Dowans ina harufu ya Lowassa


Owawa Stephen's picture

Na Owawa Stephen - Imechapwa 11 March 2009

Printer-friendly version
Tafakuri
Edward Lowassa

TAREHE 7 Februari 2008 aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa alilazimika kuachia ngazi nafasi hiyo kutokana na kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond Development Company (LLC).

Ilibainika na Lowassa akajikuta katikati ya mgogoro mkubwa wa kushiriki kuingiza serikali katika mkataba, kwa njia ya upendeleo, na kampuni hiyo iliyogundulika baadaye kuwa haikuwa na uwezo kiufundi na kifedha.

Katika hatua ya juu ya kufichuka kwa mambo, Richmond iligundulika kuwa “kampuni feki” na kufutwa katika orodha ya makampuni nchini. Kabla ya kufutwa, Richmond ilikabidhi mkataba wake kwa kampuni ya Dowans ambayo nayo haikutimiza masharti ya ufuaji umeme katika muda ulikubaliwa.

Bunge la Muungano, baada ya Kamati yake teule kufanya uchunguzi juu ya Richmond, liliridhika kuwa kampuni hiyo ilikuwa feki na kwamba mawaziri na maofisa wengine wa serikali walihusika katika kashfa hiyo.

Wakati mapendekezo ya bunge kwa serikali, ya kuwachukulia hatua wote waliohusika na ufisadi wa Richmond hayajatekelezwa, serikalai na shirika lake la umeme, TANESCO wanakuja na hoja ya kununua mitambo ya Dowans.

Na mitambo ya Dowans ni mitambo ya Richmond; mikuukuu, iliyoletwa na kampuni feki iliyoingia mkataba batili kwa kutumia uwongo mwingi na kughushi. Ni mitambo hii iliyomwachisha kitumbua Edward Lowassa.

Serikali na TANESCO wanakuja kwa kasi kuwa umeme utazimika kote nchini; hivyo lazima mitambo iliyopo ya Dowans inunuliwe mara moja ili “kunusuru” taifa kukaa gizani.

Inachekesha na kusikitisha pia. Je, kwa nini TANESCO hawajafanya utafiti na tathmini kwa muda wote huo na kujua wapi wanaweza kupata mitambo mipya ya kuweza kukidhi mahitaji ya uzalishaji wa umeme kuanzia pale maazimio ya Bunge yalipopitishwa?

Je, menejementi ya TANESCO ina majibu gani ya kuinusuru nchi kutoingia gizani tofauti na kununua mitambo ya Dowans?

Ni njia ipi mbadala ambayo TANESCO imepanga kukabiliana na upungufu wa umeme? Ni kweli kwamba katika hili, hakuna mkono wa wamiliki wa Dowans unaotumika kuwasukuma wabunge kukidhi matakwa ya TANESCO na maswahiba wao Dowans?

Serikali na TANESCO kwa ujumla wanatakiwa kuwa na majibu ya maswali hayo. Hatutarajii majibu mepesi ya kuwa ni lazima tununue mitambo iliyopatikana kwa njia ya kifisadi ili tuepeshe nchi na giza.

Hakuna njia yoyote ile ya kuweza kuhalalisha uharamia huo machoni mwa Watanzania. Hatua yoyote ya kununua mitambo ya Dowans ni kunufaisha mafisadi na kuwageuza Watanzania makatuni wasiokuwa na akili na wanaoweza kufanyiwa kitu chochote kibaya ili mradi tu kimeamuliwa na wanaojiita viongozi.

Lazima Tanzania kama taifa huru liwe na maamuzi yake na yaheshimiwe, kusimamiwa na kutekelezwa kwa manufaa ya wengi.

Kulikuwa na umuhimu gani wa kutumia pesa za umma na muda kwa kuunda Kamati ya Bunge na kuchunguza mkataba wa Richmond?

Au wanataka kutuambia hapa kwamba Bunge haliendeshwi kwa kufuata sheria na kanuni, badala yake linaendeshwa kwa majungu, fitina, hisia na chuki?

Kwa mtazamo huu, Watanzania watarajie vituko vingi kutoka kwa wabung na serikalini kwa ujumla; kwa maana ya kukubaliana kupiga kelele bungeni na baadae kujutia kelele zao.

Kama serikali inataka kushughulikia ufisadi kwa dhati, ni vema ichukue hatua zifuatazo kuhusiana na mtambo wa Richmond/Dowans.

Kwanza, kutaifisha mitambo hiyo kwa manufaa ya taifa kwa sababu serikali ina misingi ya kisheria kuwa mitambo ililetwa kwa ulaghai.

Pili, kuna vipengele vya sheria vya manunuzi vilikiukwa wakati wa ununuzi wa mitambo yenyewe; ikiwa ni pamoja na udanganyifu uliofanywa na aliyepewa zabuni ya kuingiza mitambo hiyo.

Tatu, imethibitika kuwa kuna makosa ya jinai yanayotokana na kughushi nyaraka yaliyofanywa na mtu aliyejitambulisha kama mwakilisha wa Dowans nchini.

Nne, kwa kuwa Richmond ndiyo ilivunja mkataba kwa kushindwa kutimiza masharti, basi serikali haitakuwa imefanya makosa kuvunja mkataba.

Tano, uchunguzi ufanywe kubaini mahusiano yaliyopo kati ya watendaji wa TANESCO, wabunge wanaojiita wazalendo na mmiliki wa Dowans.

Sita, TANESCO watoe taarifa ya ukweli na ya kina kuhusu ni lini wamegundua upungufu unaotajwa wa umeme na wamechukua hatua gani kukabiliana nazo kama mitambo ya Richmond na Dowans isingekuwepo?

Bila kufanya haya, Tanzania itazidi kukidhi matakwa ya mafisadi waliopanua midomo yao kama mamba wakisubiri kodi ya Watanzania itakayotumika kama sadaka kununua mitumba ya Richmond na dada yake Dowans.

Wale wanaotaka kununua mitambo ya Richmond na Dowans, wana njama ya kumsafisha Edward Lowassa na mawaziri Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.

Hili wananchi wengi wameshang’amua na huu ni mradi mchafu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: