Dowans ni chuma ulete wa ikulu?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

HERI ya Mwaka Mpya wapenzi wasomaji wa safu hii ya Wazo Mbadala inatolewa wakati bei mpya ya umeme imeanza.

Katika salamu zake za Mwaka Mpya, Rais Jakaya Kikwete, alikomalia wananchi wakubali maumivu ya bei mpya zilizopitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kufuatia maombi ya Tanesco.

Rais anasema bei hiyo mpya ni kwa maslahi ya kibiashara au kiuchumi. Hapa rais ameficha ukweli.

Ukweli ni kwamba serikali yake ilipandisha bei ya umeme ilipotengeneza nyoka mfano wa ‘chuma ulete’ aitwaye Richmond ili kufyonza fedha za Watanzania masikini.

Hivi sasa ‘serikali ya Kikwete’ inachungulia namna ya kupokea Sh. 185 bilioni kama fidia ya ‘chuma ulete’ Dowans eti imeshinda kesi ilipozuiwa kufyonza fedha kupitia mkataba feki wa Richmond ambao iliruhusiwa kuurithi.

Rais anathubutuje kuzungumzia bei mpya bila ya kugusia athari za fidia hii? Je, huu si ushahidi wa kimazingira kwamba anahusika?

Mazingira ni haya: nyoka akiingia ndani ya nyumba, kimbilio la watoto na mama huwa kwa baba yao; kama hayuko mbali basi watatimua mbio kumfuata au kumtwangia simu arudi haraka kupambana na nyoka.

Watoto wanajua kwamba baba yao ana uwezo, mbinu na mikakati ya kumtoa nyoka bila kusababisha madhara kwa familia.

Lakini kama baba ataingia ndani ya nyumba na kupiga usingizi huku nyoka akionekana kuranda vyumbani na watoto wakiwa nje, familia yake itakuwa na jibu moja tu – kumbe baba ndiye mmiliki wa nyoka huyo.

Au kama baba ataonekana kukwepa kujadili tatizo au ugonjwa unaoathiri familia yake au anakataa kumpeleka mgonjwa hospitali au kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya kumpatia tiba, basi baba moja kwa moja ndiye mhusika wa ugonjwa huo.

Baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu Frederick Werema na Waziri wa Afrika Mashariki Samuel Sitta kutoa maoni yanayotofautiana kuhusu uhalali wa fidia kwa chuma ulete Dowans, masikio ya Watanzania yalibaki kwa ‘baba yao,’ Rais.

Sasa akakwepa. Hakuelezea. Badala yake, akakomalia watu walipe bei mpya. Jamii inamtilia shaka baba kwamba ameridhia chuma ulete Richmond/Dowans.

Haiwezekani katika mazingira haya, wananchi wajadili kwa miaka minne, kwa hisia kali, halafu Rais anakwepa na anaingia Ikulu kupiga usingizi!

Anathubutuje kulala kwa raha zake, wakati Richmond/ Dowans imeitikisa nchi na kusababisha anguko la kisiasa kwa msaidizi wake mkuu na rafiki yake mkubwa, Edward Lowassa? Kikwete anaamini Lowassa ameridhika?

Au zilikuwa mbinu za kifisadi kwamba mradi huo wa kifisadi ukijulikana “mmoja ajiuzulu na tuseme hiyo ni ajali ya kisiasa?”

Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa chini ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ilitumia mabilioni ya shilingi kwa safari ya Marekani kuchunguza nyaraka muhimu na kuhoji watendaji wakuu.

Kamati hiyo ikawasilisha ripoti yake, lakini haikumtaja mmiliki isipokuwa ilisema ni kampuni feki na kwamba serikali iliingia mkataba wa kufua umeme na kampuni feki.

Mjadala ulipopamba moto na kamati hiyo kurushiwa tuhuma kuwa ililenga kuchafua watu, Dk. Mwakyembe alisema wako radhi kueleza hata mambo waliyoyaacha ambayo yangeikomoa serikali.

Je, nani aliokolewa? Hii ndiyo sababu Dk. Mwakyembe kazibwa mdomo kwa kupewa uwaziri? Ndiyo sababu aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta naye kapewa uwaziri ili asiruhusu mijadala mikali bungeni?

Je, Kikwete atapuuza kwa kusema “…kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala usingizi” au atajifariji kwa kusema “mtapambana lakini hamtashinda?”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: