Filamu mpya ya Rostam Aziz


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

TUKIO la kujiuzulu nyadhifa zake zote Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz linafanana sana na alichofanya aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Kilombero, Abbas Gulamali.

Mwaka 2000 akihisi kwamba anakabiliwa na upinzani mkali katika hatua ya mchujo, Gulamali alifanya usanii kupima upepo kama bado alikuwa anakubalika ndani ya CCM.

Aliwakusanya waandishi wa habari akatangaza kwamba hatawania tena ubunge katika jimbo hilo. Alitoa sababu mbili; kwanza eti anataka watu wengine wajitokeze, na pili anataka kuendelea kushughulikia biashara zake.

Siku ya pili yake walijitokeza watu walioitwa wazee wa wilaya ya Kilombero wakamtaka abadili uamuzi wake. Siku nne baadaye, Gulamali alidai amesikia na kupima uzito wa ushauri wa wazee hivyo ameamua kubadili msimamo wake.

Hivi ndivyo alivyofanya Rostam. Alikusanya waandishi wa habari Dar es Salaam, akawapeleka Igunga kwa ‘pipa’ ili waripoti tukio la yeye kutangaza kujivua gamba.

Rostam alifanya mambo kisasa; alikusanya hata vijana wa kulia na kusaga meno eti wakisikitika mbunge wao kutangaza kuaachia nyadhifa zake zote alizopata kupitia CCM – ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na ubunge.

Waandishi wakaandika na vijana waliokodishwa rasmi walinyanyua mabango kuonyesha msimamo wao kwake na wengine wakapiga mayowe kulia hadi wakazirai na macho yao yakatoa mvua kujaza vidimbwi vya mashavu yao.

Halafu mzee wa busara akanyakua kipaza sauti na kutoa ushauri mzito kwamba abadili uamuzi wake. Rostam akapanda gari lake na kuondoka. Gulamali alikuwa mjanja, hakutoa nafasi watu kumjadili, akabadili uamuzi haraka. Rostam amechelewa, imekula kwake.

Nikiri mapema kwamba sijawahi kutembelea wilaya ya Igunga, lakini kwa kutazama makundi ya wananchi wanavyohangika kutafuta maji na aina ya nyumba maeneo ya barabarani ninapopita nikienda mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Kigoma na Mara, naamini tukio la watu kulia lilipangwa.

Maswali Rostam ni kati ya wabunge ambao hawajawahi kuuliza maswali ya msingi wala ya nyongeza katika kipindi chake chote cha ubunge wake.

Vilevile, mbunge huyo hajawahi kuchangia hoja yoyote kwa kuzungumza wala maandishi. Maandishi pekee yaliyoko kwenye kumbukumbu za Bunge ni alipojitetea ili kujinasua katika sakata la Richmond, si vinginevyo.

Hapa ndipo najiuliza, wananchi waliokuwa wanalia hadi kuzirai amewasaidia vipi, mbona hata barabara ni shida?

Waliolia na kuzirai ni wale wananchi maskini, ambao wanahangaika kila siku kuchota maji upande huu wa malambo huku upande ule mifugo (mbuzi, kondoo, ng’ombe na punda) ikinywa maji hayohayo na kuchafua?

Waliokuwa wanalia hadi kuzirai ni wale ambao asilimia kubwa nyumba zao bado ni ‘fulusuti’ yaani zimejengwa kwa matope na kuezekwa kwa matope (tembe)? Je, ni wale ambao nyaya za umeme wa gridi ya taifa zimepita juu ya nyumba zao lakini nyumba zao hazina umeme?

Waliokuwa wanalia ni wale waliokumbwa na njaa kiasi kwamba serikali inapaswa kuwapa chakula cha msaada ili kuwanusuru mwaka huu? Je, ni wale wanaokaa kwa makundi wanaotembea na mifugo umbali mrefu kwa ajili ya usaka malisho na maji?

Je, ni wananchi wanaonunua mafuta ya taa yaliyofikia Sh. 2200 kwa lita katika vituo vingi katika wilaya za Igunga, Kahama, Kibondo na Kasulu? Huu si usanii tu bali ni unafiki.

Kama hii ndiyo hali halisi, waliolia ni wanafiki na tukio zima liliandaliwa kinafiki. Je, Rostam alikuwa anaandaa filamu inayofanana na One Down Two To Go ya msanii maarufu Mmarekani mweusi Jimmy Brown?

Rostam ameanguka, bado wawili; Mzee wa Vijisenti na Mzee wa Richmond. Watamfuata au ametolewa kafara kama waasisi wa CCJ walivyomtosa Mhandisi Fred Mpendazoe? Mzee wa Vijisenti na Mzee wa Richmond wasipojiuzulu Rostam atakuwa ameigiza filamu mpya ya One Down Two To Go.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: