Gazeti la Rai lina siri nzito lichunguzwe


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version

WIKI mbili zilizopita, gazeti la kila wiki liitwalo Rai, lilichapisha habari  iliyotushtua wengi. Kwamba kuna mkakati mzito wa kuiangusha serikali ya Rais Jakaya Kikwete unaodaiwa kuendeshwa na MwanaHALISI, mfanyabiashara mmoja na vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hili ni gazeti ambalo liliwahi kuwa maarufu sana huko nyuma, na kwa hiyo lina wasomaji kila kona ya nchi. Ni dhahiri habari hiyo inaweza kuaminika na kusababisha mtafaruku ndani ya serikali yenyewe na kwenye jamii kwa jumla.

Habari ile ilikuwa nyeti na nzito na kwa hiyo nalazimika kuandika makala kueleza haja ya gazeti hili kukamilisha kazi ya kizalendo waliyoianza ya kuelimisha jamii, ambayo wengine wanaona bayana ni mikakati ya kuiangusha serikali ya Kikwete.

Awali nilidhani gazeti la Rai linacheza mchezo wa kuwaondoa wananchi katika kujadili masuala muhimu ya kitaifa, ili kuwafanya sasa wahamie katika kutafuta mchawi huyu mpya anayetaka kuiangusha serikali.

Nikiri wazi kuwa kama huo ulikuwa mtego wa gazeti, mimi nimenaswa na ndiyo maana nalazimika kuhamishia mawazo yangu katika suala hili zito waliloliibua.

Miaka michache iliyopita, gazeti la MwanaHALISI lilichapisha habari ya uchunguzi iliyoonyesha Ridhiwan Kikwete anashiriki katika njama za kuzuia baba yake, Rais Kikwete asigombee kipindi kingine. Uchunguzi ule ulionyesha alikuwa akishirikiana na wenyeviti kadhaa wa CCM mikoa.

Serikali, bila kutafakari mara mbili, baada ya kusoma habari ile, ikaamua kulifungia gazeti.

Ni jambo lililo wazi kuwa serikali yetu inakabiliwa na changamoto nyingi zinazoweza kuiangusha pasipo msaada wa mtu au kundi lolote. Hata wahariri wa gazeti la Rai na mmiliki wake wanajua hili na kulizungumzia hadharani.

Wamekuwa wakiorodhesha mambo kadhaa ambayo wanadhani yanaweza kuiangusha serikali hii. Kwa mfano, katika toleo hilo hilo Na 907, gazeti limeandika, “CCM sasa yafika njiapanda.”

Habari hiyo ilisema kwamba kuna mapande mawili yanayotafunana ndani ya chama. Hakika hakukuwa na tofauti kati ya habari ile na iliyosema “Rais Kikwete ana kundi, anaogopa kila kundi” iliyoandikwa na MwanaHALISI wili iliyotangulia.

Katika habari ile, Rai ilikuwa imejaa majina ya watu ambao ama ni mahasimu wao kisiasa au kibiashara. Gazeti hilo linalomikiwa na mfanyabiashara Rostam Aziz, linataka kuaminisha wananchi kwamba adui wa gazeti la Rai ni adui wa serikali ya Rais Kikwete na adui wa serikali ya Kikwete ni adui wa gazeti la Rai na mmiliki wake.

Mantiki hii ni ya ajabu sana kwa sababu wakati wamiliki wa serikali ni wananchi, wamiliki wa Rai wanabadilika badilika. Awali lilimilikiwa na baadhi ya wazalendo, leo lina Rostam na hatujui kesho litanunuliwa na nani. Kulifanya gazeti hili liwe na hadhi sawa na serikali ya Tanzania ni kuidhalilisha serikali na watu wake.

Orodha ya changamoto zinazoaminika na wananchi walio wengi kuwa zinaweza kuiangusha serikali hii, ni pamoja na mfumo wa ufisadi unaoelekea kuinyima serikali pumzi na kuifanya ipumulie mashine.

Ufisadi ni mfumo uliotamalaki kila kona ya nchi hii na kuyafanya maisha ya watu wengi kuwa magumu sana katika kila sekta. Nchi imo gizani, huduma za afya ziko taabani, elimu bora ni kwa matajiri tu, mikataba ya madini na raslimali za nchi ni siri ya wakubwa.

Si hivyo tu: Mikataba mikubwa imeshikwa na mafisadi na ndugu zao, makampuni makubwa ya kigeni yanalazimishwa kuwapa hisa vigogo wa serikali, haki za watu mahakamani zinachelewa sana au hazipatikani, ardhi inachukuliwa na wageni au matajiri tu, janga la ukame, na rushwa ndani ya ofisi za serikali zinazidi kuongezeka.

Umaskini umekithiri sana kiasi cha kuwafanya watu wanauza damu hospitalini ili wapate mlo mmoja; wengine wanaishi kwa kutegemea idadi ya watoto wachanga wanaokufa hospitalini ili wakazike na wao wapate senti ya kununua mchicha.

Ili kuongeza pato lao kwa kubana matumizi, wanaamua kudunduliza maiti ili ziwe nyingi na kuzika katika kaburi la halaiki kama ilivyotokea hospitali ya Mwananyamala.  Haya yanaweza kuiangusha serikali yoyote duniani bila kuhitaji msaada wa MwanaHALISI, mfanyabiashara maarufu wala vigogo wa CCM wanaoililia chama hicho kinachoangamia katika lindi la ufisadi mkubwa.

Hayati Mzee Mwinamila aliwahi kuimba katika tungo zake, “Rafiki yake Yesu alikuwa Yuda” akimaanisha wanaojifanya ni marafiki wa mfumo ndio waharibifu wa mfumo wao wenyewe.

Rai katika habari hiyo limechambua kwa urefu tena kwa kuorodhesha masuala kadhaa linayodhani maadui wa serikali wanatumia kutaka kuiangusha serikali ya Kikwete.

Yameorodheshwa masuala kama Kagoda, EPA, Richmond/Dowans, migomo, maandamano, na maisha magumu yanayowakabili wananchi walio wengi. Lengo ni kutaka kujitambulisha kama rafiki na mtetezi wa serikali ya Kikwete.

Tunaolifahamu gazeti hilo na watu wake, tunadhani hili ni busu la usaliti kwa serikali ya Kikwete na rais mwenyewe.

Mpaka sasa, gazeti la Rai haliamini kuwa Richmond ilikuwa kampuni ya kitapeli. Linaendelea kutetea usiri unaolizunguka suala la Kagoda kwa kisingizio cha usalama wa taifa, kumbe haya ni makumpuni yanayofahamika wamiliki wake halisi.

Watetezi hawa wa usalama wa taifa, ndio leo wanaokuja na habari kuwa serikali inapinduliwa hivi karibuni. Hata Rais Kikwete mwenyewe amesema tena hadharani kuwa hata yeye aliishtukia kampuni ya Richmond; haijui Dowans na hana hisa nayo; na aliwahi kudokeza kuwa hajui kampuni ya Kagoda.

Kwa kuwa Rais Kikwete yuko  wazi, hawezi kuwa na hofu ya kuangushwa,  kwa hiyo wanaojaribu kuyatumia kujenga hoja ya kuiangusha serikali, wachunguzwe kwa makini sana.

Kwa bahati mbaya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimenunuliwa au vimezama katika ufisadi mfumo. Kila kundi ndani ya CCM lina wana usalama wake. Baadhi yao wamekuwa wanasiasa kuliko wanasiasa wenyewe.

Vinginevyo, ingekuwa vyema vyombo vya usalama kutaka maelezo kutoka Rai juu ya mkakati huu wa kuiangusha serikali. Kupuuza suala hili si jambo jema maana yawezekana pia hao hao wanaosema hivyo ndio wana mpango wa kuiangusha serikali, ila wanasingizia wengine ili kuchelewesha uchunguzi dhidi yao.

Kwa mshangao na masikitiko ya wengi, vyombo hivi vya usalama tutashtukia vikiwaandama waliotajwa na Rai ili kudhihirisha kuwa gazeti la Rai lina ubia na serikali ya Kikwete. Hatutarajii hilo kutokea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: