Faragha ya ikulu mashakani


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

FARAGHA ya ikulu iko mashakani. Ujenzi wa majumba makubwa na marefu karibu na Kitalu Na. 1, Mtaa wa Luthuli, Dar es Salaam ambako ni makao ya rais, unatishia faragha hiyo.

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam walioongea na mwandishi wa habari hizi wamesema kuna uwezekano wa kila kinachofanyika ikulu kuonekana kwa walio katika majumba hayo marefu.

“Sasa ikulu watachunguliwa kama tunavyotendewa na wenye maghorofa mitaani; maana kule tunaonekana watupu,” amesema Leticia Magasha mkazi wa Magomeni aliyekutwa karibu na jumba refu lililo mita chache kutoka ikulu.

Mkazi mwingine wa Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini amesema, “Kuonekana unaoga siyo hoja sana; lakini kuna suala la usalama wa ikulu.

“Wanaojenga waweza kuwa na nia njema, lakini watumiaji je?” aliuliza huku akitingisha kichwa mbele ya jengo ambalo linaota kwa kasi.

Hoja za wakazi wa jiji zinatokana na ujenzi wa jengo linalotarajiwa kuwa na ghorofa 19 lililoko pembeni mwa hospitali ya Ocean Road, Barabara ya Chimara, Kata ya Kigamboni, katika wilaya ya Ilala.

Taarifa zinasema jengo litaendeshwa kwa ubia kati ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na kampuni ya Palm Residency Limited.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Evance Balama, alipoombwa kusema lolote juu ya jengo hilo, alisema kwa kadri anavyojua, kibali (building permit) cha ujenzi huo hakikutolewa na Manispaa ya Ilala.

“Kibali kimetolewa na TBA wenyewe maana ndiyo wanaomiliki jengo hilo,” alieleza Balama.

Kuhusu suala la usalama, Balama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani, alishikwa “kigugumizi” kulielezea hilo.

“Kwa kweli kuwepo kwa jengo hilo kwenye eneo lile, si jambo zuri sana. Hadi sasa naendelea kumtafuta meneja wa miradi wa TBA anieleze kwa kina jambo hilo; pia vijana wa Usalama wa Taifa wanaendelea kulishughulikia,” alieleza mkuu wa wilaya.

Jengo linalohusika liko karibu na ikulu kiasi kwamba ni dakika tatu hadi tano kwa mwendo wa miguu wa kawaida.

Afisa Uhusiano wa TBA, Segolena Francis alipotakiwa kuelezea, pamoja na mambo mengine ubia huo, alitaka MwanaHALISI kuandika maswali na kumwachia ili “yafanyiwe kazi na wahusika,” na kwamba majibu yangetolewa wakati wowote wiki hii.

Ujenzi wa jengo hilo ni utekelezaji wa “mpango wa kujiendeleza na kujiimarisha kiuchumi” unaoelezwa kwenye taarifa ya utekelezaji kazi za TBA, kwa miaka mitatu ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne, kuanzia Desemba 2005 hadi Septemba 2008.

Katika taarifa yake ya Januari 2009, wakala huyo anasema ameingia ubia na wadau mbalimbali katika sekta ya ujenzi wa majengo makubwa, kwa kuzingatia sera yake ya uwekezaji.

Jumla ya miradi sita inaelezwa kutekelezwa ambapo mmoja kati ya hiyo ni huo wa ujenzi wa jengo lenye gorofa 19 jirani na ikulu. Miradi yote inatarajiwa kugharimu jumla ya Sh. 65 bilioni.

Taarifa zilizopatikana baadaye zimeeleza kuwa TBA imetoa ardhi ambayo ni kiwanja namba 45 na 46 huku mbia wake akigharamia ujenzi wa jengo hilo.

Taarifa zilizopatikana kutoka chanzo cha uhakika ndani ya ofisi za TBA zinasema mradi ukikamilika, jengo linatarajiwa kutumiwa kibiashara.

Eneo la chini litatumiwa kwa maduka ya bidhaa mbalimbali (shopping centre) huku eneo la juu likikodishwa kwa ajili ya makazi (apartments).

Baadhi ya wafanyakazi kwenye mradi huo wamesema karibu kila anayefika kwenye ujenzi huo na kuambiwa zitajengwa ghorofa 19, huwa anauliza iwapo ikulu imeridhia.

Hata hivyo, wafanyakazi hao wamethibitisha kuwa hawajawahi kuona yoyote akitishia au kushauri usimamishaji wa ujenzi. “Tunafanya kazi kwa kujiamini,” alieleza mmoja wao.

Hadi sasa maghorofa yaliyo karibu na ikulu ni ya urefu wa wastani ya wizara za Elimu na Ardhi na hayatumiki kwa biashara au makazi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: