Fursa pekee kwa Yanga kuandika ukurasa mpya


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 23 June 2010

Printer-friendly version

HUU ni wakati wa wanachama wa klabu ya Yanga, Dar es Salaam kuandika ukurasa mpya baada ya mkutano uliomalizika kwa ‘kuufurusha’ uongozi wa Mwenyekiti, Imani Madega.

Kamati ya uchaguzi wa klabu ya Yanga ilikutana Jumapili iliyopita, pamoja na mambo mengine kuhakiki majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu hiyo uliopangwa kufanyika Julai, 18, mwaka huu.

Halafu, kamati hiyo inayoongozwa na Jaji John Joseph Mkwawa ikawapa fursa wanachama, kuanzia jana Jumanne, kuweka pingamizi dhidi ya mgombea wa nafasi yoyote ambaye ataonekana hajakidhi vigezo vya kugombea.

Kamati imetoa muda mpaka Juni 26, mwaka huu kwa wanachama ‘kuchinjana’ na siku inayofuata yaani Juni 27, kamati itapitia pingamizi zilizowekwa.

Ratiba ya uchaguzi huo inaonyesha wagombea watakaokuwa hawana matatizo wataitwa kwenye usaili Juni 28, mwaka huu na siku inayofuata kamati itatangaza matokeo ya usaili kabla ya kuanza kampeni.

Julai 2 kamati hiyo itapokea rufaa kutoka kwa wagombea waliowekewa pingamizi kabla ya Julai 6, kutangaza majina ya mwisho ya wagombea watakoingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.

Ingawa ratiba imepangwa hivyo, ukweli wagombea wa nafasi mbalimbali wanapita huku na kule kuona kama wanaungwa mkono au la.

Wagombea, wengi wao ni watu wenye heshima zao, wenye kazi zao na baadhi yao wamewahi kutoa na wanaendelea kutoa mchango wa hali na mali kwa ajili ya maslahi ya klabu.

Baadhi ya wagombea hao wamelazimika kuchukua fomu baada ya kushawishiwa na wanachama hao baada ya kuona wanafaa ilhali wengine wamefanya hivyo kwa utashi wao wenyewe.

Katika nafasi ya uenyekiti wamejitokeza watu sita akiwemo Francis Kifukwe ambaye ameshawishiwa na wanachama kwa kuzingatia mchango mkubwa aliowahi kutoa alipokuwa rais.

Wanachama wengine watano waliojitokeza ni Ally Mwanakatwe, Llyod Nchunga, Mbaraka Igangula, Edgar Chibula na Abeid Abeid ‘Falcon’.

Katika nafasi ya makamu mwenyekiti wapo Ayoub Nyenzi, Davis Mosha aliyewahi ‘kumiliki’ klabu ya Moro United, Hashim Lundenga aliyewahi kuwa kiongozi wa kundi la Yanga Family pamoja na Constantine Maligo aliyewahi kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo

Katika nafasi ya ujumbe wamejitokeza wanachama wengi kuanzia Mohanmed Bhinda, Edgar Fongo, Edson Mwandemane, Ahmadi Mamba, Theonest Rutashoborwa, Jackson Mregi hadi David Ngarapi.

Wengine ni Charles Mayala, Abbas Bomba, Majid Rajab, Evans Mtee, Seif Mohammed, Paul Malume, Pascal Kihanga, Salum Rupia, Ramadhani Kampira, Saburi Saburi, Ismail Idrisa, Omari Ndula na Yusuf Yasin.

Vilevile wamejitokeza Ally Mayay, Isaack Mazwile, Ally Bwamkuu, George Mnyama, Lameck Nyambaya, Robert Kasela, Tito Ossoro, Hamisi Ambari, Awadh Juma, Mzee Yussuf, David Luago na Bashiri Mang’enya.

Wanachama wote hao hakuna mamluki na wengi wao kama hawajawahi kutoa mchango wakiwa wachezaji basi wametoa wakiwa wapenzi wakubwa na wanachama.

Kwa hiyo, hii ni fursa adhimu waliyopata Yanga kutengeneza upya safu ya uongozi baada ya ule wa sasa chini ya Imani Madega kumaliza muda wake. Hii ni fursa ya kusafisha uozo uliopo.

Hivyo basi, ni vema wanachama wakatumia busara wakati wa kuweka pingamizi, kwamba wawe na hoja za msingi kupinga badala ya kupinga kwa sababu ya kukomoana.

Yanga haiwezi kupata malaika wa kuongoza klabu hiyo kongwe bali ni lazima watoke miongoni mwa wanachama, ambao kwa hulka hakuna binadamu asiye na makosa.

Wanachama ni lazima waelewe kwamba kufungwa na mahasimu wao Simba si kigezo cha kupoteza sifa ila wezi wa mali za klabu, wasioitisha vikao na mikutano ya wanachama.

Uzoefu unaonyesha kuwa, baadhi ya wanachama hukosa usingizi na kuusakama uongozi timu yao ikifungwa, lakini hufumbia macho wakiambiwa kuwa uongozi umetafuna pesa.

Katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi, wanachama huzungumzia marekebisho ya katiba lakini ukishapita suala hilo huwekwa kando hadi pale kundi moja litakapoonyesha upinzani.

Hivyo, nashauri uongozi utakaoingia madarakani ufanyie marekebisho katiba kwa kuweka vipengele au ibara ambazo zitaepusha migogoro.

Kwanza ionyeshe kwa uwazi ukomo wa madaraka kama inavyoainishwa katika Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Pili ionyeshe jinsi ya kupata viongozi kidemokrasia ama kwa kuchaguliwa au kuteuliwa kama Katiba ya TFF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) zinavyoelekeza.

Katiba iwe na vifungu vinavyokataza wanachama kuwaondoa viongozi kwa aibu kama walivyofanya kwa Madega na wenzake.

Katiba ionyeshe mipaka ya madaraka, kwamba si kila mjumbe wa kamati ya utendaji itakayoingia katika uchaguzi uliopangwa Julai 18, ni msemaji wa klabu hiyo.

Kwa kuwa si rahisi kuandika kila kitu, Katiba hiyo iwe na kifungu kinachoonyesha kwamba katika masuala ambayo hayajaelezwa, yaamuliwe kwa kuzingatia Katiba ya TFF.

Wanachama wajue kwamba, japokuwa klabu yao iko kwenye wilaya ya Ilala, migogoro na masuala yao ya uchaguzi, baada ya kuwa wanachama wa TFF yanasimamiwa kufuata katiba na kanuni za TFF.

Mwisho, wanachama waelewe kuwa, kwa utaratibu huo ulioanza kutumika mwaka 2004, wanachama wanaokimbilia kwa msajili msaidizi wa vyama na klabu za michezo watakuwa wanapoteza muda bure.

Hii ndiyo fursa kwa Yanga kuandika ukurasa mpya wa kuwa na katiba madhubuti na ambayo itaondoa migogoro isiyo ya lazima.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: