Funzo la uokoaji kutoka Chile


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MIAKA 14 iliyopita, takribani wachimbaji madini 50 inadaiwa walifukiwa wakiwa hai katika Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu nchini Tanzania. Lengo lilikuwa kupisha wawekezaji wakubwa wapate eneo la kuchimba.

Hadi leo, hakuna anayejua watu wangapi walikuwapo katika machimbo hayo wakati tukio hilo likitokea. Ni familia chache tu za watu zilijitokeza kudai ndugu zao walikuwamo ndani ya mashimo ya dhahabu wakati serikali ikifukia mgodi kwa magreda.

Endapo ilitokea kweli, maana serikali ilikanusha, basi ule ulikuwa unyama maana badala ya kuokoa uhai—nguvu kazi ya taifa, inafukiwa.

Chile, nchi iliyoko mbali kabisa bara la Amerika Kusini imeonyesha tofauti na imetoa somo. Rais wa nchi hiyo, Sebastien Pinera, aliweka kambi katika machimbo ya San Jose, kuongoza juhudi za uokoaji wa wachimbaji 33 waliokuwa wamebanwa ndani ya mgodi kwa siku 69.

Lakini si Rais Pinera pekee aliyekuwapo katika mgodi huo kuongoza juhudi hizo. Walikuwapo madaktari wa magonjwa ya binadamu, wanasaikolojia, wapishi, wajenzi, vifaa vya uokoaji na kila kilichohitajika.

Niliwafikiria sana wale waliopoteza ndugu zao katika machimbo ya Bulyanhulu mara baada ya kuona tukio la Chile. Wangejisikiaje iwapo serikali yao ingefanya vile ilivyofanya serikali ya Pinera?

Rais Pinera ametoa somo kubwa kwa viongozi wa serikali ya Tanzania.

Wakati wa tukio la kubomoka kwa jengo la iliyokuwa Hoteli ya Chang’ombe Village jijini Dar es Salaam mwaka 2006, viongozi wa serikali walifika katika eneo la tukio bila ya waokoaji wala vifaa vya uokoaji.

Pinera alifika katika mgodi huo ulioko katika jangwa la Atacama, baada ya kuwa tayari waokoaji na huduma zote zilizohitajika kuwa zimefika. Hali huwa tofauti hapa nchini. Viongozi hupenda kuonekana ‘wakiuza sura’ kabla hata waokoaji na vifaa hawajafika.

Kama serikali ya Chile ilikuwa tayari kufanya lolote kwa ajili ya watu 33 waliokuwa wamefukiwa, ni kwa vipi serikali ya Tanzania ilishindwa kuhakikisha kila mtu ametoka machimboni kabla ya kufukiwa katika mgodi wa Bulyanhulu?

Kwa vyovyote vile, kazi kubwa na ya kwanza ya serikali yoyote ni kuhakikisha usalama wa raia wake. Ndiyo maana serikali zote huhakikisha vyombo vyake vya usalama vinawalinda raia wake kwa hali yoyote ile.

Tanzania ilipoingia vitani dhidi ya Iddi Amin Dada mwaka 1978, ilikuwa kwa sababu dikteta huyo wa Uganda alikuwa amehatarisha maisha ya Watanzania waliokuwa wakiishi Kagera.

Hasara ambayo Tanzania iliingia baada ya vita hivyo ni kubwa. Lakini, hakuna serikali ambayo inaweza kuruhusu raia wake waonewe, waporwe na kuuawa na bado ikaendelea kujiita serikali. Serikali ipo kwa ajili ya kulinda watu.

Ilikuwaje basi serikali ikafanya kile inachodaiwa kufanya kule Bulyanhulu? Vipi kuhusu maisha ya wananchi wale maskini ambao serikali ilipaswa kuangalia usalama na uhai wao lakini ikawatosa?

Nilipokuwa natazama televisheni wakati wachimbaji wale wa Chile wakitoka shimoni, kuna kipindi nilitokwa na machozi na mwili kunisisimka.

Hii ni kwa sababu wale waliookolewa walitoka, baadhi yao, wakiwa na bendera za taifa za nchi zao. Kuokolewa kwao kuliwafanya wajisikie fahari kuwa raia wa Chile.

Je, kama wale waliokuwa Bulyanhulu wangeokolewa, si wangekuwa wazalendo waadilifu kwa taifa lao? Si wangeipenda nchi na serikali yao? Si wangekuwa na furaha?

Furaha ni jambo kubwa katika maendeleo ya nchi yoyote hapa ulimwengni. Watafiti duniani hutumia kitu kinachoitwa ‘Happyness Index Factor’ (Kipimo cha Furaha katika Nchi, tafsiri ni yangu), kuangalia utajiri wa nchi husika.

Mara zote, nchi ambazo watu wake huishi kwa furaha, ndizo ambazo zimejikuta zikiendelea zaidi. Kwamba wananchi wanapokuwa na furaha, wanazalisha zaidi, wanajituma zaidi na hawaumwi mara kwa mara na hivyo wanakuwa wafanisi.

Wananchi wanapoona ya kuwa serikali yao inawajali na iko tayari kufanya kila iwezalo kuhakikisha wanaishi vizuri, nao wataweza kufanya lolote kwa ajili ya nchi yao.

Hebu tujiulize swali moja hapa la kawaida kabisa, hivi leo Rais Pinera akiomba lolote kutoka kwa wananchi wa Chile, kuna atakayemgomea? Atamgomea vipi wakati anajua kiongozi anafanya kila kitu kwa maslahi ya taifa?

Tukio la Chile, zaidi ya mambo mengine, linafundisha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwa watu wengi zaidi wamewahi kufukiwa katika migodi wakati zinapotokea ajali.

Katika miaka mitatu au minne iliyopita, kumetokea ajali kubwa katika migodi ya madini ya Tanzanite kule Mirelani, Manyara. Idadi ya waliokufa inayojulikana ni ile ya miili iliyookotwa na si zaidi ya hapo.

Sik 17 baada ya tukio la Chile, wananchi waliambiwa wazi kabisa kwamba kuna wachimbaji 33 walioko hai chini ya ardhi. Katika siku 17 za awali, hakuna aliyejua iwapo wamekufa au wako hai.

Maafa kama haya yanapotokea Tanzania, utasikia baada ya siku nane au kumi kwamba watu wote wamekwisha kuokolewa na hakuna aliyebaki ndani. Hata hivyo, huwa hatuambiwi wangapi walikuwa ndani ya migodi kabla maafa hayajatokea.

Miaka 14 baada ya Bulyanhulu, serikali bado inapinga kuwa hakuna mtu aliyefukiwa kwenye mashimo hayo. Hata hivyo, wapo wananchi waliojitokeza hadharani na kusema ndugu zao walifukiwa.

Ingekuwa muhimu kwa serikali kuunda tume huru ya uchunguzi na kubaini nini hasa kilitokea Bulyanhulu. Kama kuna watu ambao waliathiriwa na tukio hilo basi watambulike na walipwe fidia zao.

Hiyo ndiyo itakuwa njia nzuri zaidi ya kupata ufumbuzi wa kile kilichotokea Bulyanhul. Wakati wenzetu Chile wakishangilia kile serikali yao ilichofanya kwa wananchi wake; Watanzania nao wanasubiri hatua za serikali yao.

Na wana kila sababu ya kufanya hivyo. Labda kama wao si walioiweka madarakani.

0
No votes yet