Dk. Slaa: Serikali haiaminiki


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Dk. Willibrod Slaa

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amesema serikali ya Rais Jakaya Kikwete haiaminiki tena machoni mwa wananchi na jumuiya ya kimataifa.

“Tumewaeleza siku nyingi viongozi wa CCM (Chama Cha Mapinduzi), kwamba wananchi hawana tena imani nao. Hiki ndicho ambacho leo kampuni ya nje imeona,” anaeleza Dk. Slaa.

Dk. Slaa alikuwa akihojiwa na gazeti hili juu ya kampuni ya British Aerospace Systems (BAE) ya Uingereza iliyoiwekea masharti serikali ya Tanzania jinsi itakavyorejesha mabilioni ya shilingi yaliyokwapuliwa kupitia ununuzi wa rada ya kijeshi.

Amesema, “Watu wa nje ambao wametuibia, nao hawana imani tena na wezi wenzao waliopo ndani ya serikali ambao waliwarahisishia uuzaji wa rada kwa bei iliyopitiliza. Hii ndiyo tafsiri ya msimamo wa kutotaka kurejesha fedha hizo kupitia mikono ya serikali.”

“Hii maana yake ni kwamba wizi kupitia ununuzi wa rada uliofanywa na baadhi ya vigogo waandamizi serikalini, umevunja hadhi ya Rais Jakaya Kikwete na serikali yake machoni mwa wananchi na jumuiya ya kimataifa,” ameeleza.

Alhamisi iliyopita, serikali kupitia waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe ilitoa wito kwa wale iliowaita “wananchi wazalendo na wenye nia nzuri kwa taifa hili,” kusimama na serikali yao kupinga “udhalilishaji” wa kampuni ya BAE.

Wito wa serikali ulitolewa bungeni mjini Dodoma kufuatia BAE kusema itapeleka fedha hizo kwa asasi za kijamii za Uingereza ili ziangalie jinsi ya kuzitumia kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania na siyo  kuzikabidhi kwa serikali.

Rada ambayo ilinunuliwa kwa zaidi ya dola za marekani 60 milioni, kupitia mawakala wa ndani na nje, ilikuwa inagharimu kiasi kidogo zaidi kuliko walichotoza. Hivi sasa BAE inapaswa kurejesha dola za Marekani 20 milioni, karibu sawa na Sh. 30 bilioni za Tanzania.

Kauli ya Dk. Slaa inashabihiana na ile ya kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya CCM aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa gazetini. Amesema serikali haipaswi kung’ang’ania kurejeshwa fedha hizo nchini kwa kuwa haikufanya juhudi zozote katika kuziokoa.

Kada huyo aliyeongea kwa sauti ya uchungu alisema, “Waingereza wamesaidia katika kufanya uchunguzi na kugundua kuna rushwa ya dola za Marekani 19 milioni. Lakini serikali imeshindwa kuchukua hatua. Leo wanaibuka na kusema wanataka wapewe fedha zilizookolewa. Hii si sahihi.”

Amesema, “Serikali imeshindwa kuchunguza. Imeshindwa kukamata wahusika. Imeshindwa kufungua mashtaka na imeshindwa kupeleka watuhumiwa mahakamani. Katika mazingira haya, serikali inapata wapi ujasiri wa kudai fedha hizo,” anahoji.  
Kuhusu serikali kuanza sasa kudai fedha hizo kwa kiwewe, Dk. Slaa amesema hicho ni “kichekesho.”

Amesema, “Kutokana na yaliyofanyika, Uingereza ina haki ya kuamua njia ya kurejesha fedha hizo nchini. Serikali imezembea katika suala hili na hakuna uhakika iwapo fedha hizo zikirejeshwa kwake zitatumika ipasavyo.”

Dk. Slaa amesema kwa muda wote wa kashfa hii, serikali haijaonyesha dhamira safi ya kushughulikia ufisadi; na kwamba imeshindwa hata kupeleka watuhumiwa mahakamani. Kwa msingi huo, amesema hana sababu ya kupinga fedha hizo kuelekezwa moja kwa moja kwa jamii.

“Eti serikali inataka kutumia fedha hizo kununulia madawati; kama hiyo ni kweli mbona walikuwa hawajazihangaikia? Mbona hawasemi yalipo mabilioni mengine ya shilingi yaliokwapuliwa na makampuni ya Meremeta, Deep Green Finance Limited, Kagoda na Tangold?” amehoji.

Amesema, serikali ya Rais Kikwete haikufanya juhudi zozote kuhakikisha “…fedha zetu zinaokolewa. Hata pale ambapo ilishinikizwa kupeleka watuhumiwa mahakamani, iliishia kumfungulia mashitaka mmoja wa watuhumiwa ambaye hata hivyo hajulikani aliko.”

Kwa zaidi ya miaka saba sasa wanaharakati mbalimbali wakiwamo vyombo vya habari na wanasiasa wa upinzani, wamekuwa wakikaba koo serikali kutaka kufikisha mahakamani wote waliotuhumiwa kula rushwa kwenye ununuzi wa rada.

Miongoni mwa waliotuhumiwa na wamo kwenye orodha ya Shirika la Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai la Uingereza (SFO), ni aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Andrew Chenge na mfanyabiashara wa asili ya kiasia, Sailesh Vithlani.

Wengine ni aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Taifa (BoT), Dk. Idris Rashid; aliyekuwa katibu mkuu wizara ya fedha, Gray Mgonja na baadhi ya watendaji serikalini na katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Chenge ndiye alikuwa mshauri wa serikali katika kuridhia ununuzi wa rada, tena kwa kutumia sheria ya Uingereza badala ya sheria za Tanzania.

Aidha, Chenge alikubali akaunti za BoT zishikiliwe jijini London, ili iwapo serikali ya Tanzania ingechelewa kulipa deni hilo, na mahakama ikaamua kuwa ni lazima ilipe; basi iwe rahisi kwa kampuni ya BAE kuchukua fedha zake.

Ripoti ya SFO ambayo nakala yake anayo pia Rais Kikwete inasema,   “maamuzi haya mawili – kutumia sheria za Uingereza na kuhamishia akaunti ya BoT nje ya nchi – hayakuwa na maslahi kwa taifa wala kwa maendeleo yake kiuchumi… Chenge alihatarisha maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa kufanya maamuzi hayo.”

Kama kawaida, Rais Kikwete hakuchukua maamuzi magumu au hata mapesi kukabiliana na wizi ulioripotiwa na shirika la Uingereza.

Makachero wa SFO wanaamini kuwa Chenge asingeweza kufanya mambo hayo makubwa bila kushawishiwa kwa mlungula kwa vile, “mambo hayo hayakuwa na maslahi kwa taifa na ni ya hatari.”

Akizungumzia madai ya serikali kuwa imedhalilishwa kutokana na hatua ya kampuni hiyo kung’ang’ana na fedha hizo, Dk. Slaa amesema, “Nani amedhalilisha serikali? Imejidhalilisha yenyewe. Ni yenyewe iliyoshindwa kukamata watuhumiwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Sasa hadi hapo nani anaweza kusema kuwa sisi tumedhalilishwa?” amehoji.

Fedha za rushwa ili kulainisha watendaji serikalini wakati wa ununuzi wa rada, zinadaiwa kupitia akaunti ya kampuni ya Chenge iliyoko katika benki ya Barclays, tawi la Jersey, nchini Uingereza.

Ripoti ya SFO inasema Chenge, kupitia kampuni yake ya Franton Investiment Ltd., alipokea dola za Marekani milioni 1.5 (karibu Sh. 2.5 bilioni) kutoka madalali wa ununuzi wa rada.

Kuhusiana na hongo ya BAE, makachero wa SFO wanaeleza katika ripoti yao kwamba, Chenge alimmegea Dk. Idris Rashid kiasi cha dola za Marekani 600,000 (Sh. 1.2 bilioni) kwa lengo la “kumlainisha.”

Taarifa zinasema ugawaji fedha za mlungula kuhusiana na rada ulifanyika kati ya 19 Juni 1997 na 17 Aprili 1998.

Katika ripoti yake ya kurasa kumi na moja, SFO wanasema, “Hatua ya Chenge kupeleka fedha kwenye akaunti ya Dk. Rashid kunaonyesha si tu alipokea mlungula kwenye suala hilo, bali pia yeye ndiye alikuwa msambazaji wa rushwa ya rada kwa wengine,” inasema taarifa ya SFO ya Machi 21 mwaka 2008.

Kuhusu wabunge wa Bunge la Muungano kwenda nchini Uingereza kwa kile kinachoitwa “kushawishi urejeshwaji wa fedha hizo kupitia mikononi mwa serikali,” Dk. Slaa anahoji, “Nani aliyewatuma?”

“Hawa watu wametumwa na nani kutumia fedha za umma kwenda Uingereza kutafuta fedha hizo? Serikali hii imekuwa kiziwi; haiwasikilizi hata wabunge ambao wametaka mara kadhaa kuchukuliwa hatua madhubuti dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi. Sasa leo tunaambiwa wametumwa kwenda Uingereza. Kufanya nini,” amehoji.

Alipoulizwa mbona uwakilishi wa wabunge hao umetokana na vyama vyote, Dk. Slaa alikana chama chake kushirikishwa.

Alisema, “Sisi ndiyo tunaongoza upinzani bungeni. Wabunge wetu hawajashirikishwa. Chama chetu hakijashirikishwa. Sasa huo uwakilishi unatoka wapi,” ameshangaa.

Miongoni mwa wabunge wanaodaiwa kutumwa na serikali nchini Uingereza, kuna John Cheyo kutoka United Democratic Party (UDP) ambaye uteuzi wake haukushirikisha kambi ya upinzani.

Wengine ambao wote ni kutoka CCM, ni Job Ndugai (Kongwa) ambaye pia ni Naibu Spika, Mussa Azzan Zungu (Ilala) na Anjela Kairuki (Viti Maalum).

Gazeti hili lilipowasiliana na kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe kuhusu suala hilo, alisema “Sifahamu lolote juu ya hilo, zaidi ya kumsikia waziri Membe bungeni.” Alisema ofisi ya kiongozi wa upinzani haikuhusishwa katika safari hiyo ambayo Dk. Slaa amesema “haina maana.”

Mbowe amesema kwa ufahamu wake, hakuna kikao chochote ambacho yeye amehudhuria ambako jambo hilo limezungumzwa.

Kada wa CCM amesema, “Kuna maswali mengi katika suala hili. Kwanza, kwa nini serikali haikunua rada hiyo moja kwa moja kutoka kwa mtengenezaji, na badala yake ikanunua kupitia wakala?”

Kada huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, amesema kimsingi katika suala hili la fedha za rada, anayepaswa kulaumiwa ni serikali yenyewe.

Katika mazingira haya, amesema “…tayari serikali ilishabariki kuzitupa? Kiwewe cha leo cha nini?”

0
Your rating: None Average: 4.4 (5 votes)
Soma zaidi kuhusu: