Edward Lowassa: Usifanye kosa la pili


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version

MACHO na masikio ya Watanzania yako Dodoma kudodosa nini kitatokea huko, kunakofanyika vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa kuwa hiki ndicho chama tawala na Watanzania kama watawaliwa, wana haki ya kujua nini kinaamuliwa na chama tawala.

Tanga la merikebu ya CCM limekuwa linazidi kuchanika siku za karibuni na kilichokuwa kinasubiriwa ni uamuzi wa ama kugawana mbao au kuweka viraka kwenye tanga ili safari iendelee. Yote mawili yana ugumu wake.

Kwa walio wengi wanaona kufa na kupona kutategemea si busara za mwenyekiti Jakaya Kikwete, ispokuwa busara na utashi wa Edward Lowassa. Kwa nini?

Kwanza, uchovu mkubwa wa kufikiri uliokikumba chama hicho miaka ya karibuni unasababisha siasa za ndani ya chama ziwe za kuzungumzia watu na si masuala tena. Hata wale wanaojaribu kuzungumzia masuala hawajajipambanua kiasi cha kuaminika mbele ya wananachi waliokata tamaa.

Na kwa kuwa ni watu wanazungumziwa, basi Lowassa ndiye kiini na chimbuko la mazungumzo ndani ya chama hicho kwa sasa. Katika nafsi ya Lowassa, CCM inaanguka au kupona.

Pili, ombwe la uongozi wa taifa lunaanzia ndani ya CCM. Mbegu ya ombwe iliyopandwa ndani yake na sasa imezaa matunda hata serikalini. Mwenyekiti wake ambaye ni rais na mkuu wa nchi, amejipambanua kuwa ni dhaifu si kuongoza tu, bali hata wa kuanzisha fikra mpya za kukiondoa chama na taifa katika mkwamo unaozidi kujisimika katika kila sekta.

Kwa kuwa rais ni kila kitu katika taifa na mchakato wa katiba mpya unataka kuendeleza utamaduni huu, basi katika haiba ya Kikwete imejisimika taswira ya udhaifu na ulegelege wa kiuongozi ambao unaitwa ombwe; hali hiyo haiwezi kutatua mgogoro wa makundi uliomo ndani ya CCM kwa sasa.

Kwa hali hiyo, ni vigumu kujua ni nani hasa yuko njia panda ya maamuzi kwa sasa. Je, ni Kikwete? Lowassa, CCM au taifa? Kwa maoni yangu, anayeweza kupunguza makali ya kizungumkuti hiki, ni Lowassa. Ili kulijua hili turudi nyuma kidogo.

Lowassa aliyejiuzuru uwaziri mkuu ili kuokoa kile alichoita, “heshima ya serikali na chama chake,” habari zisizo rasmi lakini zinazoshawishi imani ya walio wengi ni kuwa, alifanya hivyo kulinda heshima ya mtu mmoja mzito sana.

Hili halijakanushwa wala kuthibitishwa japo Dk. Harrison Mwakyembe alinukuliwa akisema kama wangesema yote waliyoyaona nchi ingekuwa hatarini.

Yapo madai kwamba kujiuzuru kwa Lowassa yalikuwa ni makubaliano kati yake na bosi wake. Kwamba aandike barua ya kujiuzuru, lakini bosi wake akatae kujiuzuru huko ili kuvuta muda wa kushughulikia makali ya ripoti ya Bunge kuhusu mkataba tata wa Richmond.

Alipokabidhi barua ya kujiuzuru, kibao kikabadilika ghafla na kuruhusiwa ajiuzuru kwa ahadi kuwa angesafishwa baadaye. Haijatokea hadi leo. Je, kuna sababu ya Lowassa kuamini tena kuwa atasafishwa na waliomsaliti akatoswa peke yake?

Lowassa akikubali kujiondoa mwenyewe katika CCM atakuwa amefanya makosa makubwa. Sababu ziko nyingi; lakini nitaje chache.

Kwanza, kimantiki amejaribu kutatua hatima yake kisiasa kwa njia ya kujiuzuru na haijamsaidia yeye binafsi wala chama chake. Kwa kuwa kujizuru hakukusaidia, ni bora afukuzwe na aambiwe sababu za kufukuzwa kwake. Kama amekosa heshima kwa kijiuzuru uwaziri mkuu, atapataje heshima kwa kujivua nafasi ndogo?

Pili, vikao vya CCM vilivyopita vilitoa nafasi ya watuhumiwa wa ufisadi kupima uzito wa tuhuma na kujiondoa wenyewe. Muda uliwekwa na umepita kitambo. Kama Lowassa hakupima au alipima uzito wa tuhuma zake, hilo sasa sio suala muhimu. Ukweli wa wazi ni kuwa hajajiuzuru na kwa hiyo wanaomtuhumu kama wana mamlaka juu yake wamfukuze siyo kumtaka ajiondoe.

Tatu, kutojiuzuru kwa Lowassa kutaikisaidia chama chake kujenga upya utamaduni wa kuwajibishana maana kuwajibika kumeshindikana. Tumeona na tumeshuhudia hata baada ya ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyomchunguza Jairo kutamka kuwa katibu mkuu huyo na wenzake wengine wana hatia, bado wahusika wametamka kuwa hawatajiuzuru kwa sababu hawaoni kosa lao.

Lowassa alifanya hivyo labda kwa haraka na sasa anajilaumu. Siyo utamaduni wa chama chake kuwajibishana.

Nne, watu makini huwa wanaweza kujiuzuru nafasi zao ili kuwakinga walio juu yao au chama/taasisi zao. Hatua hii huchukuliwa kwa makini sana ikizingatiwa kuwa wanaheshimiana na kuaminiana sana na walio juu yao au taasisi yao.

Hivi sasa heshima na imani hiyo haipo kati ya Lowassa na wakubwa wake au na chama chake. Kitendo cha kujiuzuru kitatafsiriwa kuwa ni udhaifu wa kiuongozi kwa upande wa Lowassa.

Katika siku za karibuni, Lowassa amesikika akiikosoa serikali yake kuwa inaogopa kufanya maamuzi magumu. Hii inanifanya niamini kuwa Lowassa si mtu anayeogopa kufanya maamuzi magumu. Huu ni wakati wake kuonyesha kuwa si dhaifu kama serikali yake.

Haya ninayosema hayana uhusiano wa kama Lowassa ni fisadi au si fisadi. Kwangu mimi hili si muhimu sana kwa sasa, kwa sababu ikiwa Lowassa ni fisadi basi hata CCM ni fisadi na kama Lowassa si fisadi basi hata CCM si mafisadi.

Umoja kati ya ufisadi na CCM ni sawa na umoja kati ya CCM ya sasa na Lowassa. Kujaribu kutenganisha vitu hivi ni kupuuza ukweli wa mambo katika taifa hili tangu mwaka 2005 hadi leo hii.

Dhana ya kuwa ufisadi ni wa mtu binafsi si wa chama ni ya kufikirika kwa sababu tumeshuhudia wenyewe kuwa katika taifa hili, ni rahisi sana kumfunga mwizi wa kuku lakini si rahisi kumgusa aliyefisadi raslimali za nchi.

Wale wote waliotajwa na tume huru mbalimbali kwa kufanya ubadhirifu mkubwa, wametakaswa na kuachwa wafaidi wizi wao. Hata hawa waliotajwa jana katika sakata la Jairo, hawatafanywa lolote lakini wezi wa chenji kwenye daladala ama wanachomwa kwa matairi au wanaozea rumande kwa kukosa dhamana. Lowassa ana haki ya kukataa kufanywa kafara ikiwa wahujumu wenzake wanatesa mitaani wakiwamo wakubwa zaidi yake.

Aidha, ufisadi unaodaiwa kufanywa na Lowassa usingefanyika bila idhini ya wenzake na kuwanufaisha wenzake pia.

Mpaka leo hii, licha ya ama kamati teule kupuuza kumhoji au yeye kukaidi kuhojiwa, Lowassa hajalieleza taifa hili nini hasa kilitokea katika sakata la Richmond. Kimya chake kinaonyesha alishiriki.

Hata hivyo, kukimbilia kumvua gamba ni kuwanyima wananchi kujua ukweli wa sakata hili ambalo limeasisi enzi za giza na migawo ya umeme isiyo na mwisho.  Ikiwa kujiuzuru kwa Lowassa hakujaleta unafuu wa nishati ya umeme, iwe Lowassa au wananchi hawana sababu ya kutumaini kuwa kujiuzuru kwake katika nafasi ya NEC kutaleta nafuu yoyote.

Kinachotakiwa ni CCM ije mbele ya wananchi na kukiri kuwa ni chama cha ufisadi na daima kiape kutouonea haya wala aibu. Wale wasiopenda msimamo wa wazi kuhusu suala hili, waondoke kwa amani ndani ya chama hicho na kujiunga na vyama vingine ambapo ufisadi hautakiwi.

Msimamo huu pia unamhusu mwenyekiti Kikwete ikiwa ni yeye aliye nyuma ya kushinikiza kujivua gamba. Anayo ruhusa ya kuondoka ndani ya CCM na kwenda penginepo anapodhani hakuna ufisadi.

Tupende au tusipende, ndani ya CCM kuna ufisadi. Kuwatoa kafara wachache hakutasaidia.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: