Dunia yadadisi ulipuaji Sept. 11


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version

ULIPUAJI wa majengo ya Washington na New York miaka tisa iliyopita, umesababisha gharama kubwa ya umwagaji wa damu na mali.

Lakini pia majibu ya mapigo hayo nayo yamesababisha gharama kubwa zaidi ya umwagaji damu na mali, na inavyoonekana dunia haijaona mwisho wake.

Ingawa kikundi cha al-Qaeda kilichodaiwa kuhusika na ulipuaji huo wa kihistoria kinaonekana kupungukiwa nguvu, mbinu na ubunifu wa kufanikisha ulipuaji mwingine wa aina hiyo, lakini Marekani inazidi kudidimia katika dimbwi la matope liitwalo Afghanistan.

Al – Qaeda kimebaki kikundi kidogo kati ya makundi mengi ya kijihadi yalivyozagaa nchini Pakistan na katika maeneo mengine duniani.

Idadi ya Wamarekani waliokufa katika mapigano nchini Iraq na Afghanistan inakaribia mara mbili ya Wamarekani waliokufa katika ulipuaji wa 11 Septemba 2001.

Jumla ya gharama ya vita viwili hivi virefu vinafikia mabilioni ya dola za Kimarekani.

Wakati Marekani inaivamia Iraq mwaka 2003, bei ya mafuta yasiyosafishwa yalikuwa dola za Kimarekani 25 kwa pipa. Bei hii ilifikia dola 140 kwa pipa mwaka 2008 ingawa sasa hivi bei bado ni zaidi ya mara tatu ya ile ya mwaka 2003.

Hata wakati dunia inaadhimisha miaka 9 ya “ulipuaji wa Septemba 11,” bado kuna hali ya wasiwasi wa kushuhudia machafuko zaidi yanayotokana na tukio hilo.

Jumapili iliyopita, kasisi wa kanisa moja nchini Mmarekani, Terry Jones alifuta azma yake ya kuchoma nakala za Quran kupinga kile alichokiita “uchokozi wa Waisilamu.”

Waislamu walitaka kujenga kituo cha utamaduni cha Kiisilamu karibu na pale palipokuwa minara pacha iliyolipuliwa mwaka 2001. Jones ana kanisa alilolianzisha lenye waumini wapatao 50 tu.

Kama angetimiza azma yake, dunia ingeweza kushuhudia vurugu kubwa na hata umwagaji wa damu kutoka kwa waumini wa Kiisilamu na tishio dhidi ya majeshi ya Marekani yaliyoko Afghanistan, Pakistan, Iraq, na kwingineko.

Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanasema usitishwaji wa kuchoma moto nakala za Quran haumaananishi kwamba hakutatokea akina Terry Jones wengine.

Lakini haya yote yanatokea wakati bado kuna utata mkubwa wa tukio zima la September 11 huku wadadisi wa mambo wanazidi kuhoji ‘ukweli’ halisi wa tukio hilo.

Wanahoji kutokana na namna ya ubunifu wa hali ya juu uliofanywa kisayansi, haiwezekani kikundi cha watu kama cha akina Osama bin Laden kufanya ulipuaji wa namna hiyo.

Wanasema uandaaji wa mpango huo ulihitaji muda mrefu na kuhoji vipi vyombo vya upelelezi wa taifa kubwa la Marekani lilishindwa kabisa kugundua njama hizo hadi walipostukizwa tu?

Mwandishi wa habari mmoja maarufu Muingereza, Robert Fisk, ambaye kwa miaka 30 iliyopita ameishi Mashariki ya Kati na mchambuzi wa masuala ya eneo hilo katika uhusiano wake na nchi za Magharibi, naye ana shaka iwapo ‘ukweli’ halisi kuhusu tukio hilo umetolewa.

Siku moja katika mji wa Cork, Jamhuri ya Ireland, Fisk alialikwa kutoa mdahalo ambapo mmoja wa wahudhuriaji alimuuliza:

“Kama unajiamini kwamba wewe ni muandishi huru (Fisk anaandikia gazeti la “The Independent” la Uingereza), kwa nini basi huandiki ule ukweli kabisa unaofichwa wa tukio la Septemba 11?”

Alisema, “Kwa nini huuelezi ukweli – kwamba utawala wa Bush, ukishirikana na CIA na Mossad (Shirika la kijasusi la Israel) ndiyo walipanga kulipua minara pacha?”

Fisk anasema kuanzia hapo kila mara alijikuta anaulizwa swali kama hilo na kila mara anajaribu kueleza kuwa yeye siyo bingwa wa njama zinazosukwa katika ardhi ya Marekani.

Anasema anachojua yeye ni kwamba Bush amehusika katika njama nyingi tu – za kisiasa na kijeshi – na kufanya uhalifu mkubwa wa kivita huko Mashariki ya Kati na kusababisha vifo vya malaki ya watu wasio na hatia, lakini haamini iwapo huyo huyo Bush angeweza kufanya mauaji ya raia wake!

Hata hivyo, anasema ingawa amejitahidi kusema kile ambacho anafikiria ni ukweli kuhusu ulipuaji uliofanyika, lakini ambayo yeye mwenyewe anashindwa kuyaamini.

Kwa mfano anasema: Inakuwaje mabaki ya ndege iliyoligonga jengo la Makao Makuu ya wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington yasionekane? Kwa nini maafisa waliohusika na ndege ile ya tatu (Flight 93) iliyoanguka katika jimbo la Pennsylvania wamezibwa midomo?

Kwa nini mabaki ya ndege hiyo yalienea kwa umbali wa kilometa kadha wakati awali ilielezwa kwamba ndege hiyo ilianguka nzima nzima katika eneo moja?

Utata kuhusu ulipuaji wa Minara Pacha: Kama ni kweli kwamba katika hali ya kawaida mafuta ya taa huwaka katika nyuzi joto 820C, kwa nini nguzo na boriti za chuma cha pua (steel) za jengo la Minara Pacha (ambazo kuyeyuka kwake ni katika nyuzi joto 1,480C) zikatike kwa wakati mmoja?

Mafuta ya taa ni nishati inayotumika katika injini za ndege za abiria aina ya jet – zilizotumika kulipulia Minara Pacha.

Je, kwa nini mnara wa tatu (uliokuwa ukijulikana kama ‘World Centre Building 7 – kwa kifupi “WTC7”’) ambao ulianguka wote ndani ya sekunde 6.6 tu, na kuangukia ndani ya eneo lake, saa 11.30 jioni Septemba 11?

Kwa nini jengo hilo nalo lilianguka kwa “nidhamu nzuri” tu wakati ambapo halikuwa limegongwa na ndege yeyote?

Taasisi ya The American National Institute of Standards and Technology (ANIST) ya nchini Marekani ilipewa jukumu la kuchunguza chanzo cha kuanguka kwa majengo hayo matatu. Mpaka sasa, bado haijatoa ripoti kuhusu WTC7.

Tayari maprofesa wawili wa masuala ya uhandisi wamepeleka pingamizi mahakamani kupinga ripoti ya ANIST wakidai ina udanganyifu mkubwa.

Aidha, kiuandishi wa habari kuna vitu kadha katika tukio la Septemba 11 ambavyo haviendani. Kwa mfano, ripoti za awali za tukio ziliosema kulikuwapo na sauti ya mlipuko, ambazo ni kuvunjika kwa boriti – hazikuwa za kweli.

Hata taarifa kwmaba mwili wa mfanyakazi mmoja wa kike wa ndege uliokotwa barabarani, nazo zilijaa uwongo.

Hizo pengine ni ripoti za kuambiwa tu, kama vile ile orodha ya awali ya CIA ya wateka nyara ambayo ilijumuisha pia majina ya watu walio hai hadi leo na wanaishi huko Mashariki ya Kati.

Kwa upande wao, wanaharakati nchini Marekani wanaopinga serikali yao kupeleka majeshi kupigana nchi za nje wanasema Septemba 11 ni mradi uliobuniwa na rais George W. Bush kwa lengo la kuvamia Afghanistan na Iraq.

0
No votes yet