Dk. Slaa: Ndio tunaanza


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Mgombea Urais kupitia CHADEMA, Willibrod Slaa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepanga kutoa elimu kwa wapigakura kwa njia ya kutoboa siri zote za ufisadi zinazoigusa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia wiki ijayo.

“Wananchi wana haki ya kujua serikali inafanya madudu gani; kwa nini imeshindwa kutawala na kwa nini wanapaswa kuiondoa kwa njia ya sanduku la kura,” ameeleza ofisa mmoja wa chama hicho.

Katika hatua hiyo ya kampeni za lala salama, viongozi wakuu wa CHADEMA wataandamana na mwasisi wa mageuzi nchini, Mabere Marando ambaye amepewa jukumu la kufafanua kwa kina, ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka Hazina na Benki Kuu (BoT).

Jukumu hilo jipya kwa Marando ambaye ni miongoni mwa wanasheria wanaoheshimika nchini, linakwenda sambamba na uteuzi wake wa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA uliotangazwa wiki hii.

Marando ni wakili wa baadhi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) uliofanyika kati ya mwaka 2005 na 2006.

Wakati wa uzinduzi wa kampeni za kitaifa za CHADEMA zilizofanyika katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) lilikatisha matangazo yake ya moja kwa moja ya tukio hilo baada ya Marando kuanza kutaja aliowaita “mafisadi wakuu” nchini.

Habari kutoka ndani ya CHADEMA zinasema Marando atajiunga na kampeni za mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kuanzia Oktoba 6 mwaka huu.

“Wabunge na viongozi wa CHADEMA ndio walikuwa wa kwanza kutaja hadharani orodha ya watuhumiwa wa ufisadi wakiwemo viongozi wa sasa wa kitaifa na waliostaafu,” amesema kiongozi mmoja wa CHADEMA aliyezungumza na gazeti hili juzi Jumatatu.

Mtoa taarifa huyo amesifia Marando kwa uwezo wake wa kujenga hoja na kusema, “Sasa, kwa kuwa tumepata bahati ya kuwa na Marando, nafikiri kipele kimepata mkunaji. Tutamwachia yeye alishughulikie hilo,”

Mbali na Marando kupewa kazi hiyo ya kushughulikia tabia ya serikali na wizi kupitia EPA, sasa MwanaHALISI linaweza kuthibitisha kwamba mwanasheria huyo ni miongoni mwa wajumbe wa kamati ya ufundi iliyoundwa kuteua wabunge wa viti maalumu wa chama hicho.

Timu hiyo ya ufundi inaundwa na watu wanne ambao ni; Mwenyekiti wa kampeni ya kitaifa ya chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Dk. Kitilla Mkumbo, Marando na Shida Salum – mama mzazi wa mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Timu hiyo imepewa kazi ya kuchambua sifa za wagombea zaidi ya 60 wa viti hivyo maalumu na kuteua wabunge hao kabla ya Septemba 30 mwaka huu.

Tayari Kamati Kuu ya CHADEMA imekwishatangaza vigezo vikuu sita vitakavyotumika kuteua wabunge wa viti maalumu ambao uteuzi wao tayari umeibua kutoelewana katika siku za karibuni.

Kigezo cha kwanza ambacho MwanaHALISI linafahamu kitatumika katika uteuzi huo ni matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Kigezo hicho kinamaanisha kwamba wagombea wanaotoka katika maeneo ambako CHADEMA ilipata kura nyingi katika uchaguzi wa mwaka 2005, ndio watakaopewa kipaumbele.

Uteuzi huo unamaanisha kwamba mwaka 2015, wagombea watakaokuwa na nafasi zaidi ni wale ambao mikoa yao itafanya vizuri zaidi mwaka huu.

Kigezo cha pili kitakachozingatiwa ni kuenea kwa chama. Uteuzi utazingatia kukieneza chama nchi nzima na kufuta kabisa dhana za ubaguzi kimikoa.

“Hapa tutakachofanya ni kuhakikisha kwamba maeneo mengi nchini yanapata uwakilishi katika viti hivi maalumu. Mahali chama kilipopata kura nyingi zaidi kitapata wabunge zaidi lakini tutaangalia pia kuenea kwa chama chenyewe,” amesema kiongozi mmoja wa CHADEMA.

Kigezo cha tatu kitakuwa elimu ambapo wagombea wenye elimu – kwa maana ya ujuzi na maarifa juu ya mambo mbalimbali kijamii na kisiasa – ndio watapewa kipaumbele.

Kigezo cha nne kitakuwa ni uzoefu ndani ya taasisi. Hii ina maana kwamba wale ambao tayari wana uzoefu wa kufanya kazi katika sehemu mbalimbali watakuwa na nafasi kuliko wale wasio na uzoefu kabisa au wenye uzoefu kidogo.

Aidha, chama kitaangalia rekodi ya wagombea katika kukichangia chama hicho – huku wale waliowahi kukichangia chama – kwa aina mbalimbali – katika siku za nyuma wakipewa nafasi kuliko wachangiaji wapya au wale ambao hawajawahi kukichangia kwa namna yoyote ile.

“Hapa, kikubwa tunachotaka kukiona ni kuhakikisha kwamba asiyefanya kazi na asile. Haiwezekani mtu ambaye ametumikia chama na kuhenya kwa miaka mingi na kwa njia mbalimbali, awe na fursa sawa na yule anayeanza leo,” gazeti hili limeelezwa.

Kigezo cha sita kitakachoangaliwa na timu teule ni kutoa kipaumbele kwa wagombea walioshiriki kuwania ubunge kwenye majimbo ya uchaguzi.

Hatua hii, gazeti hili limeambiwa, ina maana kwamba wagombea wanawake waliowania ubunge kwenye majimbo ya uchaguzi, wana nafasi kubwa ya kupata ubunge wa viti maalumu kuliko wale ambao hawakuwania nafasi hiyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: