Genge laundwa kumkabili Kikwete


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 May 2008

Printer-friendly version
Lahofia mabadiliko serikalini
Yeye ajiandaa kuwakabili
Rais Jakaya Kikwete

GENGE la watuhumiwa wa ufisadi nchini linajiandaa kukabiliana na utawala wa Rais Jakaya Kikwete ili kuudhoofisha kabisa, MwanaHALISI limeelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, genge hili sasa linaunda mtandao wa nchi nzima ili "kulegeza nguvu za Kikwete."

Hadi sasa wanaotuhumiwa kuwa kwenye genge, tayari wamekutana mjini Morogoro kwa kikao cha siku moja. Kikao cha pili kimefanyika jijini Dar es Salaam mwezi uliopita.

Vikao vyote viwili vimehudhuriwa na baadhi ya makada na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa zamani serikalini na waandishi wa habari walioitwa kama "waalikwa maalum" ili wasaidie katika kujenga kile walichoita "mkakati usioshindwa."

Taarifa za kuwepo genge hilo na majukumu yake zimekuja wakati kuna taarifa nyingine kutoka ndani ya serikali kwamba Rais Kikwete amejiandaa kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.

Rafiki wa karibu mno wa mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi waliomo serikalini alilidokeza MwanaHALISI kwamba watuhumiwa wamejiapiza kumdhoofisha Kikwete kabla hajawaumbua zaidi.

Viongozi wa genge hilo hawajafahamika bali kuna fununu kwamba limebuniwa na litaongozwa na waliokuwa marafiki wa karibu sana na Kikwete wakati wa mchakato wa kutafuta urais ambao wanajihisi wameenguliwa au kudhoofishwa kisiasa.

"Mambo mengi yanayojitokeza, wameyafanya kwa pamoja au anajua kuwa waliyafanya; kwa hiyo wanasikitika kuona anakaa kimya bila ya kuwatetea au kuwakemea wanaowatishia au kuwaumbua mbele ya wananchi," kimeeleza chanzo cha gazeti hili.

Hata hivyo, taarifa za kuwepo genge hilo zinaonekana kuwa siyo habari kwa utawala wa Kikwete. Ofisa mmoja serikalini amekiri, "Hata rais anajua hayo; usidhani amelala tu. Huyu ni mkuu wa nchi bwana," ameeleza.

Akizungumza kwa kujiamini, ofisa huyo wa ngazi ya juu amesema: "Tunafahamu kinachoendelea. Tuko makini. Nakuhakikishia hawatafanikiwa kudhoofisha utawala."

Ofisa huyo akizungumza kwa sharti la kutotajwa, amesema: "Subiri. Utaona mabadiliko makubwa yatakayotokea katika kipindi cha mwezi mmoja kutoka sasa."

Mtoa habari huyo amesema serikali ina taarifa za kutosha juu ya wanaotaka kuleta vurumai serikalini na hatua waliyofikia katika maandalizi yao.

Amesema genge hili lina nia ya kupaka matope baadhi ya viongozi serikalini, kuwadhoofisha na kuhakikisha kwamba hawatakubalika kwa umma kuchukua nafasi za juu kama uwaziri pale itakapolazimu kufanywa mabadiliko.

Taarifa zaidi zinasema waliolengwa mbali na Kikwete ni Spika wa Bunge, Samwel Sitta, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Dk. Harisson Mwakyembe.

Wengine ni Profesa Mark Mwandosya ambaye ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, na Mbunge Simanjiro, Christopher ole Sendeka, Naibu Spika Anne Makinda, Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii na mfanyabiashara mmoja mashuhuri nchini.

Mtoa habari hizi amesisitiza: "Rais ana taarifa zote. Yuko makini. Amejiandaa kukabiliana na lolote na kamwe hatarudi nyuma."

Kuna taarifa kwamba baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi waliokwishaathirika kwa maamuzi ya Bunge, wana mkakati wa kuhakikisha wanarudi kwenye nafasi zao serikalini na kwamba watafanya kila liwezekanalo kufanikisha hilo.

MwanaHALISI liliwasiliana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, kutaka kupata usahihi wa taarifa hizi alisema, "Sijui kama kuna kitu hicho. Nadhani huo ni uzushi wa mjini wa kawaida usioisha."

Taarifa ambazo gazeti hili limepata zinasema Rais Kikwete ana mpango wa kufumua uongozi kuanzia baraza la mawaziri hadi ngazi ya chini anakofanya uteuzi.

Hatua ya rais kutoteua waziri mpya wa Wizara ya Miundombinu tangu 20 Aprili alipojiuzulu Andrew Chenge, kumewaweka mawaziri matumbo moto na kutoa nafasi kwa wachunguzi wa mambo ya kisiasa kuona mabadiliko hayo kuwa suala linalowezekana.

Tangu kutokea mfumko wa madai ya ufisadi kwa baadhi ya viongozi wa serikali ya CCM, mawaziri wanne wameshajiuzulu.

Hawa ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri waliokuwa katika Wizara ya Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi. Chenge alijiuzulu wiki mbili zilizopita.

Hata hivyo, kuna orodha ndefu ya mawaziri na maofisa wa serikali wanaotuhumiwa kula mlungula kutokana na ununuzi wa rada na ambao kwa sasa wanachunguzwa na shirika la uchunguzi wa ufisadi la Uingereza (SFO) na serikali ya Tanzania.

Imefahamika kuwa kutokana na uteuzi wa mawaziri kuwakumba wale ambao baadaye wanapatikana na kashfa, rais ameanzisha utaratibu mpya wa kupata wateule wake.

"Sasa kila mtarajiwa sharti achunguzwe kwanza na chombo maalum kabla ya kukabidhiwa madaraka ili kumwondolea rais aibu ya kujirudia kila mara," ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali.

Tayari rais amefanya mabadiliko mara nne katika Baraza la Mawaziri tangu achukue madaraka ya kuongoza nchi karibu miaka miwili na nusu sasa.

Mara ya kwanza alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kubadilisha baadhi ya mawaziri wakiwemo Karamagi kutoka Biashara na Viwanda kwenda Nishati na Madini na Dk. Msabaha kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wakati huo pia Chenge aliyekuwa Afrika Mashariki alipelekwa Miundombinu kuchukua nafasi ya Basil Mramba aliyekwenda Biashara na Viwanda.

Mara ya pili mabadiliko yalitokana na kifo cha Juma Akukweti aliyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu aliyeshughulikia masuala ya Bunge.

Mara ya tatu mabadiliko madogo yalifanywa kuziba nafasi ya Asha-Rose Migiro aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuwa msaidizi wake.

Rais alifanya mabadiliko ya nne alipovunja baraza zima la mawaziri na kuliunda upya Februari mwaka huu. Alimrejesha Chenge kwenye wizara yake ya awali akipuuza kelele za umma na vyombo vya habari za kudai "hakustahili."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: