Furaha ya Rostam kuzimwa?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version
Rostam Aziz

SHIRIKA la umeme la taifa (TANESCO) limetupa kete muhimu likilenga kusimamisha ulipaji tozo ya Sh. 94 bilioni kwa mbunge wa Igunga na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC-CCM), Rostam Aziz kupitia kampuni ya Dowans Holdings SA, MwanaHALISI limeelezwa.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili limezipata, TANESCO wamewasilisha mahakama kuu mjini Dar es Salaam, hoja sita kupinga hukumu iliyotolewa na mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya biashara (ICC) iliyoipa Dowans tozo ya mabilioni hayo ya shilingi.

Katika maelezo yake ambayo gazeti hili limeyaona, TANESCO kupitia jopo la mawakili wanaoongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, inataka mahakama hiyo itengue tozo hiyo kwa kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni za uadilifu na ukweli.

Wanasheria wa TANESCO wanasema, “Jopo la wasuluhishi lilijipa mamlaka isivyo halali au lilitumia vibaya mamlaka yake, kwa kutumia sheria ya Texas nchini Marekani kuonyesha uhalali wa kuwepo kwa Richmond.”

Jopo la mawakili wa TANESCO linaundwa na Masaju (kiongozi), Prof. Florence Lwoga, Dk. Angelo Mapunda, Dk. Alex Nguluma na wakili Mwandambo.

Mawakili hao wanaeleza kwamba majaji wa ICC walitafsiri kinyume cha haki, sheria ya manunuzi ya umma ya Tanzania (PPRA) ya mwaka 2004 inayoelekeza kuwa mlipaji wa huduma ndiye anayepaswa kushiriki katika vikao vya majadiliano kabla ya zabuni kutolewa.

Wanadai kwamba wasuluhishi walipuuza, kwa makusudi, ushahidi wa TANESCO kuwa ilikuwa ni kinyume cha sheria ya PPRA kuidhinisha kusainiwa kwa mkataba bila kwanza kufuatwa utaratibu wa kutangazwa zabuni ya kukaribisha waombaji; hasa kwa kuwa zabuni ya awali ilifutwa na bodi ya zabuni ya TANESCO.

TANESCO wanadai kuwa Wizara ya Nishati na Madini au Kamati ya Majadiliano iliyoundwa na serikali, haikuwa na uwezo wowote wa kisheria kuidhinisha mkataba kati yake na Richmond na baadaye Dowans.

Gazeti hili linaweza kuthibitisha kuwa kamati ya majadiliano ya serikali ambayo ndiyo iliyosimamia mkataba unaobishaniwa mahakamani, iliundwa kwa shinikizo la waziri mkuu aliyejiuzulu mwaka 2008 kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa.

Mawakili wa TANESCO wanajenga hoja katika kupinga uamuzi wa ICC kuwa mahakama hiyo ilikosea kisheria kwa kutozingatia nyaraka kadhaa likiwamo tangazo la zabuni Na. PC010/2006, jambo ambalo limesababisha kufikiwa kwa makubaliano yaliyokiuka vigezo vilivyobainishwa katika zabuni hiyo. 

Vilevile, mawakili wanaeleza kwamba haikuwa sahihi mrufani (TANESCO) kulazimishwa kusaini makubaliano na Richmond Development Company (LLC) yaliyojadiliwa na kampuni ya Texas ambayo haikuwa na uzoefu wa kutekeleza mradi wala uwezo kifedha.

Mawakili wanadai msimamo huo wa TANESCO unazingatia ukweli kwamba katika zabuni iliyotangazwa na baadaye kufutwa, ilielekezwa kwamba kabla ya kufikiwa kwa makubaliano ya kuidhinisha mkataba, sharti mambo kadhaa yazingatiwe.

Mambo ambayo walitaka yazingatiwe ni ufungaji wa mitambo na muda kuanza kwa utoaji wa huduma, muda wenyewe wa kutolewa huduma, gharama za awali, malipo ya ushuru wa forodha na kodi nyinginezo, malipo ya uendeshaji badala ya kutumia gesi iliyopo.

TANESCO inadai wasuluhishi walikosea walipotafsiri vibaya sheria ya manunuzi ya umma na kushindwa kuona kwamba mrufani hakuwahi kutoa zabuni yoyote kwa Richmond Development Company (LLC) ambayo ndiyo ilisababisha kuingia kwa kampuni ya Dowans katika makubaliano.

TANESCO wanadai pia kuwa wasuluhishi walijihusisha na ukiukwaji wa utaratibu kwa kushindwa kutafsiri sheria ya manunuzi juu ya katazo la kununua mitambo ya mitumba.

“Matokeo yake, wasuluhishi walishindwa kuamua kwamba zabuni kwa Richmond (kama ilikuwepo) ilipatikana kinyume cha sheria za kimataifa zinazoelezea hoja ya kuzingatiwa kanuni za zabuni za huduma zinazohusu suala linalogusa usalama wa nchi.”

TANESCO inadai kwamba wasuluhishi walipuuza ushahidi uliotolewa na mrufani kuhusu uwezo wa mkataba na kule kutotambua kwao sheria ya kutumika katika usuluhishi juu ya uhalali na kuwepo kwa Richmond Development Company (LLC).

Mawakili wa TANESCO wanadai kuwa wasuluhishi walidharau ushahidi uliotolewa kuonyesha namna mrufani alivyojengewa mazingira ya nguvu ili tu asaini makubaliano na matokeo yake kulazimisha mrufani “kufikia makubaliano” na mrufaniwa.

TANESCO inadai kwamba kwa kutozingatia ushahidi wa kutoshiriki kwa kampuni hiyo katika majadiliano, wasuluhishi wameonyesha upendeleo wa dhahiri na kuchukulia ukosefu huo kuwa ni sababu muhimu ya kutohusika kufikiwa kwa makubaliano.

Aidha, wasuluhishi walishindwa kutambua ushahidi wa mrufani kwamba saini kwenye nyaraka zinazohusu utoaji zabuni, kuidhinisha kutolewa kwa huduma na kuhamisha mkataba kulikofanywa 14 Oktoba 2006, zinatofautiana na saini zilizopo kwenye mkataba.

Mrufani anasimama katika hoja kwamba utolewaji wa tozo umefanywa kwa makosa kisheria; makosa yanayotokana na kupuuza kumbukumbu na kwamba wasuluhishi walikosea kisheria waliposhindwa kutambua ushahidi mzuri dhidi ya utolewaji wa mkataba wa kutoa huduma.

Kwa hoja hizo basi, mawakili wa TANESCO wanasisitiza, “Tunataka tozo ibatilishwe na shauri lirudishwe kwa wasuluhishi kwa ajili ya kufikiriwa upya.”

Mbali na TANESCO, wengine waliotinga mahakamani kupinga tozo hilo, ni Kituo cha Huduma za Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na wenzake wawili, akiwamo mwandishi wa habari, Timothy Alvin Kahoho.

LHRC inawakilishwa mahakamani na Dk. Sengondo Mvungi wa Chuo Kikuu cha Dar ese Salaam wakati Kahoho anajiwakilisha mwenyewe.

Kesi iliyotajwa mara ya kwanza 2 Machi, inatarajiwa kutajwa JUmatano ya 30 Machi 2011, mbele ya Jaji Emilia Mushi.

Dowans iliyorithi mkataba wa kufua umeme kutoka kwa Richmond, imepata tozo hiyo baada ya kuonekana kuwa TANESCO ilivunja mkataba nao. Dowans wamesajili hukumu hiyo kufuata utaratibu wa kutaka kukazwa kwa hukumu hiyo.

0
Your rating: None Average: 4.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: