FIFA: Makocha wa kigeni waliiangusha Afrika


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version

KATIKA fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini mwaka huu, Kocha mkuu wa Ghana, Milovan Rajevac alijizuia kushangilia bao ilipotoka sare ya bao 1-1 na Serbia kwenye hatua ya makundi.

Rajevac aliyechukua nafasi ya Rantomir Antic ambaye anainoa Serbia, aliweka mbele uzalendo kwa nchi yake kuliko kibarua chake.

Ivory Coast ilifanya vituko. Ikiwa imesalia miezi michache, ilipitia majina kadhaa na ikafikia uamuzi wa kumteua Sven-Goran Eriksson kuwa kocha mkuu wake. Sababu kuu iliyoangaliwa si uwezo wake bali kigezo cha mshahara mkubwa kuliko wachezaji kama kina Didier Drogba.

Nigeria, pamoja na kwamba kocha mzalendo Shaibu Amodu ndiye aliiwezesha Super Eagles kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (2010) nchini Angola na kufuzu kwenda Afrika Kusini, aliondolewa na nafasi yake akapewa Lars Lagerback wa Sweden.

Kati ya timu zote sita za Afrika zilizoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka huu ni Algeria peke yake iliyomwamini mzalendo Rabah Saadane.

Rekodi zilizopo zinaonyesha kwamba pamoja na imani ya viongozi wa soka kwa makocha wa kigeni, kuna ushahidi uliowazi kwamba makocha wa kizalendo wamezipa timu mafanikio makubwa kuliko wa kigeni.

Hata Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) katika ripoti yake ya fainali za Kombe la Dunia imeipongeza Hispania kwa kutwaa kombe hilo, lakini imesema kuwa nchi za Afrika zilipoteza fursa ya kufanya vizuri kwa kuajiri makocha wa kigeni.

Ripoti hiyo iliwashutumu pia makipa kwa kufanya “makosa yasiyoelezeka”—labda kutokana na mpira wa Jabulani ball — lakini ikatupia lawama kwa makosa ya uamuzi yaliyochangia baadhi ya timu kuondolewa mapema.

Ripoti hiyo iliyotolewa Alhamisi iliyopita imehoji pia kama kweli wachezaji wengi walikuwa wachovu baada ya misimu mirefu kabla ya fainali hizo zilizofanyika kwa mara ya kwanza katika ardhi ya Afrika.

Katika fainali hizo, Hispania ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uholanzi iliyolalamikiwa kwa mchezo wa vurugu.

FIFA ilikusanya jopo la makocha wazoefu na wachezaji wa zamani kufanya tathmini ya mechi 64 kuhusu mbinu na uchezaji kabla ya kuchapa ripoti yenye kurasa 289.

Ripoti hiyo ilimalizika kwa kusema Hispania ilicheza “mchezo wa hali ya juu na kuvutia”, alisema mkurugenzi wa ufundi na mafunzo wa FIFA, Jean-Paul Brigger.

“Ni timu iliyokamilika, na kusema kweli ni washindani wa timu bora ya karne,” alisema Brigger katika mtandao. “Xavi, Iniesta na Xabi Alonso katika kiungo walitawala kwa kiasi kikubwa lakini walicheza soka ya kuvutia pia.”

Washauri wa FIFA walitoa maoni ya julwa kwamba, timu nyingi ikiwemo Afrika Kusini, zilishindwa kutokana na kuwa na matarajio makubwa kupita kiasi.

Kisha wakaeleza kwa nini timu zote zita za Afrika—tano zikiwa na makocha wa kigeni—zilifanya vibaya na ikaisifu Ghana kwa kufika robo fainali.

“Nafasi ya mafanikio kwa makocha hao ilikuwa finyu kwa vile baadhi yao hawakujitambulisha na utamaduni wa Kiafrika kiakili na staili ya maisha au walikuwa na uelewa mdogo kuhusu masuala hayo,” ilisema ripoti hiyo.

Tatizo jingine kwa timu kama vile Cameroon, Nigeria na Algeria zilikabiliwa na “wakati mgumu kifikra” kushiriki fainali za Kombe la Dunia miezi mitano tu baada ya michuano mikubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola.

“Tatizo linakuwa katika kuwaweka wachezaji wakiwa na hamasa na tayari kwa mashindano hayo mawili makubwa,” ilisema ripoti hiyo ya FIFA.

Wenyeji wa fainali hizo Afrika Kusini walimwajiri Carlos Alberto Parreira kutoka Brazil, Cameroon walimchukua Paul Le Guen wa Ufaransa; Nigeria ikampa kazi Lagerback wa Sweden. Eriksson, mbali ya kuwa na mshahara mkubwa, alikuwa anaishi London, Uingereza hivyo alikuwa kiguu na njia.

Algeria peke yake ndiyo ilimwamini mzalendo Rabah Saadane.

Ripoti hiyo inaweza kutumika kama angalizo kwa timu na viongozi wa Afrika ambao kila wanaposaka kocha wa timu ya taifa, huangazia machoa yao Ulaya wakati kuna makocha wazalendo.

Wazalendo wana uchungu, uwezo mkubwa wakipewa kila aina ya msaada, huduma, mshahara mzuri, nyumba na vifaa kama wanavyofanyiwa makocha wa kigeni.

Tanzania haijakwepa ugonjwa wa kupenda makocha wa kigeni. Agosti 2006 ilimwajiri Marcio Maximo kwa ajili ya kuiwezesha Taifa Stars kufuzu na kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2008 na 2010 na fainali za Kombe la Dunia 2010. Lakini hakufanikiwa.

Nafasi yake imechukuliwa na Jan Borge Poulsen kutoka Denmark na ameanza kwa kuiwezesha Taifa Stars kutoka sare ya 1-1 na Algeria katika safari ya kufuzu kwa fainali za mwaka 2012.

Taifa Stars itaikaribisha Algeria kabla ya kumenyana na Morocco halafu Afrika Kati. Je, sare hiyo ni mwanzo mwema kwa Taifa Stars au Poulsen atakuja kuangukia katika mkumbo wa makocha wa kigeni kushindwa kusoma utamaduni wa nchi?

0
No votes yet