FFU wakesha kulinda sumu mgodi wa North Mara


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version
Gumzo

ENEO lote kuzunguka bwawa la maji ya sumu yanayotokana na kemikali za kusafishia dhahabu katika machimbo ya Nyabirama mgodi wa North Mara, wilayani Tarime mkoa wa Mara linalindwa usiku na mchana.

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambao wana mkataba wa ajira na serikali na wanalipwa kwa fedha za umma, ndio wanalinda kampuni ya nje kwa bunduki zinazotumia risasi za moto.

Wakati wote kuna askari wanaozunguka eneo hili kwa kutumia gari aina ya Land Rover. Vilevile kuna wanaosimama juu ya tuta la mawe kuzunguka bwawa hilo.

Kazi kuu ya askari hawa ni kuzuia wananchi kufika kwenye tuta hilo linalovujisha sumu inayotiririkia kwenye makazi na mashamba yao.

Hili ni eneo la hasira na ghadhabu. Wenyeji ama hulazimika kupita mbali au hupita kwa kasi wakijaribu kuepuka hasira za FFU.

Msafara wa diwani wa kata ya Matongo ulipita karibu na tuta hili la mawe ambayo baadhi ya vijana huokota na kukokotoa (au wanasema kuchakata) mabaki ya dhahabu ili wauze na kupata fedha za kujikimu.

Haikuwa rahisi kwa msafara wa diwani kuepuka kibano cha walinzi wa mgodi wanaotumikia “mabwana wawili” – serikali (ulinzi wa raia na mali zao) na tajiri anayemiliki mgodi.

“Wewe ni nani?” Alihoji askari mmoja akiwa ameshika silaha yake vizuri kama aliyetayari kufyatua.

“Mimi naitwa Machage Machage, diwani wa kata ya Matongo,” alijibu mwongozaji msafara. Aliongeza, “Nimepata taarifa kwamba bwawa hili bado linavujisha sumu. Nimekuja kuhakikisha.”

“Sawa, na mimi nakujua kuwa ni mheshimiwa diwani wa hapa, lakini si unajua utaratibu wa watu wanaotaka kuja huku? Kwanza unatakiwa kuripoti ofisini ndipo wakuruhusu,” alisema askari huyo.

Polisi alipigwa butwaa pale diwani Machage alipomjibu kwa ujasiri, “Hivi unataka mimi niombe ruhusa kwanza ili nije kutembelea eneo langu? Nasema, mgodi huu uko ndani ya eneo langu; siwezi kusubiri ruhusa.”

Huku polisi akiwa bado anatafakari anachokisikia, Machage akaendelea, “Watu wamelalamika, hivyo nawajibika kuthibitisha kabla ya kwenda ndani kulalamika.” Hali hiyo ilikuwa kabla ya kuwasili Land Rover iliyosheheni askari wenye silaha.

Mara askari mmoja miongoni mwa waliotoka katika Land Rover akaanza kumhoji diwani kwa kasi na sauti ya kushurutisha huku akimnyoshea kidole mwandishi.

Polisi: Yule ni nani?
Machage: Yule ni mheshimiwa diwani
Polisi: Mbona alikuwa anapiga picha?
Polisi mwingine: Isije akawa mwandishi wa habari! Hatutaki kuona kesho tumetokea kwenye magazeti; sisi tuko kazini. (Polisi anasogea kunihoji).
Machage: Hakuna ubaya wowote. Kumbukeni kwamba hili ni eneo langu la uwakilishi; siwezi kusubiri ratiba ya kampuni ya kufanya ziara. Watu wangu wamekuja na malalamiko nami nimeitikia wito.
Polisi mwingine: Utafanya nini wakati maji yanavuja na yatazidi kuvuja kila inaponyesha mvua (kauli ya kejeli lakini huku tukiondoka baada ya ukali wao kuyeyuka)?

Hakuna siri. Maji ya sumu yatokanayo na kemikali ya “cyanide” inayotumika kusafisha dhahabu, yanavuja kila sehemu ya tuta hilo linalolindwa kwa mtutu wa bunduki za umma.

Kampuni imechimba mashimo mawili tu ya kukusanyia maji yenye sumu. Maji haya hurudishwa tena bwawani kwa kuvutwa kwa mashine.

Hayo ni maeneo mawili tu, kwingine tuta lote linavuja na maji yenye kemikali yanatiririka moja kwa moja hadi kwenye makazi ya kaya za familia tano zilizosalia eneo hilo.

“Haya maji unayoyaona yanavuja chini kwa chini kutoka kwenye bwawa lile. Watoto wanaugua mara kwa mara; mifugo inakufa kwa kunywa maji haya,” anasema Kennedy Amos.

Kennedy pamoja na ndugu zake, Samson Amos, Chacha Amos, Amos Marwa Rhobi na mzee Marwa Rhobi Maningo mwenye familia ya watu 19 wakiwemo wake saba, kwa miaka mitano wameshindwa kulima chochote.

Wanasema wakipanda chochote katika mashamba yao kinaoza. Muda wote wakazi huvaa buti kwa vile nyumba zao zimezingirwa na maji ya sumu kutoka mgodini.

Majani katika mashamba ambayo hayajapaliliwa kwa muda mrefu yanaonekana yameozea katika maji yenye rangi nyekundu na yanayotoa harufu ya uozo; huku mengine yakibubujika katika mazizi ya mbuzi, ng’ombe na kondoo na kuzingira nyumba na maeneo mengine.

“Kama unavyoona,” analalamika Maningo, “maji ya sumu bado yanaendelea kuvuja na kutuathiri. Kwa miaka mitano sasa hatulimi eneo hili, mazao hayastawi, eneo lote limejaa sumu.”

“Kwa sasa tunatangatanga; tunaomba maeneo ya wengine, mwaka hadi mwaka ili tuweze kupanda chochote,” anasimulia Maningo.

Anasema aliwaambia wenye kampuni inayomiliki mgodi kwamba yuko tayari kuhama lakini wamlipe fidia inayolingana na hasara aliyopata na mali alizonazo.

Maningo aliwapigia hesabu ya chai ya asubuhi, chakula cha mchana na jioni kwa siku, mwezi, mwaka na kwa miaka mitano bila kuweka thamani ya nyumba na mashamba. Alisema anastahili fidia ya Sh. 273,600,000.

Hesabu zake zinaonyesha kama ifuatavyo: Chai asubuhi Sh. 2,000 kwa kila mtu kwa watu 19; chakula cha mchana Sh. 3,000 kwa kila mtu kwa watu 19 na chakula cha jioni Sh. 3,000 kwa kila mtu kwa watu 19. Jumla: Sh. 152,000 kwa siku.

Kiasi hicho kwa mwezi ni sawa na Sh. 4,560,000; kwa miezi 12 ni sawa na Sh. 54,000,000; na kwa miaka mitano – kuanzia 2004 hadi 2009, ni jumla ya Sh. 273,600,000.

Baada ya mvutano wa muda mrefu juu ya fidia ya mzee huyo na wenzake wanne, hatimaye mgodi ulituma wawakilishi hivi karibuni waliofika kufanya tathmini ya kitaalamu ya mali zake – mashamba, mazao, mifugo na nyumba.

“Kwanza wametaka kunifidia kwa kunipa ng’ombe 25. Baada ya mjadala wakataka kuniongezea ng’ombe hadi 32. Mimi nikakataa,” anasema Maningo.

Anasema hatimaye wakasema katika tathmini yao wanaona familia zote tano zilipwe fidia ya Sh. 292,341,147 kwa mchanganuo ufuatao.

Maningo alipwe Sh. 156,671,476; Kennedy Amos Sh. 25,282,638; Chacha Amos Sh. 27,621,558; Amos Marwa Sh. 43,513,398 na Samson Amos Sh. 39,252,078,” anafafanua.

Wamiliki wa mgodi wanataka fedha za fidia ndizo pia zitumike kuwajengea nyumba. Hii ina maana kwamba wakikubali malipo ya viwango hivyo, hawatapewa fedha zote kwani nyingine zitakatwa ili kuwajengea nyumba.

Hadi sasa kampuni haijawaita wadau wakuu watano wenye nyumba, mashamba na mali nyingine karibu na mgodi ili kujadiliana juu ya tathimini yake hiyo.

Athari kwa wakazi wa maeneo hayo ziko wazi ingawa vyombo vya serikali vinakwepa kueleza wazi. Mathalani mzuri ni taarifa ya uchunguzi wa mzoga iliyoandaliwa na Bwana Mifugo wa Wilaya ya Tarime, P. Masele tarehe 4 Novemba 2009.

Taarifa inasema, “Nimepima mzoga wa ng’ombe aliyekufa tarehe 4 Novemba 2009; sijui chanzo cha kifo,” ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na bwana mifugo huyo ambayo nakala yake ilipelekwa pia mgodini.

Majibu ya bwana mifugo huyo yanafanana na majibu ya serikali bungeni kwamba imekosa pesa kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa kina juu ya athari za sumu kwa binadamu kama ilivyolalamikiwa mwaka jana.

Athari za maji ya sumu hiyo zililalamikiwa kwa mara ya kwanza mwaka jana na diwani wa kata ya Kibasuka, Joseph Suleiman akisema tayari watu na mifugo kadhaa imekufa katika vijiji vya Nyakunguru, Nyarwana, Weigita na Nyangoto.

Katika taarifa yake ambayo vyombo vya serikali vimekuwa vikihofia kuweka wazi, alisema sumu kutoka mgodini ilisababisha vifo vya watu 43, ng’ombe 401, mbuzi 523, kondoo 185, punda 63 na mbwa 227.

Maji yenye sumu itokanayo na kemikali aina ya cyanide inayotumika kusafishia dhahabu, ndiyo yanavuja kutoka machimbo ya Nyabirama na kuingia kwenye visima na Mto Timbo kabla ya kuingia Mto Tigithe na baadaye Mto Mara halafu Ziwa Victoria.

Maji mengine yenye sumu kutoka machimbo ya Gokona yaliingia moja kwa moja katika Mto Tigithe halafu Mto Mara kabla ya kumwaga maji katika Ziwa Victoria.

Kampuni ya Barrick ilikiri mbele ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai iliyotembelea mgodi huo, kwamba maji yenye sumu ya paf (potential acid forming material), ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu, yanatiririkia Mto Tigithe.

Kamati ilishuhudia baadhi ya watu wakiwa wamechubuka mikono, midomo na miguu; wenye upele na ngozi iliyoharibika; na ikapokea malalamiko ya baadhi ya akina mama kuhusu mimba kuharibika ikiwa ni athari ya sumu hiyo ya paf na cyanide.

Bali mwanzoni mwa mwaka huu, kamati ya Ndugai ilivaa “miwani ya mbao” na kushindwa kuona maji yenye sumu ya paf katika machimbo ya Gokona yanayoendelea kutiririkia mtoni; wala cyanide katika machimbo ya Nyabirama.

Mgodi wa Nyabirama una mawe aina ya naf (non- acid forming material). Mawe haya hayana kemikali.

Lakini mawe ya mgodi wa Gokona yana kemikeli/sumu na ni hatari. Kamati ya Ndugai ilielezwa mwaka jana kwamba mawe yenye paf yakinyeshewa mvua hutoa kemikali ambayo huweza kuunguza kama maji ya betri.

Diwani wa kata ya Kemambo, Augustino “Neto” Sasi anasema tatizo bado lipo hadi leo.

“Walichofanya ni kuhamisha kifusi cha mawe yenye sumu na kukiweka ndani ya machimbo ya Gokona ambako si rahisi watu kuingia. Ushahidi upo, maji ya sumu hayaingii kwenye bwawa lenye zulia; yanapita chini kwa chini hadi mtoni,” anasisitiuza Sasi.

“Ukifika kwenye mto eneo la usawa na machimbo, utaona maji yakiwa tofauti na yale yanayotoka juu yake,” anasema.

Ndivyo ilivyo pia kwa upande wa Nyabirama, ambako diwani Machage anasema, “Maji ya sumu yanaendelea kuvuja; tuta hili limeshindwa kuyazuia.”

John Matete, afisa mtendaji wa kijiji cha Nyarwana katika kata ya Kibasuka anasema, “Hali haijatengemaa bali matukio yamepungua kwa kiasi fulani; kwani baada ya kilio cha wananchi, serikali ilikuja kuangalia hali ingawa hawajarudi tena.”

Matete anasema, “Serikali imekuja kupima mahali pa kuchimba visima maeneo ya Nyakunguru, Nyarwana na Weigita; na madaktari kadhaa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili walikuja kuchukua sampuli za damu.”

Yote haya yasingetokea endapo serikali ingefuata ushauri wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC). Mwaka 2008 Baraza lilishauri, hasa baada ya kuridhika kuwa kuna sumu inayotokana na shughuli za madini, kwamba ama mgodi wa North Mara ufungwe au watu wahamishwe.

Pendekezo hilo lilikuwa katika ripoti ya NEMC kwenda Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, lakini serikali haijalitekeleza. Nao viongozi wakuu wa nchi wanapofika Nyamongo, ama huziba masikio au hutoa ahadi zisizotekelezeka.

Utafiti uliofanywa na wataalamu watatu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Manfred F. Bitala, Charles Kweyunga na Mkabwa L.K. Manoko kwa kupima maji ya jirani na mgodi, umeonyesha kuwepo kwa kiasi kikubwa cha madini chuma ya Nickel, Cadmium, Lead na Chromium; na cyanide.

Sampuli za maji zilizochukuliwa mwaka jana kutoka Mto Tigithe zinaonyesha viwango vya nickel (Ni), lead (Pb) na chromium (Cr), vilipanda mara 260, 168 na 14 kuliko ilivyokuwa mwaka 2002.

Viwango hivyo viko juu kuliko inavyoelekezwa na NEMC, Shirika la Mazingira la Marekani (EPA) na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Utafiti huo unathibitisha kwamba hali ya afya ya binadamu na viumbe vingine itaendelea kuathiriwa na uchafuzi huo wa mazingira.

Mgodi wa North Mara ulikuwa chini ya kampuni ya East Africa Gold Mine (EAGM) au Afrika Mashariki Gold Mine (AMGM) ya Australia kati ya 1995 na 2003.

Kati ya 2003 na 2006 mgodi uliendeshwa na Placer Dome ya Canada na sasa umechukuliwa na kampuni ya Barrick, pia ya Canada.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: