Finias Magessa: Mhandisi anayewania ubunge Busanda


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 28 April 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana
Finias Bryceson Magessa

SI muda mrefu jina jipya litaingia katika historia ya uongozi wa siasa nchini. Ni Finias Bryceson Magessa. Anagombea ubunge wilayani Geita, mkoani Mwanza.

Magessa (38) ni mgombea ubunge Jimbo la Busanda. Anatoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Anasema haraka kuwa hakujitosa kupima upepo, bali kushinda ubunge na kuwakilisha wananchi wa Busanda. Hiyo ni katika mahojiano na MwanaHALISI wiki hii.

“Wananchi wa Busanda wana matatizo mengi. Wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, umeme, shule, zahanati na mengine mengi,” anasema na kuongeza kuwa anataka kukaa nao kama mwakilishi wao na kutafuta ufumbuzi.

Kwa mujibu wa Magessa wananchi wa Busanda wanaweza kupata umeme wa uhakika na kwa haraka kama kipaumbele kitawekwa katika uzalishaji wa umeme kupitia nguvu za jua, upepo na mito midogo iliyopo jimboni humo.

Uchaguzi mdogo katika jimbo la Buchosa unafuatia kifo cha mbunge Faustine Kabuzi Rwilomba (CCM). Alifariki karibu miezi miwili iliyopita.

Je, amesukumwa na nini kujitosa katika kinyang’anyiro hicho? Magessa anajibu, “Kuna mengi. Moja, mimi nimezaliwa kijijini na kila mwaka nakwenda kijijini. Nafahamu maisha ya huko kuwa bado ni magumu mno.”

Anasema, “Kunahitajika kitu kifanyike. Bado ninaamini kama alivyosema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, urithi wa elimu ni muhimu. Ninapoiangalia Busanda ninaona matatizo mengi yanatokana na uduni wa elimu inayotolewa.

“Nimejitosa ili kusaidia na wananchi. Tuna wajibu wa kushirikiana na wananchi kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo. Busanda kuna rasilimali nyingi, lakini bado hazijatumiwa,” anasema.

Anasema, “Sioni ni kwanini tusijenge mabweni katika kila sekondari ya kata ili kudhibiti mimba kwa wanafunzi. Hilo lipo ndani ya uwezo wetu.”

Magessa anasema mbunge anaweza kuuhakikisha mabati yanapatikana na wananchi wakachangia nguvu kwa kufyatua matofali.

“Kuna kata 13. Katika kipindi cha mwaka mmoja ninaweza kuhakikisha mabweni yamejengwa katika nusu ya shule zote hizi,” anajadili kwa njia ya kuonyesha uwezo na kutoa ahadi.

Kwenye shughuli za kiuchumi, Magessa anasema anaweza kutumia utalaam wake kuibua miradi ya kufuga na kukausha samaki na dagaa badala ya wananchi wengi kutegemea kilimo cha pamba ambayo imeshuka bei.

“Mimi ninataka platform (jukwaa) ya kuhudumia wananchi. Nilijenga hosteli katika Shule ya Sekondari ya Nyakagomba watu wakasema ninataka ubunge. Kila ninachofanya kinaingizwa kwenye siasa,” anaeleza huku akitabasamu.

“Eh, kumbe huwezo kusaidia maendeleo ya wananachi wenzako mpaka uwe mbunge? Basi sasa ninautaka ubunge ili iwe platform yangu ya kuhudumia wananchi.

Anasema yeye ni mtaalam pia wa kuandika miradi ya asasi zisizokuwa za kiserikali (NGO’s). Uzoefu huu. anasema utasaidia kupata kompyuta na misaada mingine kwa ajili ya shule.

“Nina mengi ya kufanya. Ni wakati sasa nirudi nyumbani Busanda kutoa mchango wangu katika eneo hili. Magessa amekuwa akiishi Dar es Salaam na kufanya kazi katika shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Solar Energy Association (TASEA).

“Sitakuwa mbunge wa kundi fulani la kisiasa. Ninawaomba wana Busanda waache propaganda mbaya za kisiasa. Tutumie raslimali zilizopo kama vile ardhi na maji ili kuleta maendeleo,” ameahidi mapema.

Amesema kuna haja ya kuzingatia raslimali na vipaji “tulivyopewa na Mungu ili kujenga uchumi. Kama alivyosema Barack Obama, ‘Inawezekana.’ ”

Magessa anasema ana deni kwa wananchi wa Busanda kwa kuwa wakati akisoma shule wananchi walikuwa wakikatwa fedha za mauzo ya pamba ili kuendesha shule. “Ni wakati wao sasa kunidai. Wawe tayari tushirikiane. Nimejiandaa na inawezekana.”

Akiongea kwa kujiamini, Magessa anasema, “Mimi napenda kuona matokeo ya kile ninachokifanya. Wakati ninapofunga mitambo ninapenda kuona inafanya kazi. Hivyo ndivyo nitakavyofanya kazi za ubunge.”

Finias Bryceson Magessa alizaliwa 7 Mei 1971 katika kijiji cha Nyakagomba, Kata ya Nyakagomba, Tarafa ya Butundwe, wilayani Geita, mkoani Mwanza.

Alianza masomo ya msingi mwaka 1978 katika Shule ya Msingi Nyakagomba. Alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Geita (1985-1988) na akaendelea na kidato cha tano hadi sita katika Shule ya Sekondari Tosamaganga ya mkoani Iringa na alikohitimu mwaka 1991.

Kutokana na kuwapo kwa utaratibu wa kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria wakati huo, Magessa alijiunga na mafunzo hayo Kambi ya JKT ya Mlale, Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma mwaka 1991 hadi 1992.

Baada ya hapo alijiunga na masomo ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea kozi ya uhandisi wa mitambo ngazi ya shahada ya kwanza kuanzia mwaka 1993. Alihitimu mwaka 1997.

Magessa alianza kazi katika shirika lisilo la kiserikali la TATEDO (Tanzania Traditional Energy Development and Environmental Organisation) mwaka 1997. Aliondoka mwaka 2000 ili kuongeza ujuzi.

Alikwenda nchini Ujerumani kusomea shahada ya uzamili ya Nishati Jadidifu - (Master of Science in Renewable Energy) katika Chuo Kikuu cha Oldenburg kilichomo nchini humo.

Mwaka 2001 alirejea kufanya kazi yake TATEDO hadi mwaka 2006 alipohamia TASEA ambako amekuwa akifanya kazi hadi sasa.

Magessa anasema alipojiunga na elimu ya sekondari hakuwa mpenzi wa uongozi, lakini alikuwa mstari wa mbele katika harakati nyingine za ujenzi wa taifa.

“Nilipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilikuwa mbele kudai haki za wanafunzi. Nilifanya hivyo na wenzangu kwa njia ya maandamano mbalimbali.

Magessa anasema amekuwa mwanaharakati wa mageuzi, na juhudi zake zilijitokeza wazi wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

“Tulikuwa na kazi ya kulinda kura za wagombea upande wa upinzani. Tulijitahidi kuhamasisha watu ingawa uchaguzi wa mwaka huo katika Mkoa wa Dar es Salaam ulifutwa. Ninashawishika kusema kuwa upinzani ulikuwa umeshinda viti vingi Dar es Salaam,” anasema Magessa.

Magessa, ambaye ni mtoto wa 10 kati ya 11 wa familia yao, ana mke na watoto watatu. Alijiunga na CHADEMA tarehe 6 Mei 2005.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: