Fedha za safari za JK zaibwa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete safarini

MAOFISA watano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuiba fedha zilizotengwa “kwa ajili ya safari za rais,” MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za uhakika zilizopatikana ndani ya ikulu na wizara hiyo, zimesema kwamba maofisa hao, akiwemo Mkuu wa Itifaki, walifanikiwa kuchota Sh. 3 bilioni “kutoka benki moja nchini.”

Kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa, fedha hizo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya safari za rais katika ziara za nje ya nchi.

“Hizi fedha zilikuwa zitumike kwa ajili ya kugharamia huduma mbalimbali wakati rais akiwa kwenye safari za kikazi nje ya nchi,” amesema mmoja wa watoa taarifa.

Maofisa waliohusishwa katika kashfa hiyo ya ufisadi ni pamoja na Mkuu wa Itifaki aliyetajwa kuwa ni Anthony Itatiro.

Vyanzo vya taarifa vimetaja maofisa wengine kuwa ni ofisa katika Idara ya Itifaki, Shamim Khalfa; Kaimu Mhasibu Mkuu, Kasim Laizer; Mhasibu aitwaye Deltha Mafie na karani wa fedha (mtunza fedha) aitwaye Shabani Kesi.

Wote tayari wamesimamishwa kazi yapata wiki mbili sasa ili kutoa nafasi kwa uchunguzi.

Maofisa hawa wanaendelea kukaa nje ya kazi na tayari uchunguzi umeanza, mtoa taarifa ameeleza.

“Wizi huu umefanywa kwa ustadi mkubwa. Walikuwa wameshatoa fedha zote benki. Sijui mpango wao ulikuja kufichuka vipi wakati inasemekana tayari walishapanga jinsi ya kugawana. Ila sielewi kama wamegombana,” ameeleza.

Watoa taarifa hawakuweza kujua benki gani fedha hizo zilitolewa na kutoka akaunti gani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule hakupatikana ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo, licha ya jitihada kubwa ya kumpata kwa njia ya simu ya mkononi.

Mara kadhaa simu yake Na. 0784 605933 ilipopigwa iliita hadi kukatika, bila ya kujibiwa.

Mwandishi wa MwanaHALISI alipomtafuta Afisa Habari wa wizara, Assah Mwambene, alijibu kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) akisema kuwa Katibu Mkuu “yupo kwenye kikao pamoja na mabalozi wapya walioapishwa.”

Baadaye alipopigiwa simu kutoa ufafanuzi, Mwambene alisema yuko Dodoma na katibu mkuu ameahidi akimaliza kuongea na mabalozi, ataongea na MwanaHALISI.

Taarifa nyingine zilizopatikana wakati tukienda mtamboni zilisema, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ameunda tume ya kuchunguza tukio hilo.

Mtoa taarifa amesema Balozi Sefue ameipa tume hiyo mwezi mmoja, hadi Julai 4 kukamilisha uchunguzi na kumkabidhi ripoti.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: