Gharama, usumbufu ziara ya Obama India


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version
Rais Barack Obama akiwa India

JUMAPILI iliyopita, Rais Barack Obama wa Marekani aliingia jijini New Delhi, India kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili. India ni moja ya nchi anazozitembelea katika Bara la Asia, nyingine ni Indonesia, Korea ya Kusini na Japan.

Aidha, Obama anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Kiuchumi wa Nchi za Asia na Pacific (APEC) utakaofanyika mji wa Kyoto, Japan na ule wa Umoja wa Nchi Tajiri Duniani (G20) Toronto, Canada.

Mahasimu wa kisiasa wa Obama nchini Marekani wameishutumu ziara hii kuwa ni ya matumizi makubwa ya fedha, na inasadikiwa itagharimu dola za Kiamrekani 200 milioni – hela za walipa kodi wa Marekani. Hata hivyo Ikulu ya Marekani imekataa kutaja gharama halisi.

Kwa mfano, inakisiwa kwamba gharama za kuirusha angani ndege yake ‘Air Force One’ aina ya Boeing 747 Jumbo Jet ni dola za Kimarekani 50,000 hadi 60,000 kwa saa.

Aidha alipokuwa mjini New Delhi maafisa wa ulinzi wa Obama walikuwa na hofu ya rais wao kushambuliwa na walenga shabaha wakiwa juu ya maghorofa wakati akipita katika mtaa mmoja kwenda kwenye kaburi la Mahatma Gandhi lililoko Mani Bhavan.

Gandhi ni kiongozi wa kisiasa na wa kidini aliyepigania uhuru wa India katika miongo ya mwanzo ya karne iliyopita na alifariki kwa kuuawa mwaka 1947, baada tu ya nchi hiyo kujipatia uhuru.

Wahandisi kutoka jeshi la Marekani waliamua kujenga handaki la urefu wa kilometa moja ambalo lisingeweza kuharibiwa kwa bomu kwa ajili ya shuguli hiyo ya dakika 40 na baadaye kuliondoa. Gharama ya kujenga handaki hili haijajulikana bado.

Kwa hiyo, katika ziara yake ya Asia, hii ya India ndiyo imeibua gumzo kubwa, hasa katika masuala ya ulinzi wake binafsi. Inasemekana ulinzi wake ulikuwa mkali zaidi kufanyiwa rais wa Marekani tangu baada ya Vita Kuu II vya Dunia.

Hii inatokana na vuguvugu la vitendo vya ugaidi katika eneo hilo la Asia, hasa katika nchi jirani za Pakistan na Afghanistan ambako vikosi vya Marekani (na vile vya NATO), vikishirikiana na vile vya nchi hizo mbili vinapambana na wapiganaji wa vikundi vya Kiisilamu vya Taliban na Al Qaeda.

Novemba mwaka 2008, magaidi walishambulia hoteli tatu za kitalii katika mji wa Mumbai na kuua watu 164, wengi wao wakiwa raia wa nchi za kigeni. Uchunguzi ulionyesha wahusika walitokea Pakistan.

Kufuatana na msemaji mmoja wa Ikulu ya Marekani, ulinzi wa Obama ulijumuisha mizingiro mitano (security rings) ya wana usalama ambayo ilishirikisha mamia ya maafisa wa usalama, miwili kati ya mizingiro hiyo ikiwa mita chache tu kutoka kwa Obama.

Mizingiro mingine mitatu ilishirikisha vikosi maalum vya wanausalama wa India, National Security Guards (NSG) na kile cha Kijeshi—Indiann Paramilitary Forces (IPF) na vikosi vingine vya polisi vya New Delhi.

Aidha, vikosi vya manowari za kivita vilikaa katika hali ya utayari karibu na pwani ya Mumbai.

Kufuatana na hali hii, ulinzi mkali kwa Obama si kitu cha kufanyia mzaha na hasa ikizingatiwa kwamba yeye, mkewe Michelle na ujumbe wake ulipangiwa kufikia katika hoteli ya kitalii ya Maurya Sheraton mjini New Delhi.

Lakini kabla ya kwenda New Delhi, siku ya Jumamosi Obama aliingia katika mji wa Mumbai ambapo ulinzi uliomzunguka haujawahi kutokea katika historia ya mji huo, bila shaka likikumbukwa hilo tukio la kigaidi la mwaka 2008.

Mamlaka ya mji wa Mumbai ilitoa amri ya kukata, kuangusha na kuondoa matawi yote makavu, pamoja na nazi zenyewe zilizo juu ya minazi pembezoni mwa barabara alizopita Obama kwa hofu kwamba ingeweza ikaangukia msafara wa Obama na kuzua tafrani.

Aidha, taarifa zinasema katika mji wa New Delhi mamlaka za mji zilitoa amri za kuwadhibiti wafugaji wa mbwa, nyani na ngedere kwa kuwaamuru kufungia wanyama hao hadi Obama atakapomaliza zira yake. Adhabu kali zilitangazwa kwa mtu yeyote ambaye angeonekana akitembea na wanyama hao barabarani.

Aidha, vikosi maalum vya mamlaka ya mji huo vilipewa kazi ya kuwasaka wanyama hao wasiokuwa na wenyewe ili kuwafungia.

Wasiwasi ulikuwa kwamba wanyama hao, hasa nyani wasiofungiwa wangeweza kuvamia msafara wa Obama akipita katika mitaa ya Mumbai na kuweza kusababisha tafrani kubwa. Kwani ni kwaida kwa wakazi wa mji huo kuona manyani yakipita huku na huko.

Isitoshe, hoteli ya Maurya Sheraton alimofikia Obama haiko mbali sana na msitu wa Central Ridge ambao ni makazi ya manyani wengi, na mamlaka ya mji huo ililazimika kukodisha mamia ya wataalam maalum wa kuhakikisha wanyama hao wanabakia humo humo msituni katika kipindi cha masaa 24 Obama alipokuwa New Delhi.

Idara inayotoa ulinzi kwa marais wa Marekani, ilitoa taarifa kuhusu wasiwasi wa usalama wa eneo la msitu huo, kwamba ni eneo ambalo magaidi wengeweza kulitumia kufanya mashambulizi.

Aidha, sehemu yote hiyo, pamoja na eneo la msitu linalotazamana na hoteli ya Maurya Sheraton ziliwekwa taa zenye mwanga mkali kuwezesha wanausalama kulinda makazi ya Obama.

Eneo lote linalozunguka hoteli hiyo, kulikuwepo makomandoo 250 wa kikosi cha NSG, huku makumi ya walenga shabaha wakiwekwa juu ya maghorofa ya jirani, na juu ya hoteli yenyewe.

Minara maalum ya walinzi na wanausalama ilijengwa kuzungukia hoteli na walenga shabaya wenye bunduki zenye darubini kali waliwekwa kulinda.

Maafisa wa usalama wa Bunge mjini New Delhi walitoa agizo kwa idara ya polisi ya mji huo kukagua magari yote yaliyokuwa yanaingia ndani ya eneo la Bunge siku ya Jumatatu.

Ziara ya Obama nchini India pia imeleta mguso hasi kwa imani ya dini mbili kuu nchini humo – Wahindu na Waisilamu. Kwa kiasi fulani imeathiri shamra shamra za sikukuu kubwa ya Wahindu–Diwali ambayo husherehekewa kila mwaka mwezi huu.

Aidha, Waisilamu nao wameripotiwa kuchukizwa na habari kwamba ndani ya ujumbe wa Obama kulikuwamo mbwa mmoja bingwa wa kunusanusa ambaye alikuwa na jina la ‘Khan.’

Iliripotiwa na magazeti ya Mumbai kwamba mbwa huyo, alikuwamo ndani ya ndege ya kijeshi iliyotua katika uwanja huo na shingoni mwake kulikwa na jina ‘MWD Khan.’ Khan ni jina la Kiislamu hasa nchini India na Pakistan na wanaona Marekani ilifanya hivyo kwa makusudi.

0
No votes yet