Doa lisilofutika


editor's picture

Na editor - Imechapwa 12 May 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TANZANIA imeingia doa. Ripoti ya Taasisi ya Freedom House imeiweka katika kundi la nchi zilizoshindwa kutambua uhuru wa vyombo vya habari mwaka 2008.

Taasisi hii ya Marekani inafanya tathmini ya viwango vya uhuru wa vyombo vya habari. Ripoti yake hutoka kila mwaka sambamba na maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari duniani, Mei 3.

Tanzania imewekwa kundi moja na Afrika Kusini, Botswana, Chad, Congo-Brazzaville, Lesotho, Madagascar na Senegal.

Kejeli ni kwamba Angola, Comoro, Liberia na Sierra Leone – nchi zilizotulia majuzi tu baada ya kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi – kuwa ni miongoni mwa zilizopiga hatua.

Taifa hili lilijenga historia nzuri ya umoja na mshikamano na kuwa mbele katika kupigania haki za Waafrika waliokuwa wakikandamizwa.

Lilitumia raslimali nyingi kusaidia harakati za ukombozi na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Inakuwaje serikali yake ikandamize uhuru wa vyombo vya habari?

Vyombo vya habari ni nyenzo muhimu katika utawala bora na heshima kwa haki za binadamu. Penye watu walio huru katika kujieleza na kupata habari, pana nafasi ya amani na maendeleo.

Tanzania ilifeli mwaka jana katika jambo hili; itajivuna vipi kutekeleza vizuri Malengo ya Milenia (MDGs) wakati serikali yake haijali watu wake kuwa huru kihabari?

Baada ya kuingia madarakani kwa mbwembwe nyingi Desemba 2005, kufuatia ushindi uliochangiwa sana na vyombo vya habari, serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete ililala usingizi wa pono.

Ni vyombo vya habari ambavyo vimeibana serikali na hata kuionyesha njia. Ni vilio na sauti za kudai haki za wananchi ambazo zimeitoa serikali usingizini ingawa imekataa kuchukua hatua kwa wahusika.

Lakini Oktoba mwaka jana serikali ilikamilisha ujabari wake kwa Waziri wa Habari, George Mkuchika kufungia MwanaHALISI licha ya kujua fika linategemewa na mamilioni ya Watanzania kwa taarifa zake.

Waziri alifanya hivyo bila kujali kuwa uamuzi huo ulitokana na matumizi ya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 iliyokwishatajwa kuwa ni kandamizi. Baada ya kibano kutoka ndani na nje ya nchi hatutarajii serikali kufanya makosa hayo tena.

Tunataka serikali inayojali na kuthamini uhuru wa raia wake; serikali inayotii kauli ya umma; isiyotaka kutuziba macho na midomo. Kwani katika kifo cha uhuru kuna kifo cha serikali.

0
No votes yet