Fedha za EPA ni za umma


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 02 September 2008

Printer-friendly version

USHAHIDI unaendelea kupatikana kwamba zile zinazoitwa fedha za EPA ndani ya Benki Kuu (BoT) ni fedha za umma.

Rais Jakaya Kikwete, akihutubia bunge, Alhamisi 21 mwezi uliopita, alisema fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) “hazina mwenyewe” na kuongeza kuwa ni fedha ambazo “zinazagaazagaa” BoT.

Jumla ya Sh. 133 bilioni zilichotwa na makampuni binafsi kutoka BoT, mengi yakiwa yamethibitika kuanzishwa kwa nyaraka za kugushi.

Sasa kuna ushahidi kuwa fedha za EPA zina wenyewe, hazizagaizagai BoT na ushahidi zaidi unasema ni fedha za umma.

Imefahamika kuwa makampuni mengi yaliyopeleka fedha zake NBC na CRBD kulipia bidhaa kutoka nchi za nje yalikuwa makampuni ya umma.

Mfano mkuu unaotolewa ni ule wa uagizaji magari na spea zake katika miaka ya 1980 hadi 1990.

Magari na spea zake viliagizwa na Shirika la Magari la Taifa (State Motor Corporation- SMC), ambalo liliuza bidhaa hizo kwa fedha za Tanzania.

Miongoni mwa wanunuzi wa vifaa hivyo walikuwa K.J. Motors, Kampuni ya Kuunganisha Matrekta (TRAMA), Kampuni ya Kuunganisha Magari (TAMCO), Tanzania Motor Services (TMS), Cooper Motors na Tanganyika Motors.

Karibu makampuni yote ya umma, ambayo hayakuwa na fedha za kigeni, katika kipindi cha 1980 hadi 1990 yaliweka kiasi kilichohitajika katika mabenki ya NBC na CRDB kwa kuongeza asilimia 10 ya gharama ili kukabiliana na kushuka kwa thamani ya fedha za ndani.

Mabenki yaliyosimamia waagizaji yaliwekeana mikataba na waleta bidhaa. Ni kutokana na mabenki hayo kuendelea kukosa fedha za kigeni, yalikubaliana na BoT kwamba fedha hizo zihamishiwe kwenye akaunti maalum inayoitwa EPA.

Kwa mtindo huu, makampuni ya umma yalikuwa yanadaiwa na makampuni mengi ya nje ambayo baadhi yao pia yalikuwa ya umma au serikali zao zilikuwa zina hisa katika makampuni hayo.

Si hivyo tu, makampuni hayo ya nje yalipopata hasara ya kutolipwa na yale ya “dunia ya tatu” – nchi zinazoendelea – Tanzania ikiwamo, yaliingizwa katika mpango maalum.

Ama makampuni hayo ya nje yalipewa fidia na serikali zao au yalilipwa kwa bima za biashara katika nchi dhaifu kiuchumi kama Tanzania wakati huo.

Katika hali hii, baadhi ya makampuni ya nje yalilipwa; mengine baada ya kusubiri kwa muda mrefu, yaliifutia madeni serikali ya Tanzania na sasa hayadai. Makampuni mengine ya nje hayapo tena.

Hivyo fedha zilizosalia ni za benki ya umma; ni za umma. Hakuna kampuni ya ndani inayodai BoT kutokana na fedha hizo, kwani tayari waliishapata bidhaa na kuziuza.

Katika mahusiano ya biashara kimataifa, kuna kitu kinaitwa "status of limitation" – muda wa kudai na kudaiwa. Kama usipodai deni lako kwa kipindi fulani, tuseme miaka kumi (hii inapishana hapa na pale), unapoteza haki yako ya kudai.

Tanzania imeishafunga au kuuza karibu mashirika yake yote ya umma ambayo yalikuwa yanahusika na fedha hizo za EPA.

Wale wanaodaiwa kuwa wadai, watakumbwa na muda wa ukomo huu wa kudai endapo watajitokeza miaka zaidi ya 25 toka deni liwepo.
 
Bali kuna hoja muhimu hapa. Fedha zote zilizoko benki huwa fedha za benki na hulindwa na benki na bima zake. Katika Tanzania BoT ni mali ya umma.

Katika hili, fedha zote, kutoka makampuni na mashirika ya umma na hata makampuni machache binafsi, ambazo ziliwekwa benki wakati huo, zilikuwa zinamilikiwa na mabenki ya umma kwa asilimia miamoja.

Fedha zikipotea mikononi mwa benki; tena benki ya umma; basi umma umepata hasara na wahusika katika benki hawana budi kuzilipa au kuwajibishwa ipasavyo.

Kwa mantiki hiyo, fedha zote zilizokuwa CRDB na NBC halafu zikahamishiwa BoT, zilikuwa, na bado ni, fedha za BoT ambayo ni mali ya umma. Ni fedha za umma wa Tanzania.

Ushahidi upo kwamba fedha ziliibwa benki; benki ni ya umma na kwa maelezo hapo juu, fedha ni za umma. Rais anamwambia nini aliyefungwa kwa wizi wa kuku?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: