Dowans: Matokeo ya serikali ya kifisadi


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 08 December 2010

Printer-friendly version

KILA ninapotafakari masuala mbalimbali, huishia kujiuliza, Je, katika mapambano yoyote yanayofanywa na binadamu (ya vita, ya siasa au mengineyo), Mwenyezi Mungu huwa anakaa upande gani – wa wanyonge au upande wa wababe?

Kwa nini machungu makubwa yaliyoibuka ghafla na yanayotukabili wananchi wa Tanzania kipindi hiki – hususan mgao wa umeme – hayakuibuka kabla ya uchaguzi?

Kama Mwenyezi Mungu alipanga kuyachelewesha, basi yumkini hakuwa upande wa wanyonge katika uchaguzi. Iwapo angeyatanguliza, bila shaka matokeo ya uchaguzi yangeathiri ule upande wa mshindi. Hapo wapenda mabadiliko wangepeta.

Mifano ipo. Wiki moja kabla siku ya uchaguzi mkuu wa Hispania Machi 2004, milipuko ya mabomu ilitokea ndani ya mabehewa ya treni katika stesheni ya Madrid; watu 191 walikufa na mamia wengine kujeruhiwa.

Serikali ya waziri Mkuu Jose Maria Aznar wa chama cha PP ilikimbilia kudai wahusika ni magaidi wa ETA wanaotaka Jimbo la Basque lijitenge. Lengo lilikuwa kulifanya tukio hilo ni ulipuaji wa kawaida uliokuwa ukitekelezwa na kikundi hicho kwa miaka mingi tu.

Serikali hiyo ilificha ukweli halisi kwamba ulipuaji huo ulifanywa na kikundi cha kigaidi cha Al-Qaeda. Kama ingesema ni Al-Qaeda wananchi wangeishutumu serikali kwa kusema hayo ndiyo matokeo ya serikali yao kupeleka majeshi kuiunga mkono Marekani katika vita yake nchini Iraq, kinyume cha matakwa ya Wahispania wengi.

Uchaguzi ulipofanyika, serikali ya Aznar ikaangukia pua. Iliyoingia ikawa ya Luis Rodriguez Zapatero. Iwapo tukio hilo la ulipuaji lingetokea baada ya uchaguzi, huenda Aznar angepeta katika uchaguzi.

Hapa kwetu kuna hukumu iliyotolewa wiki iliyopita na Baraza la Uluhishi wa Biashara Kimataifa (ICC) ya kuamuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuilipa kampuni ya Dowans Sh. 185 bilioni za fidia kutokana na kuvunja mkataba.

Kama hukumu hii ingekuja kabla ya uchaguzi, ingeweza kukiathiri chama tawala kwani wapinzani wangetumia kama agenda katika majukwaa ya kampeni – kuonyesha jinsi ufisadi unavyoliangamiza taifa.

Lakini hukumu hiyo huenda ilipangwa makusudi na wadau husika kwamba itoke baada ya uchaguzi ili isiathiri nafasi ya CCM kushinda uchaguzi huo kutokana na masuala ya ufisadi.

Tusisahau ‘mahakama’ ya usuluhishi iliyopo Ufaransa ni taasisi binafsi inayokubali kusikiliza mashauri kuhusu migogoro ya kibiashara baada ya pande husika kuridhia kusikilizwa nayo.

Kuna ripoti zilizosema kwamba maafisa wa Richmond waliokwenda kununua mitambo ya kufua umeme kwa kampuni ya General Electric ya Marekani walijaribu kushawishi maafisa wao kuongeza bei katika ofa waliyoitoa wakati TANESCO ikihitaji mitambo, kitu ambacho kiliwastua na ndipo harufu ya ufisadi wa Richmond ilianza kuvuja.

General Electric ni wakala wa serikali ya Marekani wa kutengeneza injini za ndege za kivita. Inawezekana Watanzania hao waliitazama General Electric kama vile BAE Systems ya Uingereza ambayo imethibitishwa kuhusika na ufisadi katika mipango ya kuuza bidhaa zake. Kama General Electric ilitaka kuingiliwa kifisadi, sembuse ‘mahakama’ hiyo ya usuluhishi?

Suala la hukumu iliyoinufaisha Dowans limezidi kuonyesha jinsi ufisadi katika sekta ya nishati uliofanyika katika miezi ya mwanzo tu ya kipindi cha kwanza cha uongozi cha Jakaya Kikwete unavyozidi kulitesa taifa.

Pia hukumu hiyo ni kielelezo tosha cha udhaifu wa serikali na vyombo vyake katika kushughulikia suala hilo.

Kitu kikubwa kinachoendelea kukosekana ni wahusika halisi kutochukuliwa hatua zozote za kimahakama, licha ya kuisababishia hasara kubwa serikali, katika uchumi wa nchi na machungu makubwa kwa watu wa kawaida.

Wiki iliyopita, gazeti moja la Tanzania lilichapisha katuni iliyoonyesha dhihaka ya serikali katika suala zima la usimamizi wa nishati nchini. Katuni ilionyesha ofisi ya Waziri wa Nishati na Madini ikiwa gizani na mshumaa wenye mwanga mdogo juu ya meza yake na maneno yalisema: “Karibu mheshimiwa, wewe ni mpya huna kosa.”

Hiyo ni dhihaka kubwa. Waziri anayezungumzwa si mpya, ni yuleyule William Ngeleja, aliyekuwepo ilipoibuka kashfa ya Richmond. Na Naibu wake ni yuleyule, Adam Kighoma Malima.

Kwa tafsiri yoyote ile, wawili hao wameshindwa kazi kwa kutokuwa na mbinu na ubunifu katika kuliokoa taifa katika aibu ya upungufu wa nishati hiyo muhimu. Sasa wamerudishwa katika nafasi walikopwaya. Nini maana yake? Taswira gani inajengwa hapa kutokana na uteuzi wao.

Wanaofahamu siasa za Tanzania, hii maana yake ni moja tu – wanazo siri nzito za kilichojiri katika sakata la Richmond na ndiyo haohao wanaotakiwa kuzilinda siri hizo.

Kama kumweka Dk. John Magufuli na Dk. Harrison Mwakyembe katika nafasi ya kusimamia Wizara ya Ujenzi kulilenga kusafisha wizara hiyo nyeti yenye harufu kubwa ya ufisadi, kwa nini asitafute watu wa aina hiyo kwa inayoonekana kuwa wizara ya Ngeleja na Malima?

Au Kikwete anataka kuonyesha kuwa anakosa watu wa kutosha walio waaminifu katika kupambana na ufisadi? Kama hiyo ndiyo hali, basi ni bora rais akajaribu kusahau wimbo wake wa vita dhidi ya ufisadi, na kwamba Watanzania tumekwisha.

Sasa kuna jitihada zinafanywa kuonyesha kuna baadhi ya wanasiasa wameibuka mashujaa katika sakata hilo la Richmond/Dowans – waliowahi kusema: “Si tuliwaambieni kwamba serikali iinunue mitambo ya Dowans?”

Kati ya hawa ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba. Kwa maana nyingine “ushujaa” huu ulijikita katika kuitaka serikali ikiuke sheria na kanuni zake kwa kununua mitambo chakavu.

Ilikuwa namna moja ya kuiokoa serikali katika harakati zake za kuendekeza na hivyo kuendeleza ufisadi na kuwapa kinga watu wa mwanzo waliotenda jinai hiyo.

Hata hivyo, Kikwete mwenyewe alionyesha kutaka kuendeleza hali. Mwishoni mwa Machi 2009, katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi kwa taifa alitoa kauli ya kuwataka wanasiasa kuacha malumbano kuhusu ununuzi wa mitambo ya Dowans, na hapohapo kuipongeza TANESCO kwa uamuzi wake wa kuachana na ununuzi wa mitambo hiyo.

Kauli hiyo iliripotiwa na gazeti moja kwa mbwembwe nyingi chini ya kichwa cha habari “JK apigilia msumari wa mwisho Dowans.” Kilichotokea sasa kinabadilisha mbwembwe kuwa machungu. Ni Dowans imepigilia msumari wa mwisho kwa JK.

Haya yote yametokana na jitihada za kimyakimya za serikali ya Kikwete kutaka kufunika ufisadi wa sakata la Richmond/Dowans tangu ulipolipuka. Jitihada za kwanza zilikuwa kubadilisha umiliki wa mitambo hiyo kutoka Richmond kwenda Dowans, hatua ambayo ilifikiriwa ingenyamazisha mambo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: