Edward Lowassa 'anajua atendalo'


Ansbert Ngurumo's picture

Na Ansbert Ngurumo - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version
Tafakuri
Edward Lowassa

NI nani anaweza kumpinga Edward Lowassa? Ni nani ana uwezo wa kumtenga Lowassa na rafiki yake wa siku nyingi, Rais Jakaya Kikwete?

Lowasa mwenyewe, ambaye alikuwa waziri mkuu mara tu baada ya Kikwete kuingia madarakani, baadaye akajiuzulu kutokana na kashfa za mradi wa kufua umeme wa dharula wa Richmond, ameshajibu maswali hayo.

Amekaririwa na vyombo vya habari akisisitiza kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kumtenga yeye na Kikwete kwa sababu wametoka mbali. Ana sababu.

Na katika hili, naomba nimuunge mkono Lowassa nikubaliane naye na nimtetee. Kama yupo anayedhani ni rahisi kuwatenganisha wawili hawa, ajitokeze sasa ampinge Lowassa hadharani.

Lowassa si mjinga. Anajua asemalo. Hatumwi na mtu bali moyo wake. Isipokuwa anajua kwamba zipo jitihada za makusudi ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinazofanywa na baadhi ya wapambe na wachumia tumbo wanaotegemea fadhila za Kikwete.

Hao wanaamini na wanajua kuwa Lowassa keshachafuka kisiasa, na wanaamini kwamba hajakoma wala kukata tamaa.

Wanaona na wanajua kuwa uchafu wa Lowassa unamgusa pia Kikwete, lakini wangependa kuendelea kumlinda rais ili asichafuke kwa uchafu wa Lowassa.

Hivyo wanaamini kwamba njia ya kumlinda Kikwete ni kusema mara kwa mara kwamba wawili hawa siku hizi hawako pamoja, ili wananchi wenye hasira zao dhidi ya Lowassa wasione uhusiano wa hasira zao na Kikwete.

Hizi ni jitihada tu za CCM kumsafisha Kikwete na kumsafishia njia ya kisiasa, lakini wanajua kabisa kwamba si rahisi kuwatenga Lowassa na Kikwete; si kisiasa tu bali hata kifamilia.

Ingawa baadhi ya wachambuzi walidokeza kwamba kauli ya Rais Kikwete kwamba urais wake hauna ubia ililenga kusisitiza kutengana kwake na Lowassa na swahiba wao mwingine, Rostam Aziz, ukweli unabaki kuwa Rais Kikwete alisema tu lakini vitendo vyake vilikuwa na bado ni tofauti na kauli yake.

Kumbe naye yuko nyuma ya kampeni ileile ya kuwakana watu wake anapobanwa, lakini haachani nao maana bado anawategemea katika mambo kadhaa ya kimkakati.

Ndiyo maana wanaojua kinachoendelea bado wanahoji ulinzi ambao serikali imewapatia wahusika wa kashfa ya Richmond kiasi cha kushindwa hata kutekeleza maazimio na maagizo ya Bunge.

Na Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwahi kudokeza kwamba masuala haya yako ofisini kwa bosi wake. Kama si Lowassa na watu wake wanaolindwa, serikali inamlinda nani kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya Bunge?

Ikumbukwe kuwa Ofisi ya Rais, ambayo ndiyo inasimamia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ndiyo awali ilimsafisha Lowassa na wahusika wengine kabla ya Bunge kuingilia kati. Ikulu ilikuwa inamlinda nani kama si Lowassa na watu wake?

Na licha ya kauli za rais kuwa urais wake hauna ubia, wananchi wanajua kuwa rafiki zake ndio watuhumiwa wakubwa katika kashfa za wizi wa fedha kutoka akaunti ya madeni ya nje katika Benki Kuu (EPA), hasa kupitia kampuni ya Kagoda. Na juzi tu Rais Kikwete alikiri kwamba "mafisadi hawakamatiki kwa sababu ni wajanja."

Kuna ulinzi gani mwingine ambao mafisadi hao wataupata kutoka serikalini kama rais mwenyewe ameshakiri hadharani kwamba watu wenyewe ni "wajanja" kuliko serikali yake? Ni kwa jinsi gani urais wake utashindwa kuwa na ubia nao?

Jeuri ya Lowassa kujitokeza sasa na kusema kwamba hakuna atakayeweza kumtenga na Kikwete inatokana na kweli kwamba anajua kinachoendelea dhidi yake ndani ya chama na serikali; lakini anajua moyo wa rafiki yake uko pamoja naye.

Kwani tumesahau kwamba Lowassa alipopata msukosuko hadi akajiuzulu uwaziri mkuu, wananchi wote walimzomea na kumsonya, na alitetewa na mtu mmoja tu katika serikali nzima?

Nani alikuwa mtetezi wake, tena hadharani? Ni Rais Kikwete, pale aliposema kwamba yaliyompata rafiki yake wa siku nyingi na mwenzi wake kisiasa na kifamilia, ni bahati mbaya tu – "ajali ya kisiasa."

Sasa mtu mwenye kinga kubwa ya rais wa nchi, kwa viwango hivi, atashindwaje kusimama na kujitetea mwenyewe kwa msisitizo, kwamba wanaofurukuta kumtenga na Kikwete wanapoteza muda?

Ukweli mmoja uko wazi. Lowassa hakuridhika na jinsi Kikwete alivyoshughulikia suala hili kabla hajakubali barua yake ya kujiuzulu. Alichukizwa pia na ulinzi wa rais kwa mafisadi wengine walioasisi mradi wenyewe uliomwondoa madarakani.

Anajua uhusika wa Kikwete katika mchakato mzima wa Richmond. Anakerwa na kelele za umma zinazomwonyesha yeye kama fisadi mkuu pekee katika suala hilo.

Lakini anafarijika kwamba pamoja na serikali kudiriki kuwapeleka mahakamani baadhi ya watendaji wa zamani wa serikali na kuwashitaki kwa matumizi mabaya ya madaraka, imeacha kuona kwamba Lowassa naye alitumia vibaya madaraka yaliyolisababishia taifa hasara kubwa kupitia mradi wa Richmond.

Haiwezi kumgusa kwa sababu siku ikifanya hivyo, ndipo ukweli wote wa Richmond utakapomwagika, na tutajua waasisi halisi wa mradi huo na waliomtuma yeye kuusimamia bila woga.

Lowassa anajua kuwa pamoja na vita vya ndani kwa ndani vinayomsumbua yeye na wenzake, bado ana ulinzi wa makao makuu. Chukua mfano huu mdogo.

Wakati Rais Kikwete anaweza kuitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kuwasakama, kuwatisha na kuwasulubu wabunge wanaokikosoa chama na kupinga ufisadi, akiwamo Spika wa Bunge, Samwel Sitta, ameshindwa kuwashughulikia akina Lowassa kwa kuiletea serikali yake fedheha ya kudumu.

NEC ilipokaa Butiama, Aprili mwaka jana, ilikataa katakata kuwajadili na kuwachukulia hatua kali watuhumiwa wakuu wa ufisadi, akiwamo Lowassa. Na muda mfupi baadaye tulisikia taarifa kuwa chama kimemsafisha Lowassa kuwa hahusiki na uchafu wa Richmond.

Si kwamba hahusiki, bali hahusiki peke yake. Ukimgusa yeye utawagusa na wengine wasiotaka kuguswa na ambao kwa bahati mbaya, ndiyo wanaopanga na kuongoza vikao vikubwa vya chama.

Lakini NEC hiyo hiyo ndiyo inapata ujasiri wa kumwita na kumshughulikia Sitta kwa sababu eti anawapa mwanya wabunge machachari wa CCM na upinzani kuikosoa serikali bungeni. Ni wazi kuwa kundi ndani ya NEC, linalomsakama Sitta, ni lilelile lililokuwa likimtetea Lowassa.

Na yote haya yanafanyika katika vikao vinavyoandaliwa na kusimamiwa na mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete ambaye alishatangaza urafiki wa kisiasa na kifamilia kati yake na Lowassa; na ambaye anasema urais wake hauna ubia na mtu yeyote.

Katika mazingira haya, Lowassa ana kosa gani naye kujitokeza akijigamba kwamba hakuna awezaye kumtenga na Kikwete? Nani anaweza kumwondolea ulinzi wa Kikwete? Kama yupo ajitokeze. Ajenge hoja.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: