Dowans wasilipwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

WANASIASA wanataja Dowans. Wanaharakati wanataja Dowans. Vyombo vya habari tunataja Dowans.

Hata wasiopenda Dowans kutajwa sana, na wenyewe wamo kuitaja Dowans. Dowans ni tatizo. Tatizo juzi, ni tatizo jana, ni tatizo leo. Dowans itakuwa tatizo hata kesho.

Tatizo kubwa kuhusu Dowans ni kwamba suala linalowahusu “watu hawa” na namna linavyogusa maslahi ya Tanzania na watu wake, halijawekwa sawasawa.

Iliingia katika njia tata na sasa inatakiwa ivune wakati haina ilichokipanda kihalali. Hivi Dowans imetokea wapi?

Kama Dowans wenyewe ndio wale waliorithi kinyemela mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura uliosainiwa na serikali mwaka 2006 pamoja na Richmond, basi wananchi wana haki na sababu ya kushtushwa na malipo ya Sh. 94 bilioni.

Lakini, sasa kumekuja jipya: Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinataka serikali ilipe Dowans mabilioni hayo yaliyoamriwa na mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya biashara (ICC).

CCM iliyomaliza kikao chake cha Kamati Kuu, imetoa tamko ikisema malipo hayo kwa Dowans hayakwepeki maana ni “suala la kisheria.”

Tunataka maelezo zaidi. Chama kiseme kwanini kinataka sheria zifuatwe leo wakati hazikufuatwa jana? Kama kina nia njema na kinajali maslahi ya nchi, kwanini hakikusikika kuhimiza sheria zifuatwe wakati wakuu wake walipokuwa wanahaha kuipenyeza Richmond ipewe mkataba hata bila ya kuwa na sifa na uwezo?

CCM ilikaa kimya wakati Richmond inanyatia mkataba; ikaendeleza kimya mkataba huo ulipohamishwa kifisadi kwa Dowans; na ikakaa kimya hata baada ya Bunge kubaini uchafu uliofanywa kuhusiana na utaratibu mzima wa kusaini mkataba na kuuhamisha.

Katika hali kama hiyo, haikubaliki CCM inapotoka hadharani wakati huu genge la wajanja wachache linapojitahidi kugida mabilioni kutoka mfuko wa serikali ya Watanzania.

Tunasema wakuu wa CCM ambao kwa bahati mbaya baadhi yao ndio wanufaikaji wa uchafu uliofanywa kuneemesha Richmond/Dowans, wabadilishe msimamo kwa kuitaka serikali isilipe Dowans maana ikilipa itakwenda kinyume na maslahi ya nchi.

Na kama kweli CCM inaheshimu utawala wa sheria, basi ihimize na kuibana serikali kumlipa Vhalambia aliyeshinda kesi hadi Mahakama ya Rufaa Tanzania dhidi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na malimbikizo ya walimu nchini.

Kwa kuwa suala la Richmond/Dowans linaihusu CCM haiwezi kuwa mbele katika kushadidia malipo huku ikidharau maoni ya umma unaoona haistahili malipo hayo kufanywa kwa vile kashfa iliyohusu suala hilo haijapatiwa ufumbuzi wake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: