Ferguson aifutia England ubingwa Kombe la Dunia


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version
Michezo
Asema haitakuwa na jeuri Afrika Kusini
Sir Alex Ferguson

WAKATI Kocha Fabio Capello wa England, akitamba ataonyesha maajabu ya soka kwa kuipa ubingwa wa kwanza baada ya miaka 43, kocha mkongwe wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amemkata maini, akisema ni miujiza kwa timu hiyo kutwaa Kombe la Dunia.

Amedai kwamba, hana chembe ya imani na England licha ya kuwa ana nyota tisa katika timu ya taifa.

Nyota wa United katika kikosi cha England ni pamoja na Wayne Rooney, Rio Ferdinand, Michael Carrick, Wes Brown na Ben Foster ambao wana kila dalili za kuwamo katika kikosi cha mwisho kitakachokwenda Afrika Kusini wakati Owen Hargreaves, Michael Owen, Gary Neville na Danny Welbeck wanajaribu kumshawishi Capello aliyepania kuipa England ubingwa wa kwanza wa Dunia nje ya Ulaya.

Badala yake, kocha huyo anayeinoa United kwa miaka 23 sasa, anaielekeza kete yake kwa Brazil.

“Sioni wa kuizidi kete Brazil,” anasema Capello aliyeitabiria kutwaa ubingwa wa dunia kwa mara ya sita tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 1930.

"Msimu uliopita, Brazil ilikuwa na mastaa 103 katika klabu za Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati England ilikuwa na wachezaji 15 tu.

“Nyota wengi wa Uskochi walicheza Ligi ya Mabingwa msimu uliopita kuliko wa kutoka England.

Kwa mara ya kwanza na ya mwisho England ilitwaa ubingwa wa Dunia mwaka 1966 nchini England.

"Idadi ndogo ya nyota wa England ni ndogo kulingana na Ligi ya Mabingwa ilivyopanuka.

“Tujiulize, kwa stili hii utatengeneza timu gain bora ya taifa? Ndiyo maana nasema hakuna kitu kwa Waingereza."

Naye, gwiji wa soka wa Ureno, Luis Figo amebainisha wazi kwamba anaamini England haina nafasi ya kulitwaa taji la Dunia kwenye fainali zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Baada ya kuwa na mafanikio mazuri wakati wa kufuzu kwa fainali hizo, England maarufu zaidi kama Simba Watatu, wanapewa nafasi ya kufanya vizuri kwenye michuno hiyo, lakini Figo kwa upande wake anaona kwamba nafasi hiyo wanayo Hispania, Brazil na Argentina.

Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid, pia ametabiri kwamba timu moja kutoka Afrika itafanya maajabu kwenye michuano hiyo kutokana na ukweli kwamba inafanyika kwenye ardhi ya kwao.

“Hispania, Brazil na Argentina ndiyo timu ambazo kwa sasa zipo kwenye kiwango bora zaidi na pengine kutakuwa na maajabu kwa timu kutoka Afrika,” alisema Figo akiliamba gazeti la The Mail.

“Nafikiri kwamba Hispania itakuwa katika kiwango kizuri. Wanacheza vizuri na kwa upande wangu mimi nawapa nafasi kubwa zaidi.”

Figo alistaafu kucheza soka Mei mwaka huu, baada ya kuwa dimbani kwa zaidi ya miaka 20 akicheza katika ngazi ya juu Ulaya.

Wakati England ikiwa imepangwa katika kundi lisilo na ushindani, Figo amesema kwamba Ureno ipo kwenye kundi la kifo ikiwa na Brazil, Ivory Coast na Korea Kaskazini.

0
No votes yet