FIBUCA kuing'oa TUICO


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 18 August 2009

Printer-friendly version

HATIMAYE Chama cha Wafanyakazi wa Asasi za Fedha, Viwanda, Benki, Uzalishaji wa Nishati, Biashara na Kilimo (FIBUCA), kimesajiliwa.

Hati ya usajili ya FIBUCA ni Na. 24 ya tarehe 24 Julai 2009.

Habari zilizopatikana juzi Dar es Salaam na kuthibitishwa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa FIBUCA, Mrisho Rashid zinasema tayari chama hicho kimeanza kazi.

Anasema makao makuu ya FIBUCA yapo jengo la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Msajili wa vyama vya wafanyakazi, Doris Urio alisajili chama hicho baada ya viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), kushindwa kutokea kwenye mkutano uliopangwa kufanyika saa 4.00 asubuhi ya Julai 23 mwaka huu.

Msajili huyo ambaye kwa muda mrefu alishutumiwa na FIBUCA kushindwa kusajili chama hicho kutokana na maelekezo ya TUICO, aliamua kuita viongozi wa pande zote mbiliili kuondoa utata.

Hata hivyo, viongozi wa TUICO walikacha kikao hicho. Baada ya kusubiri kwa saa tatu, ilipofika saa saba mchana, msajili akafanya uamuzi.

Habari zinasema kwamba TUICO walikacha kikao hicho kwa sababu hawakuwa na hoja mbele ya msajili kupinga usajili wa chama hicho huru cha wafanyakazi wa sekta husika.

TUICO iliandika barua nyingi, wakijenga hoja mbalimbali kuipinga FIBUCA, wakidai ni chama cha waajiri.

Baada ya kushindwa kutokea kikaoni, msajili akapata mwanya wa kusajili FIBUCA. Hata hivyo, TUICO walikwenda Mahakama ya Kazi, Agosti 5 mwaka huu kupinga usajili huo.

Kuna madai kuwa TUICO ilitumia kiasi kikubwa cha fedha, ambazo ni michango ya wanachama wake, kukikandamiza FIBUCA.

Kuna ushahidi wa barua kutoka TUICO kwenda kwa makatibu wa kanda na mikoa wa chama hicho, ukielekeza kutolewa kwa fedha kwa ajili ya kazi mbalimbali za kuboresha TUICO.

Barua hiyo ya 8 Juni 2009, yenye kichwa kisemacho 'Muhimu,' Kumbukumbu Na. TUC/CW-F/75, inasema, "Makao makuu yamewatumia fedha kuanzia TSh 1,000,000 hadi 2,000,000/- za kufanya ziara sehemu za kazi zilizoko mkoani kwako penye wanachama wa TUICO."

TUICO imeagiza makatibu wa Kanda na mikoa, kuingiza wanachama wapya, kukusanya malimbikizo na ikibidi sehemu zingine kuelezea mtafaruku ndani ya TUICO. "Maelezo mnayo."

Barua hiyo ilielekezwa kwa matawi katika ofisi za NSSF, NMB, NBC, CRDB na makampuni ya Bia.

Katika kutia mkazo huo, TUICO inaeleza, "Sehemu hizi zijulikane ili tulete nguvu za ziada."

Barua hiyo yenye kipengele kingine cha kikao cha makatibu inasema, "Kila katibu atatoa taarifa ya sehemu za kazi, ambazo hawajajaza form No. 6 (Fomu Na. 6) na sehemu ambazo zina wafanyakazi wengi, ambao si wanachama, ili tukusaidie kuwaingiza kwenye chama.

"Katibu wa Mkoa aeleze bila kudanganya mafanikio yake ya kupambana na FIBUKA (FIBUCA).

"Lakini pia Katibu atoe taarifa kama tatizo la FIBUCA ni kubwa ili tukusaidie," inasema barua hiyo na kuongeza, "Maagizo yote yaliyomo ndani ya waraka huu yatekelezwe bila kukosa ili uweze kuhudhuria kikao hicho."

Aidha, TUICO imetajwa kutumia wakili Sylvester Shayo kumwandikia barua Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri Tanzania kueleza mapungufu ya FIBUCA ili kisajiliwe.

FIBUKA ilianza kutafuta usajili tangu Machi mwaka huu.

0
No votes yet