DPP Feleshi: Kagoda itakumwagia upupu


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version
Gumzo

MKURUGENZI wa Mashitaka wa Makosa ya Jinai nchini (DPP), Eliezer Feleshi amenukuliwa akisema ameshindwa kufikisha mahakamani wamiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited kwa kuwa hafanyi “kazi kwa shinikizo la wanasiasa.”

Amesema ofisi yake haina ushahidi wa kutosha wa kuwezesha Kagoda kufikishwa mahakamani na kwamba hilo litawezekana iwapo makampuni ya nje yanayodaiwa kuipa kazi Kagoda yatapatikana na kutoa ushahidi.

DPP amesema hawezi kufanya kazi kwa utashi wa kisiasa au wananchi wanavyotaka na kwamba hadi sasa hakuna ushahidi wa kupeleka Kagoda mahakamani.

Alisema atafanya hivyo baada ya kujiridhisha kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kuipeleka Kagoda mahakamani.

Kampuni ya Kagoda ilikwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wiki moja baada ya kusajiliwa.

Kauli ya Feleshi imetolewa ikiwa ni takriban mwaka mmoja tangu Rais Jakaya Kikwete aunde Kamati ya watu watatu kuchunguza wizi katika akaunti ya EPA na miezi mitano baada ya serikali kufikisha mahakamani baadhi ya watuhumiwa.

Kamati ya Rais Kikwete iliongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Johnson Mwanyika na wajumbe wake wengine walikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Saidi Mwema.

Sababu za Feleshi zinaonyesha wazi kuwa ni  “mbeleko ya serikali” ya kuibebea Kagoda.

Hoja kwamba DPP hawezi kupeleka Kagoda mahakamani hadi hapo utakapopatikana ushahidi kutoka kwa makampuni ya nje, ni uthibitisho wa kile ambacho wananchi waliona tangu awali, kwamba serikali haina ubavu wa kupeleka Kagoda mahakamani.

Hii ni kwa sababu, katika kesi zote za EPA zilizofunguliwa, hakuna hata mshitakiwa mmoja anayehusishwa na makampuni ya nje ambaye Feleshi anasubiri uthibitisho wake.

Makampuni yote ya nje yanayodaiwa kusaini mikataba ya kuuziana madeni na makampuni ya ndani, hayamo katika kesi zilizofunguliwa na serikali mahakamani.
 
Kutokana na hali hiyo, kile kinachodaiwa kutafutwa na DPP kwa Kagoda, hakikupewa nafasi kwa makampuni au watu binafsi ambao wameburuzwa mahakamani.

Aidha, Feleshi anajua kuwa hata maodita, kampuni ya Delloite & Toche waliofanya ukaguzi wa hesabu za BoT walishatangaza kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kuomba wanaotajwa na Kagoda kuwa waliwapa kazi wajitokeze. Hakuna hata kampuni moja iliyoitikia wito huo.

Si kampuni ya Lindetivs J. Export BV ya Ujerumani wala nyingine yeyote iliyojitokeza. Maodita walithibitishia serikali, pasipo na chembe ya mashaka, kuwa makampuni yaliyotajwa na Kagoda hayapo. Kagoda ilitumia nyaraka za kugushi kujipatia fedha.

Sasa swali ni kwa nini hadi hapo serikali haiwezi kufungua kesi mahakamani dhidi Kagoda kwa kosa la udanganyifu na kujipatia fedha kwa njia ya uwongo?

Je, iwapo makampuni yaliyofanya biashara na Kagoda hayapo na Feleshi anajua kuwa hayawezi kupatikana, kwa nini serikali inaendelea kutumia rasilimali za nchi kwa kuchunguza kitu ambacho hakipo?

Kwa nini Feleshi na wenzake wanadanganya wananchi kwa kusema serikali ina ubavu wa kupeleka mahakamani wamiliki wa Kagoda, wakati ubavu huo haupo?

DPP anasema serikali inachukua tahadhali ili Kagoda isije ikashinda mahakamani na kulazimika kulipwa fidia ya mabilioni ya shilingi kwa kuchafuliwa jina.

Hapa Feleshi amekuwa mpelelezi, mwendesha mashitaka na hakimu. Anataka kusema kuwa ana uhakika serikali itashinda kesi zake zote ilizofungua mahakamani na hivyo haitalipa fidia.

Hili si kweli. Ukweli ni kwamba Feleshi anatumia kisingizio hicho ili kuibeba Kagoda. Ni ukweli usiokuwa na chembe ya mashaka, kwamba ushahidi uliopo kwa Kagoda ndiyo huo huo uliotumika kushitaki makampuni mengine.

Kesi dhidi ya Kagoda haihitaji kuendeshwa na watalaamu kutoka nje.  Hakuna asiyefahamu kwamba Kagoda ilitawanya fedha hizo kupitia matawi saba ya Benk ya CRDB jijini Dar es Salaam, na kwamba waliopewa fedha wanajulikana. Hata mahali walipo panafahamika.

Kwamba Kagoda haikuwa na mkataba na makampuni hayo, ni jambo ambalo liko wazi. Kwanza, kwa sababu tayari imethibitika kuwa makampuni hayo hayapo huko yanakotajwa.

Lakini pili, mkataba wa Kagoda una mapungufu mengi ya kisheria ikiwamo usahihishaji uliofanyika ndani ya saa 24, jambo ambalo Kagoda haiwezi kuthibitisha kwamba walisafiri kutoka Tanzania hadi Ujerumani na kurudi nchini kwa muda huo.

Halafu kuna hili la madai ya DPP kukataa kufanya kazi “kwa shinikizo la wanasiasa.”

Ukiangalia kwa makini suala zima la kilichoitwa, “Sakata la EPA,” kazi zote na hatua zote zilichukuliwa baada ya kuwapo shinikizo kutoka kwa wanasiasa, wanaharakati, wananchi na kwa kiwango kikubwa, vyombo vya habari.

Hata mara moja ofisi ya DPP haikuwahi kushinikiza serikali kufanya uchunguzi katika wizi huu. Ni kutokana na shinikizo la wananchi na asasi nyingine za kiraia, Rais Jakaya Kikwete aliunda Kamati ya kuchunguza wizi huu.

Kabla ya wanaharakati kumkalia kooni Kikwete, awali serikali na hata rais mwenyewe alisema, “Fedha za EPA, si za serikali.” Aliingiza hata utani wa “hawa bwana walichomeana utambi.” Tafsiri ya kauli hizo ilikuwa kupoza moto uliokuwa umeanza kuwawakia watuhumiwa.

Hata hivyo, uteuzi wa Feleshi kuwa DPP  unafanywa na rais ambaye, katika mazingira ya Tanzania, ni mwanasiasa mkuu anayeongoza chama kilichoko ikulu.

Kutokana na hali hiyo, suala hapa si ushahidi kutokuwapo, kama anavyosema Feleshi, bali serikali haina ubavu wa kupeleka wahusika wa Kagoda mahakamani.

Je, serikali haina andishi la wakili wa Mahakama Kuu, katika kampuni ya mawakili ya Malegesi – Malegesi Law Chambers – ya Dar es Salaam, Bhyidinka Michael Sanze?

Mbona Sanze anasema wazi katika andishi lake kwamba alishuhudia mikataba ya Kagoda ndani ya ofisi za kampuni ya Caspian Construction Limited ambayo inamilikiwa na mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz?

Sanze anasema aliitwa na Malegesi ofisini kwa Rostam Aziz, 50 Milambo. Alipofika aliwakuta Rostam, Peter Noni na Malegesi ambao walimwambia kuwa fedha alizokuwa anashuhudia mikataba yake, zilikuwa zinahitajika kwa ajili ya kugharamia uchaguzi wa mgombea wa CCM mwaka 2005.

Andishi la wakili linaeleza kuwa Rostam Aziz, Peter Noni na Bered Malegesi walimthibitishia Sanze kuwa Rostam alikuwa kwenye kikao ambako rais mstaafu Benjamin Mkapa alitoa maelekezo kwa Gavana Daudi Ballali wa BoT kutoa fedha hizo kwa Rostam kwa ajili ya uchaguzi.

Wakati huo Peter Noni alikuwa Mkurugenzi wa Mipango na Uchumi katika BoT. Hivi sasa ni Mkurugenzi wa Mipango ya Kimikakati. Ballali alifariki dunia mwaka jana nchini Marekani.

Sanze anasema Malegesi aliishakwenda kujiridhisha kwa Ballali na Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula kuwa yaliyosemwa na Rostam yalikuwa kweli.

Sasa serikali haina andishi la Sanze? Kama inalo imelifanyia kazi kwa kiasi gani? Je, imewahi kumhoji rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye Sanze anadai kuwa aliambiwa na Rostam kuwa alikuwapo katika kikao kilichopanga mkakati wa kukwapua katika EPA?

Je, DPP anaweza kusema sababu iliyofanya Mkapa asihojiwe? Ni kweli kwamba ushahidi wake haukuhitajika katika kutafuta ukweli juu ya Kagoda, hasa baada ya maodita kujiridhisha kuwa Kagoda ilighushi nyaraka?

Kwa nini Kamati ya Rais haikumuhoji aliyekuwa katibu mkuu wa  zamani wa CCM, Phliph Mangula? Ilimwogopa! Au serikali ilidharau maelezo ya Sanze?

Serikali haina andishi la Ballali lenye kufichua kila kitu juu ya ukwapuajia huo na jinsi baadhi ya vigogo walivyoshiriki katika mchezo huo? Kama haina, Feleshi alichukua jukumu gani kuhakikisha Ballali anahojiwa?

Wananchi wanajua mamlaka na madaraka aliyonayo DDP. Lakini inavyoonekana katika hili la Kagoda, DPP ameamua kulimaliza kwa usemi wa Kiswahili, “funika kombe mwanaharamu apite.” Kuna haja ya kufunua kombe ili mwanaharamu aadabishwe.

Kinacholeta faraja ni kwamba wananchi wanaelewa nini kilifanyika na nini kinaendelea kufanyika. Wanajua kupembua, nini mazingaombwe na nini halisi.

Kama Rais Kikwete hajaamua wana-Kagoda kukamatwa, basi na Feleshi anaendelea kuwa likizo. Lakini basi asiendelee kutoa kauli za hadaa hata mahali palipo wazi.

Kagoda haishitakiwi wala kushitakika kwa kuwa inalindwa na wanaoifahamu kampuni na wanaowafahamu walioiunda. Wanawalinda. Feleshi ni kofuli tu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: