Familia yabana polisi Tabora


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 04 August 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

JESHI la Polisi halijafikisha mahakamani hata mtu mmoja kwa mauaji ya kikatili yaliyomfika diwani wa kata ya Ibiri, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, karibu mwaka sasa, MwanaHALISI imebaini.

Mzee Salum Said Mgeleka aliyekuwa maarufu mjini Tabora na nguvu kubwa ya siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliuawa kwa kupigwa risasi na vijana wawili waliopakizana kwenye pikipiki, akiwa karibu na nyumbani kwake, mtaa wa Kanyenye, mjini Tabora.

Tukio hilo lilitokea kiasi cha saa 3.30 usiku wa 19 Desemba, mwaka jana.

Uchunguzi wa kina wa MwanaHALISI, umebaini kwamba polisi wameshindwa kukamata na kushitaki hata wale watu wawili ambao marehemu aliwataja mbele ya polisi, dakika chache kabla ya kukata roho hospitalini Kitete.

Taarifa zilizofikia gazeti hili zimesema kuwa baada ya upelelezi wao, polisi walikamata watu sita, hapo Januari Mosi mwaka huu lakini, baada ya kuwekwa ndani kwa siku sita, waliachiwa huru.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emson Mmari, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kukiri pia kwamba hakuna mtu aliyefikishwa mahakamani hadi wiki iliyopita.

Kamanda Mmari aliyezungumza kwa simu na mwandishi wa habari hizi, alisema ni kweli walikamata watu sita na kuwaachia baada ya kukosa ushahidi unaowagusa.

"Bado tunaendelea kutafuta wahusika hasa wa tukio hili. Tunajua, kama unavyosema kuwa muda ni mrefu umepita, lakini nadhani unajua upelelezi wa tukio la mauaji unachukua muda mrefu mpaka utakapopata ushahidi makini," alisema Kamanda Mmari.

"Hiyo ni shida sana maana ushahidi wa tukio la mauaji unatakiwa kumgusa moja kwa moja mtuhumiwa. Huu hatujaupata ndio maana tunaendelea kutafuta wahusika," alisema alipoulizwa kama ushahidi wa mazingira hauwezi kuwa kianzio hasa kwa kuwa marehemu alitaja majina ya watu alioamini walimshambulia.

Kuhusu madai kwamba Jeshi la Polisi mkoani Tabora limeingia ndani ya mgogoro na wanafamilia wa marehemu kutokana na namna walivyoshughulikia kesi hiyo, Kamanda Mmari alisema:

"Nina uhusiano mzuri na wanafamilia. Walikuja hapa ofisini kwangu nikawasikiliza; nami niliwaelewesha tunachokifanya. Nadhani walinielewa bali kama hawakunielewa, sasa hilo ni suala jingine," alisema.

Alipoulizwa iwapo polisi wameshinikizwa na baadhi ya viongozi wakuu wa dola kuacha kufuatilia wahusika halisi, haraka Kamanda Mmari alisema, "Hakuna kitu kama hicho. Mimi natangaza kwa mtu yeyote mwenye kujua wahusika aje kwangu binafsi."

"Si kweli kwamba sisi polisi tunalinda wahusika kwa maslahi ya watu fulani. Hatujapata mhusika ndio maana nasema, na tusaidie kuwaeleza wananchi, nipo tayari kuwasikiliza," alisema.

Kulingana na taarifa zilizopo, kabla ya kukata roho hospitalini, marehemu alitaja majina ya watu wawili, ambao wanafamilia wanadai walihusika kutekeleza mpango wa mauaji hayo.

Mmoja wao, habari zimesema, alitajwa kwa jina la Rajabu Hussein Telepi, ambaye anasadikiwa amejificha wilayani Uyui. Pia kulikutwa karatasi kwenye suruali ya marehemu yenye majina ya Omari Rajabu Mhaya (Magasi) na Yaduni Rajabu Mhaya.

Zipo taarifa kuwa polisi walifanikiwa kumhoji mzee Mgeleka kitandani kama kuna anaowashuku kumshambulia.

Taarifa zinasema alitaja watu kadhaa waliopanga mpango huo katika vikao vya Chama cha Ushirika cha Msingi cha Tupendane, wakiwemo baadhi ya viongozi wa CCM Wilaya ya Uyui na wale wa Ofisi ya Ushirika Wilaya ya Uyui.

Waraka wa wanafamilia uliotumwa MwanaHALISI unaeleza kuwa baada ya baba yao kutoa maelezo machache, alilalamika kuwa anajisikia vibaya na kwamba labda angewaeleza zaidi pindi akipata nafuu. "Ghafla alikata roho," umeeleza waraka huo.

Hata hivyo, Kamanda Mmari amekiri kuwepo mtu mmoja anayeshukiwa kuhusika na ambaye alisema wanamtafuta. Alikataa kumtaja kwa jina kwa alichokiita "itaharibu upelelezi."

Imeelezwa kwamba kijana huyo na wenzake wamekuwa wakilindwa na viongozi wa serikali mkoani Tabora kwani baadhi yao wamo waliotamka ndani ya kikao kuwa "Mzee lazima aangamizwe."

Waraka wa wanafamilia unalaumu hatua ya polisi kuachia watu waliokamatwa awali, kwa vile "kulitoa mwanya kwao kujipanga upya na kuandaa kamati ya kuua zaidi ndugu zetu walioonekana kufuatilia kesi hii."

Waraka unaendelea kudai, "Waliandaa kikao pamoja na wauaji halisi (waliompiga risasi Mzee). Tulitoa taarifa hii polisi na kufanikisha kuwakamata. Lakini nao waliachiwa huru huku polisi wakidai hakuna ushahidi."

Polisi inatuhumiwa na wanafamilia kwamba imekuwa ikitoa habari za kipelelezi kwa watuhumiwa, kitendo kinachohatarisha usalama wa familia na kupoteza haki stahili lakini kamanda Mmari amekana.

"Ukipeleka maelezo kituo kikuu cha Mkoa (Tabora) leo asubuhi basi jioni yake unasikia yote mliyoisaidia polisi juu ya watuhumiwa. Jamii ilikuwa inatoa ushirikiano lakini sasa wanarudi nyuma kwa kuhofia vitisho vya watuhumiwa," unadai waraka huo.

Kuna mtazamo kwamba chimbuko la mauaji ya Mzee Mgeleka ni nguvu zake kisiasa mkoani kiasi cha kuwepo makundi mawili yanayohusisha viongozi waandamizi wa CCM.

Kwa sasa, maisha ya wanafamilia yanatajwa kuwa katika wasiwasi kutokana na kung'ang'ania wahusika kufikishwa mahakamani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: