Dk. Slaa: Tutamshitaki JK


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Dk. Willibrod Slaa, Katibu Mkuu CHADEMA

RAIS Jakaya Kikwete anaweza kujiingiza katika mgogoro wa kisiasa na kidiplomasia, iwapo atashindwa kuchukua hatua za kuandika Katiba mpya na kuwa na tume huru ya uchaguzi, MwanaHALISI limeelezwa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeweka ajenda hizo mbili kwenye ratiba za nchi wafadhili waliokuwa wakihudhuria kikao cha ufunguzi wa Bunge la 10 mjini Dodoma, Alhamisi iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya CHADEMA, viongozi waandamizi wa chama hicho sasa wanaandaa safari za ndani na nje ya nchi “kuweka hoja hizi wazi kwa kila atakayejali kutusikiliza.”

Viongozi hao walikutana jijini Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita, kujadili jinsi ya kuhakikisha madai yao yanasikilizwa na kufanyiwa kazi.

Mkutano wa viongozi hao umeorodhesha madai makuu ambayo wanataka serikali kutekeleza ndani ya kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa.

Madai hayo, kwa mujibu wa mtoa taarifa, ni pamoja na kuandikwa kwa katiba mpya; na kuundwa upya kwa tume ya taifa ya uchaguzi.

Uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais ambao unalalamikiwa na CHADEMA kuwa uliendeshwa kwa hila ulifanyika mwishoni mwa mwezi uliopita.

“Ni kweli, viongozi wetu waandamizi wamekutana na kuweka mkakati wa kushinikiza serikali itekeleze madai yetu. Kwanza, tunataka serikali iandae mchakato wa kupatikana katiba mpya. Lengo ni kupatikana katiba mpya kabla ya uchaguzi mwaka 2015,” ameeleza mtoa taarifa.

Pili, “Tunataka serikali iunde upya tume ya ya taifa ya uchaguzi na tatu, serikali ikubali kuunda tume huru ya kuchunguza wizi wa kura.”

Taarifa zinasema miongoni mwa mambo ambayo yamepangwa kutekelezwa na viongozi hao wakuu katika kushinikiza madai hayo, ni kufanya mikutano ya ndani na nje ya nchi.

“Tumepanga kufanya mikutano ya ndani katika mikoa na wilaya mbalimbali, pamoja na kuendesha makong’amano na warsha. Lengo ni kuhakikisha kabla ya uchaguzi mkuu mwingine kufanyika, katiba mpya na sheria mpya za uchaguzi ziwe zimepatikana,” ameeleza mtoa taarifa.

Amesema wamekubaliana kutengeneza timu itakayotembelea nchi mbalimbali ili kueleza kile ambacho CHADEMA inasisitiza na kusimamia.

Anasema mpango rasmi wa utekelezaji wa mkakati huo utafikishwa katika kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao.

Mtoa taarifa anasema, CHADEMA kimepanga kushinikiza madai yake kwa njia ya amani.

Mkakati wa kushinikiza serikali kutekeleza madai ya CHADEMA umekuja baada ya Dk. Willibrod Slaa kutangaza kutotambua matokeo yaliyompa urais Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama chake, Kinondoni Dar es Salaam, siku moja kabla ya matokeo kutangazwa, Dk. Slaa alisema yeye na chama chake hawatayatambua matokeo yatakayotangazwa.

Dk. Slaa alisema msimamo wa kutotambua matokeo hayo kunafuatia matokeo mengi ya urais “kusheheni udanganyifu, vikiwamo vitendo vya wizi wa kura.”

Ni katika mpangilio huo wa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi wa rais, Alhamisi iliyopita, wabunge wa chama hicho walitoka nje ya ukumbi wa bunge mara baada ya rais Kikwete kuanza kuhutubia Bunge.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya serikali, hatua ya wabunge wa CHADEMA kumsusia Rais Kikwete, kimestua baadhi ya nchi wahisani, na inatarajiwa muda wowote serikali itaweza kulitolea tamko.

MwanaHALISI lilipowasiliana na Dk. Slaa ili kupata undani wa taarifa hizi alikataa kuingia kwa undani kuzungumzia suala hilo, badala yake alisema, “Daima mtaji wa CHADEMA ni watu.”

Alisema CHADEMA tayari kimekusanya ushahidi wa kutosha wa kuonyesha jinsi wizi wa kura ulivyofanyika, wapi na nani waliohusika.

“Tutangaza muda wowote kuanzia sasa, wote waliohusika na wizi wa kura. Tutaeleza kwa mapana jinsi kura zilivyoibwa na mbinu iliyotumika na kwa nini tunaendelea na msimamo wetu wa kutoyatambua matokeo. Nakuomba uvute subira, utapata kila kitu,” alieleza.

Alisema kwa sasa, hayuko tayari kueleza hilo kwa kuwa jukumu hilo limehama kutoka mikononi mwake kama mgombea na limechukuliwa na chama chake.

“Subiri tumalize mkutano wa Kamati Kuu. Baada ya mkutano huo, ndipo tutakapojua nini kifanyike,” ameeleza.

Huku Dk. Slaa akieleza hayo, taarifa kutoka Dodoma zinasema aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa alikwenda ofisi za kiongozi wa upinzani bungeni kuwaomba CHADEMA wasisusie hotuba ya Kikwete.

Taarifa zinasema Lowassa alikutana na mwenyekiti Freeman Mbowe na Zitto Kabwe na kuwaambia kuwa amekwenda kuwaona lakini hakutumwa na kiongozi yoyote kujadiliana nao, isipokuwa yeye binafsi.

Lowassa alikutana na viongozi wa CHADEMA siku moja kabla ya wabunge wa chama hicho kumkacha Kikwete na kuwaambia kuwa mpango wao ungetia doa mbele ya jumuiya ya kimataifa.

Kukana kwa Lowassa, kwamba hajatumwa na Kikwete kulifuatia Mbowe kumuuliza, “Mheshimiwa Lowassa, umetumwa au umekuja mwenyewe?”

Mbowe amethibitisha kukutana na Lowassa, lakini alisema katika mazungumzo yao, Lowassa alieleza mara mbili kuwa hajatumwa na yoyote kuwaona na kujadiliana nao juu ya suala hilo.

Hata hivyo safari yake haikuzaa matunda, hata kama alikuwa ameagizwa na Kikwete.

Kwa mujibu wa watu waliokaribu na Zitto, kabla ya Lowassa kukutana na viongozi wa CHADEMA alifanya majadiliano ya kina na Zitto ambaye ndiye aliyempeleka ofisini kwa Mbowe.

Ni Zitto aliyekacha kuingia bungeni kwa madai kuwa angeingia na kutoka, angemfedhehesha rais.

Wachunguzi wa mambo wanasema tatizo la Zitto ni kujipendekeza, kwani kama angetaka “kumheshimu” Kikwete, angeingia bungeni na wakati wenzake wanatoka, yeye angebaki ameketi. Hakufanya hivyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: