Dowans inatusukuma kudai katiba mpya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
Rugemeleza Nshala, mwanasheria na mwanaharakati

WATANZANIA wanatakiwa kulipa Sh. 94 bilioni ambazo Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) imeitunuku kampuni ya Dowans kwa mkataba wake na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukatishwa.

Adhabu hiyo inalalamikiwa na Watanzania wa kada mbalimbali: wasomi, wanaharakati katika nyanja tofauti, wanafunzi, wanasiasa na hata wananchi wa kawaida ambao ndio walipa kodi masikini nchini.

Wanasema si adhabu ya haki. Wapo wanaoita hatua hiyo kama mipango ya mtandao wa kifisadi kuinyonya Tanzania. Wanaibana serikali isilipe fedha hizo kwa kuwa tangu awali, mkataba wa Dowans ulikuwa na utata.

Rugemeleza Nshala ni mwanasheria na mwanaharakati mmojawapo. Anasema adhabu hiyo ingeweza kuepukika iwapo Katiba ya Tanzania ingekuwa imara.

Katika mazungumzo yake maalum na MwanaHALISI jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Nshala, amesema nchi nyingi katika Afrika haziwezi kupata haki kwenye mahakama za kimataifa kwani hazikushiriki kuanzisha.

“Hii mahakama ilianzishwa mwaka 1923 wakati nchi zetu nyingi zilikuwa hazijapata uhuru. Wakoloni ndio walianzisha kwa lengo la kunyonya makoloni yao.

“Wenzetu wa Amerika ya Kusini wamefanya maamuzi zamani sana kwamba mambo yao ya ndani hayataamuliwa na mahakama hizi. Sisi Tanzania tulipaswa kufuata mfano wao,” anasema.

Nshala anasema nchi hizo, ikiwemo Brazil ambayo ni moja ya nchi zenye uchumi mkubwa katika eneo hilo, zimeweka kitu kiitwacho “Andiko la Calvo” – Calvo Doctrine – ndani ya katiba zao.

Andiko hilo, anasema, linakataza hatua yoyote ya mambo ya ndani ya moja ya nchi hizo kuamuliwa nje ya Amerika ya Kusini.

Andiko hilo linatokana na Carlos Calvo, mtaalamu wa sheria wa Argentina ambaye ndiye aliliandika mwaka 1868. Calvo ndiye aliyetoa mapendekezo ya kuwepo tamko la kisheria ndani ya katiba zao litakalozuia mahakama za nje ya Argentina kuwa na nguvu kimaamuzi kuhusu suala lolote nchini Argentina.

“Kama mwekezaji amekuja nchini kwako, ina maana anakubaliana na sheria zenu. Kama kuna mgogoro wowote, itabidi uamuliwe kwa kutumia sheria za nchi zenu badala ya kupeleka mgogoro huo nje. Hiyo ndiyo dhana ya andiko la Calvo,” anasema.

Nshala anasema laiti Tanzania ingeweka kipengele kama hicho katika katiba yake, mgogoro uliohusu Dowans ungepaswa kubaki na kuamuliwa nchini.

“Wakoloni walianzisha ICC kwa lengo la kulinda maslahi yao. Ndiyo maana makampuni yanayotoka kwao yanakimbilia huko… wanajua huko watashinda,” anasema.

Anasema mahakama za aina ya ICC zilianza kupata nguvu kubwa miaka ya 1990, lengo likiwa ni kuvunja maendeleo yaliyoanza kupatikana katika baadhi ya nchi huru za Afrika miaka ya 1970.

“Malipo au fidia zinazoamuliwa katika mahakama hizi huwa na sifa kuu tatu. Lazima yawe kamilifu, endelevu na yafanywe kwa haraka. Hiki ndicho wanachokitaka.

“Ukitaka kujua hila za mahakama hizi, utaona maamuzi yake hayakatiwi rufaa. Yaani hapa kama wameshasema Dowans tuwalipe, watalipwa tu. Hakuna cha rufaa wala nini,” anasema Nshala.

Nshala, mmoja wa wanasheria walioanzisha Chama cha Wanasheria wa Mazingira Tanzania (LEAT), anasema kesi ya Dowans ndiyo inachochea zaidi umuhimu wa Tanzania kupata katiba mpya.

Anasema kama serikali itakubali ipatikane katiba mpya yenye vipengele vinavyozuia serikali ‘kuliwa’ fedha kama inavyotakiwa na Dowans, itakuwa imeridhia jambo la maana.

“Katiba ni mama wa sheria zote. Mtu hata kama atakuwa hakubaliani na kitu, ataogopa kukiuka akijua huko atakuwa amevunja katiba. Na hili ni muhimu sana katika ulinzi wa rasilimali za nchi,” anasema.

Ingawa anakiri katiba iliyopo inao ulinzi wa raslimali za nchi, Nshala anasema tatizo kubwa ni usimamizi wa utekelezaji wa katiba.

Anasema ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vinazungumzia umuhimu wa maliasili ya nchi na haja ya kuilinda kwa faida ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Ibara inasema; “(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.

“(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Ndivyo isemavyo katiba. Je, tunao viongozi wanaoheshimu katiba? Nshala anahoji na kubainisha kwamba hilo ndilo tatizo kubwa nchini.

Viongozi wa kisiasa na maofisa serikalini wanaopewa dhamana ya kulinda raslimali za Watanzania hawatendi kwa kuzingatia umuhimu huo.

Anasema, “Vile viapo unavyovisikia pale wanapochaguliwa (au kuteuliwa), ni vya kinafiki kwani haviashirii kwamba wana moyo wa kuvisimamia katika utendaji wao wa kila siku.”

Nshala anasema pamoja na upungufu huo, umuhimu wa katiba mpya nzuri unabaki. Tukiwa na katiba mpya ambayo pia itaweka misingi ya kuwapata viongozi wetu na miiko ya uongozi, tutajihakikishia usimamizi makini wa raslimali zetu.

Anasema sehemu nyingine ambayo katiba mpya ya Tanzania itapaswa kuangalia ni kuifanya misingi ya katiba kuwa na nguvu ya kisheria.

India, anatoa mfano, misingi hiyo imekaziwa na mahakama na hivyo nayo (misingi ya katiba) ni sheria kamili. Hiyo ni tofauti na ilivyo Tanzania. Misingi ya katiba ipoipo tu.

Misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inasema; “Kwa kuwa sisi Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani

“Na kwa kuwa misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo serikali yake husimamiwa na bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi, na pia yenye mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila ya woga wala upendeleo wowote, na hivyo kuhakikisha haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa, na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu:

“Kwa hiyo basi, Katiba hii imetungwa rasmi na bunge rasmi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya Wananchi, kwa madhumuni ya kujenga jamii  kama hiyo, na pia kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inaongozwa na serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na ujamaa.”

Nshala alipata shahada ya kwanza ya sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1992. Alipata shahada ya uzamili katika Umuduji wa Mazingira (Environmental Management) katika Chuo Kikuu cha Yale nchini Marekani.

Kwa sasa anasomea shahada ya uzamivu (PhD) kuhusu Athari za Mabadiliko ya Kisera kwa Sekta ya Madini katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa LEAT mwaka 1994 na aliwahi kuwekwa rumande mwanzoni mwa miaka ya 2000 kutokana na utetezi uliokuwa ukifanywa na taasisi yake kwa wachimbaji wadogo wa madini katika eneo la Bulyanhulu waliodaiwa kufukiwa na serikali mwaka 1996.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: