Fatma Maghimbi ajiziba mdomo


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Fatma Mussa Maghimbi

WANASIASA wengi ni kama samaki aina ya mkizi. Wana hasira ambazo mara nyingine huwaponza na ndiyo kiini cha methali isemayo “ana hasira za mkizi.”

Wavuvi husema samaki huyo anaweza kuruka kwa shabaha ya kukimbia adui, lakini akajikuta ametumbukia katika wavu au dau au mtumbwi au chombo kingine chochote cha kuvulia.

Fatma Mussa Maghimbi, mwanachama na mbunge wa muda mrefu wa Chama cha Wananchi (CUF) amekuwa kama mkizi. Alikwepa kunaswa na adui zake kwa miaka 18, lakini baada ya kukosa mvuto katika chama chake, kwa hasira akaruka na kunaswa kiulaini na adui yake wa miaka mingi – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Fatma aliyezaliwa 10 Desemba 1946, alipata hasira za mkizi baada ya wanachama wa CUF kumchoka, hivyo kumnyima nafasi ya kutetea ubunge katika Jimbo la Chake Chake, Pemba. Naye akaona heri kumezwa na papa, CCM.

Aliyopigania

Aliposoma  bungeni, maoni ya kambi ya upinzani katika bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2008/2009, aligusia hoja za katiba mpya, mgombea binafsi na mahakama ya kadhi.

Alikumbusha kuwa, katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2007/2008 alipendekeza haja ya kupitia vipengele 12 ili kupata Katiba mpya, lakini alisikitika hadi 4 Agoti 2008, alipokuwa anasoma hotuba ya mwaka 2008/2009, hakukuwa na dalili ya mabadiliko yoyote.

Alisema, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa suala la  kuwa na katiba mpya Tanzania ni la msingi, haliepukiki na lisifumbiwe macho, hivyo basi katiba mpya itungwe kwa kuwashirikisha wananchi wote kwa utaratibu utakaoandaliwa na pia kupitia vikundi mbalimbali vya kijamii, vyama vya siasa na viongozi wa kidini.

Kuhusu suala la mgombea binafsi, alisema nchi yoyote inayopenda utulivu ni lazima iheshimu sheria, demokrasia ya kweli na haki za binadamu; ikijumuisha kutoa haki za msingi kwa raia. Tanzania inaonekana inayumba katika kuheshimu mambo hayo matatu.

Suala la kuwa na mgombea binafsi ni la msingi, kilio cha muda mrefu na haliwezi kupuuza kwa sababu linaungwa mkono na Watanzania wengi.

Akitoa mifano alisema, nchi nyingi duniani na hata za kiafrika, kwa sasa zinaruhusu mgombea binafsi na alitolea mfano Ghana, Namibia na Rwanda. Kwa msingi huu lisingekuwa suala jipya iwapo Tanzania nayo itaruhusu mgombea binafsi katika nafasi mbalimbali za uchaguzi. Amefanikiwa?

Halafu alishupalia hoja ya Mahakama ya Kadhi, akisema suala la uanzishaji wa mahakama hiyo ni jambo la msingi na lisiloepukika kwa sasa. Ilani ya CCM iliona umuhimu wa mahakama hiyo.

Hii ni kwa sababu kutokuwepo kwa mahakama hiyo ni kikwazo katika utatuzi wa masuala ya msingi yanayowahusu waislam.

Utetezi wa mahakama hii ni kutokana na msingi kwamba kuna uthibitisho wa wazi kwamba yapo mambo maalum yanayohitaji kuwepo na kushughulikiwa na mahakama maalum kama ilivyo kwa mahakama ya biashara, mahakama ya ardhi, mahakama ya kazi.

Serikali ya CCM imelipatia ufumbuzi kwa kurejesha kwenye mahakama za kawaida isipokuwa iliwataka Waislamu watengeneze sheria, zipitiwe, zihakikiwe na kuidhinishwa ili zitumike mahakamani. Je, ameridhika na utaratibu huo; maana hakuridhika akiwa CUF?

Alikuwa ngangari, muumini wa siasa za jino kwa jino na aliyepita popote kudai CUF iliporwa ushindi wa urais mwaka 1995, 2000 na 2005. Alishirikiana na Prof. Haroub Othman kuanzisha kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Zanzibar.

Upemba

Lakini miezi mitano tangu mwanasiasa huyo atemwe katika kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Chake Chake, anasema “Upemba umezidi katika Jimbo la Chake Chake.”

Halafu amekaririwa akisema chama kimetawaliwa na rushwa kupita kiasi na ilikithiri katika uchaguzi wa kura za maoni.

Je, rushwa imezidi ile katika chaguzi za CCM kuanzia mwaka 2007 wakati wa kupata wenyeviti wa matawi, wilaya, mikoa wawakilishi wa halmashauri za wilaya, mikoa na taifa?

Je, ni kuzidi wakati wa kupata viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji  mwaka jana? Au kuzidi namna CCM ilivyopata wagombea ubunge mwaka huu?

Mtu akifuatilia utendaji wa Maghimbi, atagundua hizi ni hasira za mkizi. Fatma amekuwa mkurugenzi wa kitengo cha wanawake tangu mwaka 1992, huku mwanamama huyo mwenye shahada ya uzamili katika sheria akiwa bado mfanyakazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka 1995 alishawishiwa na Mussa Haji Kombo agombee ubunge katika Jimbo la Chake Chake na akashinda. Halafu aliteuliwa kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni.

Mwaka 2000 aliwania tena lakini walifanyiwa mizengwe na CCM. Mwaka 2005 aliwekewa pingamizi kuwa yeye si mkazi wa Pemba, lakini akasaidiwa na viongozi wa CUF akatambuliwa na akapitishwa katika kura za maoni baada ya kumshinda Kombo aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Uenezi.

Bungeni, Fatma aliteuliwa kuwa waziri kivuli wa Wizara ya Sheria, Katiba na Utawala Bora

Hata hivyo, alikabiliwa na tatizo moja kubwa kujisahau. Aliporejea safari hii alipika pilau na akaandaa taarab; watu wakacheza lakini hawakula; na ulipowadia wakati wa kura za maoni Fatma alianguka; nafasi ikachukuliwa na Kombo.

Hakuridhika. Akaenda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kudai kulikuwa na rushwa, lakini akaambiwa haifanyi kazi Zanzibar. Akafunga safari hadi ofisi ya Msajili wa Vyama akitaka iingilie kati akidai kulikuwa na “mobile bank,” yaani rushwa; lakini hakusikilizwa.

Dhamiri

Dhamiri yake itamsuta. Kila alipotoa hotuba kama waziri kivuli wa wizara ya sheria, katiba na utawala bora, alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye wingi wa Rehema kwa kumpa afya njema na kuweza kusimama mbele ya wabunge wenzake aweze kutoa maoni kwa niaba ya Kambi ya Upinzani.

Pili, alikuwa anatoa shukrani kwa wananchi wa Jimbo la Chake Chake kwa imani yao kwake na kuwaahidi kuendelea kuwatumikia kwa uadilifu mkubwa. Kwa umuhimu mkubwa, alikuwa anamshukuru mumewe, Mussa Maghimbi kwa uvumilivu mkubwa kutokana na muda mwingi kuutumia katika shughuli za siasa.

Halafu alikuwa anawashukuru viongozi wa CUF chini ya Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad kwa “uongozi wao makini” katika juhudi za kutetea Watanzania, ustawi na maendeleo ya taifa.

Leo,Maghimbi anaona CUF ni chama kibaya na kina upemba baada ya kukosa ubunge? Amepata wapi mapenzi na CCM aliyoilalamikia na kuiponda kwa takriban miongo miwili? Atapiga kelele au amejiziba mdomo?

Je, Katiba mpya imeshapatikana? Kama yeye aliyekuwa anapigania katiba mpya amebwaga manyanga, jamii iamini alikuwa anasukumwa na maslahi binafasi?

Huko aliko, ataungana na nani kudai katiba mpya wakati CCM wote hawaoni haja ya kuwa na katiba mpya? Amejiziba mdomo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: