Gamba lamponza Kikwete


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version

MRADI wa kujivua gamba umeanza kumyumbisha Rais Jakaya Kikwete. Baadhi ya marafiki zake tayari wamegawanyika; wengine wameanza kukata tamaa na wengine wanajisalimisha kwa wanaotuhumiwa ufisadi, MwanaHALISI linaweza kuripoti.

Taarifa za ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikalini zinasema, tayari baadhi ya marafiki wa Rais Kikwete waliokuwa wakimpa nguvu katika kampeni hiyo, wameanza kumpa ushauri tofauti na ule wa awali.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, kiongozi mmoja mwandamizi katika serikali na CCM amethibitisha Rais Kikwete kuanza kuyumba katika kusimamia kampeni hiyo na kwamba baadhi ya marafiki zake wamegawanyika mapande matatu.

Mtoa habari huyo anasema pande la kwanza, ni lile linaloongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama Tanzania Bara, Pius Msekwa na baadhi ya viongozi waandamizi wengine.

Anasema Msekwa bado anaamini falsafa ya kujivua gamba kwa kuwafukuza kwenye chama Edward Lowassa na Andrew Chenge, sharti itekelezwe ili kukiokoa chama pamoja na hadhi ya Kikwete mwenyewe.

“Ngoja nikwambie, katika hili la kuwafukuza Lowassa na Chenge, ni baadhi ya viongozi wachache sana akiwamo Msekwa wanaotaka litekelezwe. Hata rais anaonekana yuko njia panda,” anasema.

“Akikutana na Msekwa anakubali kwamba ili kukinusuru chama, lazima watu hawa waondolewe kwenye chama, lakini sisi tulio marafiki zake, tukimuangalia kwa makini, tunaona ndani ya moyo wake ana hofu,” anasema mjumbe mmoja wa Kamati Kuu (CC) ambaye yuko karibu na Rais Kikwete.

Habari zinasema Msekwa katika kupanga mkakati wake huo ameutumia mkutano wa wenyeviti na makatibu uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki tatu zilizopita kupima upepo wa jinsi makundi ya Lowassa yalivyojipanga.

“Msekwa ameutumia mkutano ule, kuangalia vipi watu wa Lowassa wamejipanga. Baada ya hapo, amewaambia tukutane Dodoma kwenye NEC,” taarifa zinaeleza.

Alipoulizwa kipi ambacho Kikwete ana kihofia, kiongozi huyo alisema kuna mambo mengi. Lakini kubwa ni amelitaja kuwa “Kikwete hafahamu kitakachofuata baada ya mabwana wale kuondolewa NEC.”

Anasema hatua ya Kikwete kumuangukia Rostam Aziz, baada ya kujiuzulu ubunge ili asaidie kampeni za chama hicho jimboni Igunga, ndiko kulikorejesha nyuma moyo wa waliotaka “mafisadi wafukuzwe kwenye chama.”

Taarifa zinasema Rostam ndiye aliyefadhili helikopta iliyotumiwa na CCM katika siku za mwisho za kampeni za uchaguzi mdogo Igunga, ndiye aliyekuwa kinara wa mkakati wa ushindi na ndiye alitumika kurejesha kundini baadhi ya viongozi wa chama waliogoma kushiriki kampeni.

Aidha, Rostam aliyeombwa na Kikwete kushiriki kampeni hizo, anatajwa kuwa ndiye aliyeshinikiza uongozi wa CCM taifa, kumzuia Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Samwel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe kushiriki kampeni hizo za uchaguzi jimboni Igunga.

Taarifa zinasema ni Rostam aliyeonya kuwa hatua yoyote ya kumpeleka Nape katika uchaguzi huo, ingesukuma wafuasi wake jimboni Igunga kutokipigia kura chama hicho.

Wakati Rostam akijiuzulu wadhifa wake Julai mwaka huu, alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuchoshwa na “siasa uchwara ndani ya CCM.”

Gazeti hili liliwahi kuandika miezi miwili iliyopita, pamoja na CCM kuwaona mafisadi ni “gamba” linalopaswa kuvuliwa; bado ni nguzo muhimu ya Rais Kikwete na chama chake.

Baada ya mkakati huo wa kwanza kuonekana mgumu, taarifa zinasema umetengenezwa mkakati Na. 2 unaotaka Kikwete awafukuze chama Sitta, Lowassa, Nape na Chenge ili kumfurahisha Lowassa na kundi lake.

Hata hivyo, wanaojiita Usalama wa Taifa kumuona Kikwete anaelekea kukosa msimamo katika suala hilo, wameamua kumpa ushauri smwingine wa kuwafukuza Sitta na Nape kwenye uongozi wa juu wa chama hicho.

Hata hivyo, kambi ya Sitta ambayo inajumuisha baadhi ya viongozi wastaafu na wale wa sasa, imejipanga kuhakikisha kuwa hakuna mtu wao anayeng’oka kwenye chama.

“Ukimfukuza Lowassa mle ndani na kumuacha Sitta, hakika hamtakalika. Sasa njia pekee ya kutuliza kundi la Lowassa, ni kumuondoa Sitta na Nape kwenye chama,” ameeleza.

Sitta na Mwakyembe pamoja na Nape wamekuwa wakishutumiwa kuwa wamesaliti chama chao kwa kushiriki kuanzisha chama kipya cha CCJ wakiwa bado ni viongozi waandamizi katika CCM. Baadhi ya makada wamekuwa wakishinikiza wafukuzwe kwa kusaliti chama chao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: