Fikra sahihi ni kuondoa CCM


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
HAPO zamani za mfumo wa chama kimoja, Watanzania walielekezwa kuamini kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiye pekee mwenye fikra sahihi.

Baada ya kusalimia “Kidumu Chama Cha Mapinduzi” na kujibiwa “Kidumuuu,” ilifuata salamu nyingine: “Zidumu fikra sahihi za Mwenyekiti wa CCM;” na wananchi walijibu, “Zidumuuu”.

Salamu hiyo ya utii ilikufa kwani ilikuja kubainika kuwa si kila fikra ya mwenyekiti ni sahihi. Lakini sasa wanatumia kiitikio cha ‘Ndiyo Mzee’ kama ilivyo katika wimbo uliotungwa na msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Prof. Jay.

Wakiambiwa jambo lolote lile ambalo hata kwa akili zao hawasadiki wanaitikia “Ndiyo Mzee”. Hawawezi kusema “Siyo Mzee”, maana hizo ni fikra sahihi za mwenyekiti wa CCM.

Mwenyekiti: Wakazi wa Nansio nitawajengea daraja mpaka Musoma; siyo daraja nitanunua kivuko, na Bukoba msiwe na shaka nitanunua meli kubwa kuliko ya mv Bukoba.

CCM: Ndiyo Mzee.

Mwenyekiti: Nitajenga viwanja vya ndege vya kimataifa Misenyi, Kigoma na kwingineko.

CCM: Ndiyo Mzee.

Mwenyekiti: Nitajenga barabara za lami kutoka Njombe hadi Makete, watu hawatapita kwenye barabara za vumbi tena. Korogwe-Bumbuli nitatandika lami.

CCM: Ndiyo Mzee.

Mwenyekiti: Serikali yangu itasaidia vyama vyote vya ushirika; madeni yaliyosababishwa na mchwa Shirecu yatalipwa haraka.

CCM: Ndiyo Mzee.

Mwenyekiti: Nilitaka kusahau, nitageuza mji wa Tanga kuwa mji wa viwanda, Kigamboni itakuwa Satellite Town, wakazi wa Tabora watapata maji kutoka Ziwa Viktoria na Kigoma itakuwa Dubai nyingine.

CCM: Ndiyo Mzee.

Mwenyekiti: Nasema mkinichagua kila mgonjwa atakuwa na bajaji yake; ‘sorry’ kila zahanati itakuwa na bajaji; kila mkoa utakuwa na hospitali ya rufaa.

CCM: Ndiyo Mzee.

Ukiangalia ahadi hizi, unajiuliza haraka, ziko wapi nyumba 10,000 za walimu na kiko wapi kiwanda cha matunda Lushoto – mambo mawili tu kati ya maelfu ya ahadi za mwaka 2005?

Mgombea urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete, ameendelea kumwaga ahadi juu ya ahadi; nao wana-CCM wameendelea kushangilia bila kujua athari zake.

Miongoni mwa wanaolipuka kwa kushangilia ni wale wanaolalamika pembeni kuwa hawajaona “maisha bora” waliyoahidiwa mwaka 2005.

Miongoni mwao pia ni wale wasio na uwezo wa kununua elimu na huduma za afya ambavyo vinapatikana kwa “gharama ya kuchangia.” 

Wananchi wamelelewa na kukulia kwenye mfumo wa kuimba, “Zidumu fikra sahihi za Mwenyekiti wa CCM.” Fikra zipi?

 Hivi ni fikra sahihi kuahidi viwanja vya ndege nchi nzima, kama hizo ni kero, wakati hakuna fedha za kumalizia kile cha Songwe, Mbeya?

Kweli fikra sahihi zinaweza kuwa mwenyekiti kukumbatia watuhumiwa wa ufisadi badala ya kupambana na ufisadi?

Nani atakubali kuwa ni fikra sahihi kwa mwenyekiti kuahidi kujenga nyumba za waathirika wa mafuriko Kilosa wakati ahadi hiyo ilitolewa na Libya?

Kikwete alitishia wafanyakazi na kuapa kutoongeza hata senti kwenye mishahara yao. Baada ya mambo kumwendea ovyo katika kampeni, ameahidi neema? Hivi maisha bora ni hisani?

Ni Abdulrahman Mohammed Babu aliyeandika blabu nyuma ya kitabu How Europe Underdeveloped Africa cha Dk. Walter Rodney.

Alisema, “Msikae mkidhani kwamba lile zimwi lililowatesa kwa miaka mingi litabadilika na kuwa mwana mbuzi…kama wa mwisho atakuwa wa kwanza basi hiyo itakuwa baada ya mapambano ya haki….”

CCM ni zimwi lililowatesa Watanzania kwa nusu karne; fikra sahihi ni kuliondoa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: