Ee Mungu nani katulaani na mikataba hii?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 06 October 2009

Printer-friendly version
Tafakuri

KATIKA jamii ya Kiafrika kuna makabila ambayo yamekuwa imara kulinda tamaduni zao, miongoni mwayo ni Wamasai. Hakuna anayeweza kukataa ukweli kwamba Wamasai wanalinda mila zao kwa nguvu zote.

Kwa Tanzania Wamasai wanatajwa kuwa kabila pekee ambalo limejipambanua kuenzi utamaduni wake. Uvaaji tu wa Wamasai unathibitisha pasi na shaka yoyote kwamba wamesimamia yale wanayoamini ni ya kwao.

Pamoja na uhodari wa Wamasai, utunzaji na uzingatiaji wa mila zao, simulizi za kuvutia juu ya ushujaa wao hasa katika kuishi na kupambana wanyamapori, ni kabila linalowaweka pembeni wanawake.

Kwa kawaida wanawake katika taratibu za kiutawala kwa Wamasai hawana nafasi, hili likijadiliwa kwa mapana yake kuna uwezekano wa kuliona kama jambo lililokubalika katika taratibu zao.

Lakini, kuna suala ambalo kwa miaka na miaka nimekuwa ninajiuliza, hivi, inakuwaje wanaume wa Kimasai wanachinja ng’ombe au mbuzi, wanakula nyama yote na kuwaachia wanawake matumbo tu?

Nimekuwa najiuliza swali hili mara nyingi, lakini jibu la maana sijapata hadi leo. Kwa hiyo imebaki tu kwamba nyama ya maana ni halali ya wanaume ilhali wanawake wakibakia na matumbo.

Hii ni mila ya Kimasai na kwa kweli itachukua muda mrefu kuvunja mila hii. Ni utamaduni ulioasisiwa na kuota mizizi kwa vizazi vingi sasa.

Hivi majuzi wakati natafakari mila hii ya Kimasai, nikajikuta nashangaa baada ya kuoanisha utamaduni huu wa Kimasai na ambao sisi kama taifa tumejikuta tumeujenga.

Huu si mwingine bali ni ule wa mikataba ambayo taifa kupitia taasisi zake mbalimbali inaingia na wale wanaoitwa wawekezaji.

Kwa ujumla wake, mikataba yote ambayo nchi hii imeingia na wawekezaji, mwisho wa yote tumejikuta tukiambulia matumbo kama wale akina mama wa Kimasai ilhali wanaume wakifaidi minofu.

Hakuna hata mkataba mmoja wa uwekezaji, iwe ni kuuza shirika la umma, au kuleta kampuni ya kimenejimenti au kuingia ubia tumenufaika kama taifa.

Kila tulichofanyiwa ni kuambulia matumbo tu. Hali hii nimeitafakari kwa kitambo na kufikia hitimisho kwamba sisi ni watu wa kubaki na matumbo wakati minofu minono ikiondoka na wajanja- wawekezaji.

Kwa kifupi hatushituki wala kuamka, kila mkataba mpya unapokuja.

Tuanze na ubinafsishaji wa Kampuni ya Bia (TBL) miaka ya mwanzo ya tisini, si tu kwamba tuliuza TBL kwa bei ya kutupa, bali pia tuliikabidhi majengo, mashamba na kila aina ya mali ambayo haikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kiwanda kwa wawekezaji.

Kwa hiyo, Indol ilichofanya ilikuwa kazi rahisi tu kujenga mtaji mpya wa TBL, waliuza mlolongo wa majumba yake yaliyokuwa yemetapakaa nchi nzima na baadaye kuwekeza kwenye kiwanda hicho.

Hata hivyo, uwekezaji wa TBL unaweza kutajwa kama wenye nafuu zaidi katika ulaji wa utumbo ninaouzungumzia.

Lakini kuna suala la kuuza NBC 1997. Hapa si kwamba Watanzania tulilishwa utumbo tu, bali tulilishwa uliooza kabisa!

Hii ni benki iliyokisiwa kuwa na thamani ya karibu Sh. 30 bilioni, lakini baada ya safari ya kwenda kuonana na watu wa ABSA wa Afrika Kusini ikiwahusu aliyekuwa gavana wa Banki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati huo, Dk. Idris Rashid na Waziri wa Fedha wakati huo, Daniel Yona, umma ukapigwa butwaa kwamba thamani ya NBC ilishuka kutoka takribani Sh. 30 bilioni hadi 15 bilioni.

ABSA ikapewa benki, majengo yake yote yaliyozagaa nchi nzima na yenyewe kwa kiburi ikafunga baadhi ya matawi kwenye wilaya za nchi hii na kubaki na matawi ya kwenye mikoa tu.

Jeuri hiyo ya kutulisha utumbo haikuishia hapo, ABSA hawakuleta fedha hapa, wakasema NBC 1997 ilikuwa inaidai Benki ya makabwela NMB Sh. 15 bilioni katika mahesabu yao.

NMB ikakamuliwa hadi ikalipa fedha hizo kwa NBC na kisha fedha hiyo ndiyo ililipwa serikali kama mauzo halali ya NBC kwa ABSA. Utumbo uliooza kwa kiwango gani huu?

Ukaja mkataba wa IPTL ambao serikali ilitumbukiza TANESCO katika kilio cha kusaga meno cha ajabu. Yaani kwa mara ya kwanza TANESCO ikajikuta ikilipa fedha kwa kampuni inayozalisha umeme na kuiuzia.

Si mbaya sana, kununua umeme, lakini mbaya ni pale unaponunua umeme unaozalishwa, lakini pia unawajibika kuilipa kampuni hata wakati haizalishi umeme wa kukuuzia kwa kigezo kipya cha capacity charges. Tumefanya haya kwa miaka mingi hadi TANESCO imeishiwa pumzi na sasa inapumulia mirija!

Upo mkataba kabambe wa kuuza iliyokuwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL). Wakaja wawekezaji walioitwa MSI/Detcon ambao walijotosa kununua asilimia 35 ya hisa za TTCL kwa thamani ya dola za Marekani 120 milioni wakati huo sawa na Sh. 120 bilioni.

Wakapiga mdomo wakapewa TTCL baada ya kulipa nusu ya kiasi hicho, yaani dola 60 milioni (sawa na Sh. 60 bilioni) kwa madai kwamba watalipa nusu nyingine baada ya kufanya ukaguzi wa hesabu za TTCL wao wakiwa wanaiongoza. Wako jikoni kupika hesabu.

Tukalewa harufu ya utumbo huo, MSI/Detcon wakakabidhiwa TTCL wakafanya vitu vyao, ghafla ukaanza mgogoro usioisha juu ya albaki yetu, mara visingizio vikaanza mara TTCL ni hasara tupu, hakuna faida yoyote, hakuna hiki wala kile.

Mwisho wakashitakiana, lakini kesi zikaondolewa mahakamani na serikali ikaishia kulipwa Dola chini ya milioni 10. Yaani zaidi ya Dola milioni 50 (wakati huo bilioni 50 na ushei) zikapeperuka. Utumbo mbaya.

Upo mkataba wa ubia kati ya lililokuwa Shirika la Ndege Tanzania na Shirika la Ndege la Afrika Kusini, ambao ulizaa ATCL, kilichovunwa hapo na ATCL marehemu, utumbo mbaya ukaachwa unatuchefua.

Hatukukifiwa na harufu ya kula utumbo, tukajitumbukiza kwenye ubia kati ya kampuni ya RITES ya India na baada ya kubadili Shirika la Reli nchini (TRC) na kuunda TRL, mkataba wa juzi juzi kabisa, chini ya serikali ya awamu ya nne, hadi tunapowasiliana sasa, hakuna kinachoeleweka ndani ya ATL.

Huduma ni hoi bin taaban, kila mkataba wa kukarabati mabehewa, injini za treni na vifaa vingine vinatoka RITES India kuja kwa mwawe RITES Tanzania anayeshirikiana na serikali ya Tanzania kuunda TRL. Hali ni ngumu kweli, hakuna kinachoeleweka ndani ya TRL, si huduma nzuri, si ukarabati wa mabehewa au injini zake, hali ni ovyo kuliko inavyoweza kuelezwa.

Serikali inaingia mkanganyiko na woga wa kukithiri, haitaki kuvunja mkataba huu ambao unaonekana wazi umetuelemea. Hali ni ya kusikitisha mno.

Upo mkataba wa TANESCO na kampuni ya Richmond wa kufua umeme wa dharura, ambao si tu uliitokea puani serikali baada ya kusababisha baraza zima la mawaziri kusambaratika, bali pia ulifunua uwezo wa ovyo mno wa wataalam wetu. Kukaa na kampuni ya kitapeli bila hata kutambua kiasi cha kuwapa kazi nyeti ya kuzalisha umeme wa dharura megawati 100.

Nimetaja baadhi tu ya mikataba, ukweli ni kwamba ni mlolongo mrefu. Kibaya katika kila mkataba tunaoingia ni kule kushia kula tu utumbo. Katika mazingira haya nani anaweza kubisha kwamba huu si utamaduni wetu?

Kwamba kila kitu kikijirudia kwa staili ileile mara nyingi kila wakati, huo ni utaratibu uliokubalika katika kuendesha mambo. Ni utamaduni. Lakini swali gumu kwa nini watu wetu hawajifunzi hata kwa makosa yao , inakuwaje wasomi wazuri warudie makosa yale yale kila siku? Nani wa kutukomboa?

Kuna shida kubwa hapa huenda mikataba hii ni laana ambayo itatuandama kwa miaka mingi ijayo, nani wa kutuisaidia? Yafaa sasa tuombe Mungu atunusuru.

0
No votes yet