Gavana BoT akana ufisadi


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version
Profesa Benno Ndullu

GAVANA wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndullu amekana matumizi ya kifisadi ya Sh. 760 bilioni kwa mwaka mmoja katika safari za ndani na nje ya nchi.

Taarifa zilizopatikana BoT, Hazina na ofisi kadhaa za serikali zimekuwa zikidai kuwa gavana “anasafiri sana” na kwamba ametumia kiasi hicho katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Lakini alipowasiliana na gazeti hili juzi Jumatatu, Prof. Ndullu kwanza alionyesha  kushangaa kama ambaye hasikii vizuri.

“He! Nisomee tena. Unasema milioni au bilioni…?” aliuliza kwa sauti ya mshangao.

Mwandishi alirudia akisema, “…bilioni! B, yaani B ya baba!”

Ndipo Prof. Ndullu alisema, “Haiwezekani. Bajeti yenyewe ya BoT nzima haifikii Sh. 700 bilioni kwa mwaka. Hiyo ni pamoja na mishahara, safari za ndani na nje, na miradi yetu.”

Katika kilichoonekana jitihada ya kujitetea, Prof. Ndullu alisema, “Hata ukifuatilia ripoti ya CAG – mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali – hutoona hilo. Hata CAG mwenyewe atashangaa.”

Dakika tano baada ya kuwa na mahojiano naye, gavana huyo aliita mwenyewe kwa nia ya kile alichosema kutoa ufafanuzi.

Alisema, kwa mfano, bajeti ya BoT kwa mwaka 2011/2012 ni Sh. 570 bilioni. Alitaja kuwa mishahara, posho na safari za ndani na nje vinachukua Sh. 270 bilioni; na bajeti ya maendeleo ni Sh. 300 bilioni.

Katika sauti ya upole na kuridhika, gavana alisema, “Asante kwa kunipigia. Wengine wangerusha vivyo hivyo. Mimi najua bwana taarifa hizi zinatoka wapi; wala siwezi kukuuliza.”

Taarifa ambazo gavana amekana zinasema malipo ya gavana kwa safari za nje yamekuwa yakipitia akaunti mbili za benki: Akaunti Na. 9949610801 na Na. 9949613701.

Ofisi ya gavana imekuwa ikitajwa katika ofisi zinazotafuna fedha nyingi; ikiwamo ikulu ambako safari za rais nchi za nje zimekuwa zikilalamikiwa kwa kipindi chote cha urais wake.

Prof. Ndullu amehusishwa pia na taarifa kuhusu hali ya uchumi nchini ambako amekuwa akilalamikiwa kwa kutoa taarifa wanazodai si sahihi hasa pale anaposema uchumi “unakwenda vizuri.”

Taarifa kuhusu benki na matumizi yake zimeambatana na takwimu za matumizi ya serikali katika kipindi cha 2011/12.

Katika kipindi hicho, serikali inaelezwa kutumia Sh. 11,172,384,000,000 (trilioni 11) wakati ilikusanya kiasi cha Sh. 6,417,862,000,000 tu.

Tayari matumizi makubwa ya fedha yamewashitua nchi wahisani. Katika mkutano mmoja uliofanyika Marekani, mapema mwaka huu, wahisani walieleza wazi mashaka yao ya ukuaji mdogo wa uchumi Tanzania.

“Hiki ndicho kilio kikubwa hata kwa wadau wa maendeleo. Wanasema matumizi yetu ni makubwa na yasiyokuwa na ulazima,” ameeleza kiongozi mmoja kutoka mashirika ya nchi wahisani aliyehudhuria mkutano huo.

Taarifa zinasema hata danadana waliyokuwa wakipigwa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na Hazina juu ya dhamana ya mkopo wa Sh. 408 bilioni, sababu yake kubwa ni ukata unaoikabili serikali.

Bunge la bajeti la mwaka jana liliruhusu serikali kudhamini TANESCO kukopa Sh. 408 bilioni ili kuwezesha shirika hilo kujikwamua kiuchumi.

Hadi hivi karibuni, wakati serikali ikijiandaa kuwasilisha bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013, fedha hizo zilikuwa hazijatolewa.

TANESCO imekuwa ikipigia magoti mkopo kutoka benki ya Citibank Tanzania Limited ambayo iliahidi kuikopesha serikali kwa niaba ya benki za umma za National Micro-Finance (NMB) na National Bank of Commerce (NBC).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: