wagombea wengine zaidi ya Dk. Slaa na Rais Kikwete na wale ambao wao timu inayoelekea kushinda ndiyo inakuwa ya kwao.

Hata hivyo, tukirudia swali hilo hilo, tunaweza kuona kuwa ushindi wa Dk. Slaa unawezekana bila kujali CCM na serikali yake vinafanya nini. Hii ina maana ya kwamba TBC, magazeti na vyombo vingine vyote vya habari vinaweza kujipanga kumpigia debe Rais Kikwete huku vyombo vya dola vikitumia mbinu mbalimbali kuhakikisha kuwa vinamminya mgombea wa CHADEMA lakini bado mgombea huyo akaweza kushinda.

Katika mazingira ya Tanzania yalivyo sasa hivi, ni muhimu kudhania kuwa, hali iliyopo sasa kisiasa itabakia jinsi ilivyo na hivyo ushindi wowote wa upinzani ni lazima uje katika mazingira haya.

Kwamba, msajili wa vyama vya siasa atakuwa mgumu zaidi kwa vyama vya upinzani kuliko CCM, na kuwa polisi na vyombo vya usalama vitajitahidi kuvuruga kampeni za vyama vingine.

Ni muhimu kutambua kuwa haya yote yatatokea bila kuonekana kuwa yatatushangaza. Ni muhimu kutambua kuwa watu wengi watakapoanza kujipanga nyuma ya CHADEMA/ Dk. Slaa, itasababisha CCM kutumia mbinu kali zaidi na wakati mwingine, naweza kutabiri kuwa, hata matumizi ya nguvu yanaweza kuwepo katika uchaguzi huu hasa kuelekea ngwe ya mwisho ya kampeni.

Hata hivyo, ni muhimu kutambua ukweli mmoja wa kushangaza sana kuwa, ujio wa Dk. Slaa katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu unakumbusha ujio wa mwanasiasa mwingine ambaye hakutarajiwa kabisa kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka 2008 na ambaye jina lake lilikuwa halijulikani sana hadi miezi michache tu kabla ya msimu wa uchaguzi kuanza.

Wamarekani wengi walikuwa hawamjui Barack Obama, Seneta kutoka Illinois hadi siku ile alipotoa hotuba yake katika mkutano mkuu wa chama cha Democrat mwaka 2004.

Ni katika hotuba yake ile ambayo ilibeba maudhui ya Kitabu chake cha “The Audacity of Hope” (Ujasiri wa Matumaini) Wamarekani wengi walifumbua macho yao kusikia sauti mpya ya mabadiliko ambayo haikuwa waliyoizoea.

Haikuwa ya Seneta Ted Kennedy au John Kerry, haikuwa sauti ya wanasiasa maarufu wa Kimarekani bali ya mwanasiasa mwenye umbile dogo tu lakini aliyekuwa na uzoefu mkubwa katika kupigana na mfumo mbaya wa kiutawala uliochangia kuendeleza umaskini katika maeneo ya Kusini ya Jiji la Chicago.

Kuanzia wakati ule, tetesi zilianza kuonekana kuwa yawezekana mwanasiasa huyo mgeni kabisa katika ulingo wa siasa angeweza kugombea urais wa Marekani. Hata hivyo, hakutarajiwa kuweza kushindana na jopo la wanasiasa wakongwe wa Democrat wakiongozwa na Hillary Clinton (Mke wa Rais Clinton) ambaye uchaguzi wa 2008 ulikuwa ni kama umeshakubalika kuwa ni wa kwake kuupoteza.

Hata katika mchakato wa kura za maoni Obama alionekana kuanza kupata moto mpya wa mabadiliko, hasa baada ya kuja na fikra mbadala na kali za mabadiliko kuliko za wagombea wengine mashuhuri kama mwanasheria John Edwards, Dk. Howard Dean, Hillary Clinton, Joe Biden n.k

Kutokana na msimamo wake mkali wa mabadiliko ambao haukuwa tayari kuurembesha utawala wa Rais George Bush, Obama alijikuta anasimama kama mgombea mwenye kuungwa mkono sana kiasi kwamba hata mpinzani wake katika kura za urais John McCain alijikuta hana ubavu wa kushindana naye licha ya kuwa jina lake lina historia ndefu katika siasa na majeshi ya Marekani kwa zaidi ya miaka 50!

Kumbe ushindi hauji kutokana na kuwa na madaraka, kubebwa na vyombo vya habari au kuwa na jina zuri na kubwa.

Ni kutokana na ukweli huo Wamarekani wamekuwa na utaratibu wa kuweza kumnyima ngwe ya pili rais wao ili waanze upya kwani walijua kuwa ile ngwe moja inatosha kabisa kuwaonesha huyo Rais yukoje. Walifanya hivyo walipomkatalia ngwe ya pili Jimmy Carter (wa Democrat) na kama walivyomkatalia ngwe ya pili George H. Bush (Republican). Wote walipitishwa na vyama vyao kugombea tena.

Hii ina maana ya kwamba, Dk. Slaa, kama Obama anaweza kabisa akijipanga vizuri na kuja na ujumbe mkali wa mabadiliko huku akiwa na ujumbe wa matumaini ambao ni kinyume na bora zaidi ya ule wa CCM na akashinda.

Tena nafasi hiyo ni kubwa zaidi kwa Tanzania ambapo Rais huchaguliwa kwa kura moja moja na siyo kama mtindo wa Marekani ambapo mfumo wao unategemea baraza la kupiga kura. Dk. Slaa kwa hakika si Obama na siasa zetu siyo za hoja kama za Marekani.

Lakini siasa za Marekani mwaka 2008 hazikuhusu sana hoja kama zilivyokuwa zile za 2004, hizi zilikuwa na zaidi ya hoja, zilikuwa zinahusu mtu mwenyewe. Kumbe kati ya hawa wawili Dk. Slaa na Rais Kikwete ni wazi kabisa Dk. Slaa ana nafasi ya kuleta sura mpya kabisa ya uongozi wa taifa kuliko Rais Kikwete.

Tunafahamu kabisa kuwa, endapo wabunge wengi wa CCM watarudishwa tena bungeni au hata wakija wengine wapya, bado watakuwa ni wengi kutoka CCM na Rais Kikwete ataunda serikali yake kutokana na watu hao hao.

Tunafahamu mabadiliko makubwa ambayo Rais Kikwete ataweza kuyafanya (tukichukulia jinsi alivyofanya mabadiliko miaka hii mitano iliyopita) ni kuwazungusha watumishi na watendaji kutoka nafasi moja kwenda nyingine huku bado wakibakia ndani ya CCM.

Lakini uongozi mpya wa Dk. Slaa, hata hivyo, utalazimisha kuingia kwa utumishi mpya katika serikali yetu.

Kumbe basi, kwa wale wanaotaka Dk. Slaa aweze kushinda, hawawezi kufanikiwa hivyo bila kuhakikisha kuwa wagombea wa CHADEMA nao wanashinda katika majimbo yao. Ni katika kufanya hivyo watajikuta wanampatia Dk. Slaa kura za ushindi na watu wa kufanya naye kazi.

Haiwezekani kumpigia kura Dk. Slaa (kwenye urais) na kumnyima wabunge kwa sababu Rais peke yake hawezi kufanya lolote.

Hata hivyo, Dk. Slaa asitegemee kura na wagombea wa ubunge wa CHADEMA wasitegemee kubebwa na wananchi. Ni lazima wawape sababu ya kwanini wachaguliwe wao. Kwanini waikatae serikali iliyoahidi “zaidi” na kwanini wamkatae mtu ambaye amerudia mara kadhaa kile kinachojulikana kama “mafanikio ya serikali ya awamu ya nne”.

Hili haliwezi hata kidogo kuwa “kwa sababu ni wa CCM”. Ni lazima iwe ni sababu yenye kugusa mioyo, yenye kuamsha hisia na yenye kuvuta akili.

Obama alijua hilo, yeye alisema “Change – Yes we Can”. Ni maneno manne lakini ndani yake yalibeba ukweli mzima wa kampeni ya Obama. Kwa upande wa Dk. Slaa Watanzania wanasubiri kuona ni mbiu gani itakayotuashiria kile tunachokitarajia.

Je “Mabadiliko-Na sisi tunaweza” nayo ni maneno manne lakini yanaweza kuamsha mioyo ya watu? Vyovyote vile ilivyo, ni ujumbe wenye kubeba ahadi ya matumaini tu ndio utakaowafanya Watanzania waweze kuamua kwa mamilioni yao kuishukuru CCM kwa uongozi wa muda mrefu, lakini hatimaye kuiaga wakiimbia “CCM bai bai, na kwa heri ya kuonana” huku wakiimba nyimbo za kumkaribisha Dk. Slaa.

Ni rahisi kufikiria hivyo, lakini ni ngumu kufanya iwe kweli. Kwani, mabadiliko ya kweli yanahitaji kulipia gharama. Na gharama ya kwanza kabisa ni kwa wananchi kufumbua macho yao na kuona kile kinachowezekana. Wakikitambua basi swali la “Je Dk. Slaa anaweza kumshinda Kikwete” haliwi gumu tena.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: