Edward Lowassa alikuwa sahihi?


Nkwazi Mhango's picture

Na Nkwazi Mhango - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Edward Lowassa

Nakuamkia na kukupa pole kwa shughuli za hapa na pale hasa kipindi hiki unapokabiliwa na pilika za kutaka kuendelea kuwa mbunge wa Monduli.

Niseme ukweli. Mahojiano ya hivi karibuni kati yako na Tido Mhando wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), yaliniacha hoi na kunitisha kwa aina ya siasa tunazoanza kujenga.

Sikuamini kuwa hili lingetokea ambapo mtu angeulizwa maswali elekezi, yenye nia ya kumjenga kwa gharama yoyote ile, bila kujali maslahi ya umma.

Hebu nikiri kwamba mimi ni shabiki wako ambaye yuko tayari hata kufungwa kwa kukutetea; lakini mahojiano yako, kusema ukweli, yaliniacha hoi ukiachia mbali kunishawishi kukuandikia waraka huu wa wazi.

Katika mahojiano hayo ulizungumzia mambo mengi, hasa yale ya binafsi, ukikwepa yale ya kitaifa ambayo kama ungeyazungumzia na kutoa majibu, huenda yangeondoa dukuduku langu au la wengi.

Watu hawataki kusikia jinsi unavyojihukumu, tena kwa upendeleo, bali wanataka ufumbuzi wa matatizo ya umeme, kujuana, ufisadi, usanii na mengine mengi yanayowakwaza.

Nianze hili la kusema kuwa yote yaliyokusibu yalisababishwa na baadhi ya watu, ambao hukuwataja, kuutaka uwaziri mkuu.

Je, unaweza kuwataja hawa wahusika wa njama hii? Kwangu mimi uwaziri mkuu hutolewa na rais. Je, una maana kuna watu wanamuendesha rais wetu nyuma ya pazia?

Je, kwa shambulio hili humlengi waziri mkuu wetu Mizengo Pinda ambaye aliteuliwa pindi tu ulipotimka?

Je, kwanini hukutaka kukiri kuwa ulikosea katika haraka na harakati zako za kuleta umeme wa dharura ambao uligeuka kitendawili na hasara kwa taifa, ukiachia mbali mateso ya kukaa kizani na kulanguliwa umeme?

Ulisema pia katika mahojiano kuwa wewe si mtu wa kukaa ofisini na kusoma mafaili. Je, huoni kwa kutokaa ofisini, unakuwa na sifa ya kufanya mambo kwa kuendeshwa na matukio badala ya kanuni? Rejea kuvurunda kwako katika kashfa iliyokugharimu.

Je, umeshataja mali zako kama sheria inavyotaka? Una utajiri kiasi gani? Nafurahi kwamba waziri mkuu wa sasa hakuogopa lolote; alitutajia umaskini wake na tukaridhika.

Najua rafiki yako kipenzi unayekiri hadharani kila upatapo fursa, Jakaya Kikwete, hajataja mali zake hadharani na sitegemei kuwa atafanya hivyo.

Je, huu si ushahidi kuwa si wewe wala rafiki yako mnapaswa kuwa viongozi wa umma – kwani mnapuuzia sheria, tena muhimu, ya kupima uadilifu wa kiongozi?

Bw. Lowassa, kwanini hukutumia fursa ya mahojiano na Tido kutoa maelezo kuhusiana na shutuma unazodaiwa kutwishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa umejilimbikizia mali nyingi ambazo huwezi na wala hujawahi kutolea maelezo ulivyozipata?

Je, hujui kuwa ukiachia mbali kashfa ya Richmond, hizi zimegeuka kongwa ya kudumu shingoni mwako?

Jitahidi utafute fursa nyingine kwa kuwatumia akina Tido na wengine unaowaamini kwa vile wana “shahada za uandishi,” wakuhoji utoe ufafanuzi wa hili, kwani yapata miaka 15 sasa tangu Mwalimu afyatue kombora hili.

Hili la kutaka waandishi wawe na digrii naona ni udikteta na ubabaishaji. Nimelieleza vizuri kwenye kitabu changu cha “Saa ya Ukombozi.” Ningeshauri utafute nakala ya kitabu hicho na kukisoma ili uone madhara ya unachotetea.

Nilishangaa kusikia ukisema maneno yafuatayo: “Rekodi yangu ni safi, nikiwa waziri kwenye serikali ya Mzee Mwinyi nilizuia kuuzwa maeneo mengi ya wazi nchini, mfano ni ule mpango wa kuuzwa kwa uwanja wa Mnazi Mmoja.

“Nilifanya hivyo pia wakati nikiwa waziri (Serikali ya Awamu ya Tatu) tulipovunja mkataba na Kampuni ya Kiingereza ya City Water...ninayo rekodi ya utumishi bora.”

Ya kweli hayo? Je, na Richmond ni sehemu mojawapo ya rekodi safi? Je, urafiki wako na Kikwete nao ni sehemu ya rekodi safi? Kuna haja ya kuzungatia ukweli na kuacha kuwachukulia wasikilizaji na watazamaji kama watu wasio na ubongo wala kumbukumbu.

Hivi kwanini unasema kuwa kamati teule ya Bunge ilikuonea kiasi cha kutokukuhoji wakati hukuwa tayari kujipeleka mbele yake kujieleza?

Je, sasa unaposema kamati ilikosea wakati nawe ni mbunge aliyeridhia iundwe, tena ukiwa mkuu wa shughuli za serikali bungeni, huoni kama unalitukana bunge na kuonyesha ugeugeu na ubinafsi wa hali ya juu?

Hapa unaweza kusema eti kweli huna kinyongo wakati unaamini ulionewa ili kupokonywa uwaziri mkuu?

Je, kwanini hukueleza mantiki ya kuingilia shughuli ambayo hukuwa na mamlaka nayo kisheria huku ukipendelea kampuni feki, iwapo hakukuwa na makosa wala maslahi binafsi au harufu ya rushwa?

Je, unakanusha kuwa hukuibeba Richmond? Je, ulikuwa na faida kiasi gani, pamoja na wengine wazito, hadi kukubali kubeba msalaba wote wa serikali ili wahusika wasijulikane?

Kuna shutuma ambazo hujajibu, kwamba ulitumia nafasi yako kumtafutia bintiyo kazi Benki Kuu (BoT). Je, si vyema ukakanusha hili au lau kulitolea maelezo mafupi?

Naomba nikupe ushauri. Kwanza soma maneno haya:“Niseme nini...Namshukuru sana askofu yule aliyenifundisha hili...sikuwa na dhamira ya kugombana na vyombo vya habari...liko jambo muhimu hapa la kutambua ni lini useme, kwa nini useme na useme kwa nani.”

Kwa vile unaye askofu mshauri, nami sasa nakushauri: Rudi kwake umuombe ushauri mwingine juu ya kusema ukweli na kuukubali; kwamba ulishachafuka kiasi cha kutosha kutoweza kusafishwa kwa urahisi.

Japo ni haki ya mtu kufurukuta, kuna kipindi naona ni kama jinai kutumia vyombo vya umma kwa maslahi binafisi.

Pia ninakushauri umuombe huyo askofu akushauri kuwa mwendelee kuwa marafiki na Kikwete; lakini hii iwe kibinafsi na si katika shughuli za umma.

Nasema iwe kibinafsi kwani ofisi aliyonayo Kikwete si yake; bali ya wananchi ambao unataka kuwaaminisha kuwa hawajui kukumbuka wala kupembua mambo.

Nimalizie na salamu kwa wale wote uliowapa tenda ya kukusafisha na kukurejesha kwenye mioyo yetu. Sijui kama wanalipwa na wanalipwa kiasi gani. Nijuacho ni kwamba hawatafanikiwa.

Nakuomba upatapo ujumbe huu unijibu haraka ili roho itulie; nami niendelee na ushabiki wangu kwako.

Kila la heri katika kupambana na ukweli. Ila ukweli huweka huru na hakuna aliyepambana nao akaushinda.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: