Dowans kuifilisi Tanesco


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 15 December 2010

Printer-friendly version
Makao Makuu TANESCO

SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco) liko hoi kiuchumi na halikopesheki, MwanaHALISI imeelezwa.

Akizungumza katika mkutano wa 41 wa Baraza la Wafanyakazi wa Tanesco mjini Morogoro wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo alisema shirika lina hali “mbaya sana” kifedha.

Taarifa kutoka ndani ya shirika zinasema hali hiyo inayoendelea kwa muda mrefu sasa, inatokana na Tanesco kukabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni huku gharama za uendeshaji zikiongezeka kwa kasi.

Kwa sasa, mapato ya mwezi ya Tanesco hayazidi Sh. 30 bilioni.

Wakati linakusanya mapato hayo, lenyewe linatumia kiasi cha Sh. 566 milioni kila siku kulipa makampuni ya kufua umeme ya Songas na IPTL.

Fedha hizo hulipwa kama gharama za kuweka mitambo – Capacity Charge.

Jairo aliwaambia wafanyakazi wa Tanesco kwamba utekelezaji wa mkakati wa kupunguza matumizi yake lazima uanze huku shirika likifuatilia madeni inayodai wateja wake.

Alisema, “nilichokisema ni kwamba lazima wajitahidi kuliweka Shirika katika hali ya kukopesheka zaidi.”

Habari hizo zinaibuka wiki tatu tangu kufichuka kwa taarifa kuwa Tanesco imeshindwa katika shauri lililofunguliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi na kampuni ya Dowans Tanzania Limited.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo imeamuru Tanesco kuilipa Dowans Sh. 185 bilioni kutokana na kosa la kuvunja mkataba.

Mkataba wenyewe ni ule wa kufua umeme wa dharura ambao Dowans iliurithi kutoka kwa kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (RDC). Ulisainiwa mwaka 2006.

Kwa msingi huo, hata kama Tanesco itaamua kutumia mapato yake yote hayo, bado itachukua zaidi ya miezi sita kumaliza kuilipa Dowans.

Aidha, taarifa hizo zinakuja wakati Tanesco ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa umeme hivyo kulazimika kuendelea kuitegemea mitambo ya kukodi ili kuongeza umeme katika Gridi ya Taifa.

Kwa mfano, wakati mahitaji ya umeme kwa wateja wake ni Megawati (MW) 906, shirika lina uwezo wa kuzalisha megawati 705 tu.

Megawati hizo zinazalishwa kupitia mabwawa ya Kidatu (MW 204), Kihansi (MW 180), Mtera (MW 80), Pangani (MW 68), Hale (MW 21) na Nyumba ya Mungu (MW 8).

Umeme mwingine unapatika kwa nguvu za mitambo iliyopo katika vituo vya Tanesco vya Ubungo (MW 100) na Tegeta (MW 45).

Wakati uzalishaji wa umeme ukiwa megawati 705, mahitaji katika mkoa wa Dar es Salaam pekee, ni MW 455.

“Kimsingi, Tanesco inakabiliwa na hali mbaya sana kifedha na miundombinu. Uzalishaji hauendani na mahitaji. Naona hata hicho wanasiasa wanachokiita ‘kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha’, ni kiini macho,” amesema kiongozi mmoja wa Tanesco aliyekataa kutajwa.

Kadhalika, Tanesco inakadiriwa kuwa na malimbikizo ya madeni yanayofikia Sh. 700 bilioni.

Katika kukabiliana na ukata, tayari uongozi umewasilisha mapendekezo Mamlaka ya Usimamizi wa huduma za maji na nishati (EWURA), maombi ya kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 34.6 kuanzia 1 Januari 2011.

Tanesco wanataka ongezeko jingine la bei la asilimia 13.8 litolewe kwa mwaka 2012 na ongezeko la tatu la asilimia 13.9 litolewe kwa mwaka 2013.

Kwa hali hiyo, bei inayopendekezwa EWURA kuanzia mwakani kwa wateja wadogo wanaotumia nishati hiyo chini ya kWh 40 kwa mwezi, ni Sh. 2,692 kutoka Sh. 2,000.

Hiyo maana yake ni watumiaji wa umeme nchini kulazimika kulipa kiasi cha Sh. 692 zaidi kwa kila Kwh kulinganisha na bei ya zamani.

Gazeti hili limeelezwa pia kwamba kutakuwa na ongezeko la gharama kwa wateja watakaotaka kuwekewa mita za LUKU au kuunganishiwa umeme majumbani.

Taarifa zimesema mapendekezo ya bei mpya yaliyowasilishwa EWURA Agosti mwaka huu, yanasubiri uamuzi wa Bodi ya EWURA.

Bodi hiyo inatarajiwa kukutana wakati wowote kuanzia sasa kupitisha maombi hayo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: