Familia ya Al Gore yasambaratika


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 June 2010

Printer-friendly version
Al Gore na mkewe Tipper

FAMILIA ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani, Al Gore inakaribia kusambaratika.

Tayari Gore na mkewe Elizabeth, maarufu kwa jina la Tipper, wametangaza kuvunjika kwa ndoa yao iliyodumu kwa miaka 40. Hiyo ilikuwa mwezi mmoja uliyopita.

Haikuchua muda, wiki mbili baadaye, mtoto wao mkubwa, Karenna, alitangaza kutengana na mumewe, Drew kutokana kile kinachoitwa, “uhusiano ulioyumba mingoni mwao.” Ndoa ya wapenzi hao wawili, ilidumu kwa kwa miaka 13.

Habari za kuvunjika kwa ndoa ya makamu rais huyo wa 45 wa Marekani zilivuja kupitia barua pepe (email) ambayo Gore na mkewe walikuwa wamewaandikia ndugu, jamaa na marafiki zao.

Gore na mkewe waliarifu marafiki zao na ndugu na jamaa wengine katika barua pepe iliyosainiwa na wote wawili kuwa wamevunja ndoa hiyo kwa hiari yo baada ya kudumu kwa miaka 40.

Wanasema, “kuvunjika huko hakumaanisha mwisho wa urafiki wetu tulioujenga kwa karibu miaka 50 tangu tulipofahamiana.”

Walitaka wote walifahamu hilo na kuliheshimu. Ni kwa sababu huo ni uamuzi wao binafsi na wangependa wote waliache suala hilo kama “letu binafsi na hatutapenda kuona tukiingiliwa.”

Wananchi wengi wa Marekani wameshtushwa na kuvunjika kwa ndoa hiyo ya Gore ambaye alikuwa akionekana kama miongoni mwa watu maarufu nchini humo wanaoheshimu ndoa zao.

Katika miaka minane ambayo yeye alikuwa makamu wa Bill Clinton, watu wengi walikuwa wakimweleza rais huyo kufuata mfano wa makamu wake Gore ambaye ndoa yake haikuonekana kuwa na matatizo.

Taarifa ya barua pepe hiyo ambayo ilionwa na taasisi ya Associated Press ambayo ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuripoti kuhusu kutalikiana huko, haikusema sababu hasa ya kuvunjika kwa ndoa hiyo.

Hatua ya wana ndoa hao kutotoa taarifa rasmi kuhusu sababu ya kutengana, imevifanya vyombo vya habari, hususani “magazeti ya udaku” kuanza kuchunguza suala hilo.

Tayari kuna taarifa kwamba ndoa hiyo imevunjwa kutokana na wivu uliokithiri wa Tipper dhidi ya mumewe. Inadaiwa kuwa katika siku za karibuni, Gore amekuwa a uhusiano wa karibu na wanawake vijana kuliko mkewe.

Sasa Gore anayefanya kazi kama mwanaharakati wa mazingira. Mwaka juzi filamu yake ya muda mfupi inayojulikana kwa jina la Inconvenient Truth, ilipata tuzo maarufu ya Oscar.

Tuzo hiyo, imeongezea umaarufu Gore na sasa amekuwa kivutio kikubwa kwa watu mbalimbali duniani wakiwamo wacheza sinema na wanamuziki, vitu ambavyo vimedaiwa kumnyima raha Tipper.

Hata hivyo, kwa mujibu wa gazeti la News of the World, katika siku za mwisho za ndoa yao, Tipper na Gore walikuwa hawazungumzi vizuri kutokana na kile Gore kuwa huyo alivyo bize.

Gazeti limedai kwamba Tipper, alikuwa akimtaka mumewe apumzike na kutulia nyumbani kulea wajukuu kwa vile familia sasa ina fedha za kutosha, lakini Gore alikataa.

Kukataa kwa Gore kutulia nyumbani kumeelezwa na gazeti hilo maarufu nchini Marekani kuwa ndiyo chanzo kikuu cha kuvunjika kwa ndoa hiyo ambayo ilikuwa ya kupigiwa mfano.

Wiki iliyopita, baadhi ya magazeti hasa yale ya udaku nchini Marekani, yaliandika kwamba ndoa hiyo imevunjika kwa vile Tipper amebaini Gore ana mahusiano nje ya ndoa.

Rafiki wa karibu wa familia ya Gore, Laurie David, ametajwa kuwa kinara wa kusababisha ndoa kuvunjika.

Hata hivyo, mama huyo tayari amekanusha taarifa hizo akisema, “ni uzushi mtupu” na kwamba kwa maoni yake, Gore na Tipper wanapendana kuliko watu wengine wowote aliowahi kuwaona duniani.

Kwa upande wa binti Al Gore, Karenna, yeye ametangaza ya kuwa ndoa yake na mumewe haijavunjika rasmi isipokuwa wametengana kwa muda ili kuweka mambo sawa.

Mara baada ya vyombo vya habari kutangaza kuhusu mgogoro huo katika ndoa ya Karenna na mumewe, Gore na Tipper walifunga safari hadi Washington kwenda kumuona mtoto wao, ingawa nao tayari walikuwa wamekwisha kutangaza kuachana.

Hata hivyo, katika siku za nyuma, Karenna aliwahi kunukuliwa na gazeti moja la Marekani akidai kwamba siku zote amekuwa akiwaona Tipper na Al kama kuwa wanandoa wa aina ya pekee.

“Hawazungumzi mara kwa mara. Wanapenda vitu tofauti sana na kwa kweli kuna wakati unaona kana kwamba hawajazoeana kabisa. Naona ajabu kwamba wameishi pamoja kwa muda wote huu,” alinukuliwa binti huyo akisema siku za nyuma.

Albert Gore na Elizabeth (Tipper) Aitcheson walifunga ndoa mwaka 1970 baada ya kuwa wapenzi kwa takribani miaka mitano.

Watu hao walikutana katika miaka ya 1960 wakati wakiwa wanafunzi katika shule ya St. Albans na walianza rasmi uchumba mwaka 1965.

Familia yao ilijaaliwa kupata watoto wanne, Karenna, Kristin, Sarah na Albert.

Gore anatoka katika familia ya kisiasa na wakati anazaliwa mwaka 1948, baba yake mzazi, aliyekuwa Seneta wa Jimbo la Tenessee, Albert Gore, alitoa picha yake katika ukurasa wa kwanza wa gazeti maarufu la jimbo hilo.

Seneta huyo alikuwa amekaa miaka kumi bila ya kupta mtoto baada ya kumzaa mtoto wake wa kwanza, Nancy, mwaka 1938, na alikuwa amekula kiapo kwamba atakapozaa mtoto wake wa kwanza wa kiume atahakikisha anatoa picha gazetini.

Mwaka 1988, Gore alitangaza rasmi nia yake ya kutaka kuwania urais wa Marekani akiwa na umri wa miaka 40, lakini alishindwa katika mchakato wa ndani ya chama chake cha Democrat na Michael Dukakis.

Mwaka 1992, Clinton alimteua Gore kuwa mgombea wake mwenza katika uchaguzi mkuu ambapo walimshinda George Bush na kuingia ikulu.

Mara baada ya kuwa makamu kwa muda wa miaka nane, Gore alijitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Marekani mwaka 2000, ambapo alishindwa na George Bush wa chama cha Republican, katika matokeo ambayo yamezua utata mkubwa hadi leo.

Je, huo ndiyo utakuwa mwisho wa historia ya kuigwa ya Gore; sasa atatumbukia katika kashifa kama ilivyokuwa kwa bosi wake Clinton? Hilo ndilo swali ambalo wengi wanalisubiri majibu yake.

0
No votes yet