Edward Lowassa: Rudi uwani


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 29 September 2009

Printer-friendly version
Gumzo
MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa

MBUNGE wa Monduli, mkoani Arusha, Edward Lowassa ameibuka. Amesema hakukutana na Rais Jakaya Kikwete barabarani; wala uhusiano alioita "imara walioujenga na Kikwete" hauwezi kuvurugwa na kikundi kidogo cha watu wenye nia mbaya.

Lowassa alitoa kauli hiyo wiki mbili zilizopita katika mahojiano yake na baadhi ya vyombo vya habari nchini.

Alisema, ‘‘Tumeshikamana wakati wote, na hata sasa bado ninaendelea kumuunga mkono… Mimi ndiye niliyekuwa mwenyekiti wa vikao vya kamati ya kampeni."

Kauli ya Lowassa ilitoka wiki moja baada ya Rais Kikwete kuliambia taifa kwa njia ya radio na televisheni, kwamba katika vita dhidi ya ufisadi "sina rafiki wala ndugu."

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Lowassa kuita waandhishi wa habari na kuzungumza nao kwa shabaha ya kujibu tuhuma au shutuma tangu alipoondoka serikalini.

Alijiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu, tarehe 7 Februari 2008 baada ya kubanwa na Bunge kutokana na shutuma za upendeleo wa kuipa kazi ya kufua umeme wa dharula kampuni ya Richmond Development Company (LLC).

Tokea wakati huo, Lowassa alikuwa hajajibu tuhuma hizo. Hajawahi kusema kwamba kampuni hiyo isiyokuwa na hadhi, sifa wala uwezo wa kufanya kazi iliyoomba, ilipata kazi hiyo kutokana na shinikizo lake.

Wala Lowassa hajasema kuwa hakuwahi kulazimisha watendaji serikalini kuipa kazi Richmond au kukaidi agizo la Baraza la Mawaziri lililotaka kampuni hiyo ifanyiwe uhakiki kabla ya kukabidhiwa kazi iliyoomba.

Badala yake, Lowassa ameishia kusema, "Nimeonewa sana, nimedhalilishwa sana na nimefedheshwa sana. Tatizo ni uwaziri mkuu." Hata katika mkutano wake huu wa juzi, hakukana kutohusika na sakata la Richmond.

Kimya cha Lowassa kuhusu tuhuma hizi kinaweza kuwa na maana kadhaa. Ama kuna mahali aliteleza au ana hofu kwamba wapinzani wake wanajua mengi na hivyo wanaweza kumuumbua.

Lowassa anafahamika. Ana uwezo mkubwa wa kujieleza na "kukana tuhuma." Ni mwanasiasa mwenye kujipenda na kupenda kutumia vyombo vya habari na waandishi wa habari mmoja mmoja.

Hata siku moja, Lowassa hawezi kutoka hadharani na kukiri kosa hata kama kosa alikanalo linaonwa hata na kipofu. Mifano ya matukio ya kale na ya sasa juu ya tabia hii ya Lowassa ni mingi.

Hata katika mkataba wa kusambaza maji katika jiji la Dar es Salaam na Pwani, kati ya serikali na mwekezaji – kampuni ya City Water ya Uingereza, Lowassa hakukawia kukana tuhuma zilizoporomoshwa na viongozi wa vyama vya upinzani kwamba aliingiza serikali katika mkenge.

Kwamba kampuni ya City Water haikuwa na uwezo wa kifedha wa kufanya kazi ya kuweka miundombinu ya maji katika eneo hilo.

Wapinzani walidai kuwa kampuni hiyo ilikuwa ya kitapeli; haikulenga kuboresha miundombinu ya maji, bali ilitaka kuchuma faida bila jasho.

Hili lilikuja kudhihirika ndani ya kipindi kifupi tu baada ya mkataba kufungwa; pale City Water iliposhindwa kuweka kiasi cha dola za Marekani 23 milioni kama ilivyokubaliwa katika mkataba wake na serikali.

Kampuni hiyo iliishia kuweka mtaji wa dola 8 milioni tu na kukodolea macho fedha zilizotolewa kwa serikali kama mkopo na Benki ya Dunia – dola 260 milioni, kwamba zitumike kama mtaji katika kazi hiyo.

Hadi sasa hakuna mwenye kujua kampuni ya Super Doll iliingiaje katika ubia na kuvuna asilimia 41 ya hisa wakati haikuchangia hata shilingi katika ubia wake ndani ya City Water.

Bila ujasiri wa rais Benjamin Mkapa wakati huo, kung'amua mapema kwamba City Water ni kampuni ya kitapeli na hivyo kutoa amri ya kuwaondoa kwa nguvu nchini, hakika njia ya kampuni hiyo kukwapua mabilioni hayo ya shilingi ilikuwa nyeupe.

Wakati taarifa kutoka serikalini na baraza la mawaziri zinasema ni Mkapa aliyeshupalia mkataba kuvunjwa baada ya kushinikizwa na Benki ya Dunia, nje ya serikali Lowassa hutajwa kwamba ni yeye aliyevunja mkataba.

Katika hali ya kawaida ya kutotaka kutukuzwa, Lowassa ilitarajiwa angesema ukweli. Angemsifia Mkapa kwa ujasiri, angalau basi katika hili. Angesema "sistahili sifa, maana si zangu."

Ni Lowassa aliyeshinikiza wabunge wa chama chake kutumia wingi wao bungeni kumfungia kushiriki shughuli za Bunge, mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe kwa madai kwamba alisema uwongo bungeni.

Zitto aliliambia Bunge kwamba aliyekuwa waziri wa nishati na madini, Nazir Karamagi alisaini mkataba wa uchimbaji madini katika mgodi wa Buzwagi, mkoani Shinyanga nje ya nchi na kinyume cha taratibu. Karamagi alikana madai hayo.

Hata hivyo, haikuchukua muda siri ya Karamagi ikafumuka. Taarifa zikavuja kwamba wakati Karamagi akisaini mkataba huo nchini Uingereza, Lowassa alikuwa nchini humo na alijua kinachotendwa na Karamagi.

Ni mazungumzo yawazi hata miongoni mwa wanachama wa CCM kwamba ni hatua hii ya Lowassa ya kushawishi, kwa kiwango cha kushinikiza, wabunge kumfungia Zitto, iliyochoche baadhi ya wananchi kuanza kuikataa CCM.

Ni hapa zogo lilipoanzia. Hata mawaziri wa Kikwete waliokwenda mikoani "kunadi bajeti ya serikali" walianza kuzomewa baada ya Bunge kumfungia Zitto.

Hata "operesheni Sangara" ambayo ndiyo imeibua upinzani mkubwa kwa CCM ilitokana na tukio hili.

Lakini hadi sasa, si Lowassa wala wapambe wake waliokiri kuwa ni uamuzi wao huo wa kumfungia Zitto ndiyo chanzo au kichocheo cha CCM kufika hapa kilipo sasa.

Kwa hoja hizi na nyingine, wachunguzi wa mambo wanasema bora Lowassa abaki uwani angalau kwa miaka kumi kutoka sasa ili ajikarabati kisiasa na kutafuta kukubalika upya.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: