Ghasia: Hakuna siri ya uovu


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 28 April 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

NILIPOSIKIA habari kuwa Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Utumishi) Hawa Ghasia amesema kuwa mtu atakayekutwa na nyaraka za siri za serikali ambazo anazitumia kwa manufaa ya kisiasa atachukuliwa hatua, nilipatwa na mshangao.

Kauli ya Ghasia ilikuja baada ya kuulizwa wiki iliyopita na Mbunge wa Matemwe, Kheri Ameir aliyetaka kujua kama kuna watu waliokamatwa kwa kuvujisha siri za serikali katika mwaka uliopita.

Maswali hayo na majibu ya waziri yalinifanya nijiulize, “Hivi hawa watu wanaumwa? Hivi hizo zinazoitwa nyaraka za siri, ni nyaraka gani hasa?

Ni wazi kuwa wabunge waliokuwa wanalengwa ni wale ambao walikuwa wanatumia majukwaa ya kisiasa kuibua kashfa mbalimbali za kifisadi na ambao kinara wao ni mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA).

Na hili halina utata kwani kuna baadhi ya wabunge waliomtaja hivyo kwa jina na katika majibu yake Bi. Ghasia alithibitisha kuwa wanaozungumzwa ni wabunge.

Hii ina maana kuwa Ghasia alikuwa anazungumzia nyaraka zilizotumika kufichua ufisadi wa EPA na makampuni ya Meremeta, Deep Green, Mwananchi Gold, Tangold na ufisadi mwingine mkubwa.

Na kwa siri, wana maana ya taarifa za kuoneesha mipango ya wizi, mazungumzo ya njama za kuiibia serikali na mazungumzo ya kuzima au kuharibu ushahidi. Vitu hivi kwao ni siri kubwa inayotakiwa kulindwa.

Lakini hakuna siri ya uovu au uvunjaji sheria na hakuna sheria inayotungwa kutetea au kulinda wizi na ufisadi au matumizi mabaya ya ofisi.

Nyaraka za siri ni zile zinazotimiza masharti fulani ya kisheria mojawapo likiwa kutangazwa hivyo na chombo chenye uwezo wa kufanya hivyo kisheria au kutokana na asili yake zinaangukia kwenye sehemu hiyo.

Nyaraka zinaweza kuwa za “siri” kwa maana ya kiofisi lakini si kwa maana ya masuala ya usalama wa taifa au ulinzi wa taifa au kwa maana ya Hifadhi ya Nyaraka za Taifa.

Ghasia akilielewa hili atatambua kuwa nyaraka zinazohusiana na Kagoda, Meremeta, Mwananchi na EPA na wenzao, kwa vile zinahusu uhalifu na jinsi ambavyo taasisi za umma zimehusika na uhalifu huo, haziwezi kamwe kuwa nyaraka za siri.

Tukifanya hizo kuwa nyaraka za siri, tutakuwa tumetoa uhuru kwa watu wachache kutuibia.

Katiba ya Jamhuri inawalinda Watanzania wote pamoja na wabunge. Tatizo tulilonalo sasa ni tatizo la serikali yenyewe na wabunge wanaouliza maswali yasiyo na kichwa wala miguu.

Kwa mfano, Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri inasema kila mtu ana haki ya kutafuta na kupata habari mbalimbali na ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

Zaidi ya yote inasema kuwa kila raia ana haki ya kupewa taarifa ya matukio mbalimbali nchini ambayo ni “muhimu kwa maisha na shughululi za wananchi na pia juu ya masuala ya jamii”.

Kwa maneno mengine, ili mwananchi aweze kuwa na maoni sahihi na ajiandae kupiga kura ambayo matokeo yake yanaweza kugusa maisha yake, sharti awe na haki ya kujua wale wanaomuongoza ni watu wa aina gani.

Kama sehemu ya ujuzi huu imefichika katika kurasa za nyaraka mbalimbali (kwani humo tunaweza kuona viongozi wetu wanafikiri vipi na kuamua vipi), basi ni haki yake kupata taarifa hizo.

Kimsingi, leo hii tulitakiwa tuwe na sheria ya uhuru wa habari (Freedom of Information Act) ambayo inalazimisha watumishi wa umma kutoa taarifa wanazoombwa na raia, taasisi au jamii bila kujiumauma.

Sheria kama hiyo inatakiwa iandike adhabu kwa mtumishi yeyote ambaye anachelewesha au anazuia kutoa taarifa hizo.

Kwenye nchi kama Marekani, Jaji akimuamuru Meya wa Mji fulani kutoa taarifa za manunuzi fulani, anampa muda wa kuhakikisha taarifa hizo zinakuwa zimetolewa bila kuzuiliwa na kila siku anayochelewesha basi anakatwa mshahara na ofisi yake inalimwa faini.

Sheria kama hiyo inafaa Tanzania. Itafanya walio na taarifa mbalimbali kuzitoa au watalimwa faini (siyo ofisi zao tu bali hata wao binafsi na wakichelewa zaidi wanatiwa pingu), hadi wakisikia mtu anaomba taarifa wanakuwa wa kwanza kuzitoa.

Kama sheria hiyo ingekuwepo wala tusingekuwa tunahangaika na kuzunguka zunguka kupata nyaraka hizi ambazo si za siri

Kwa hiyo, kauli ya Ghasia ni ya vitisho; siyo kwa kina Slaa bali kwa watumishi serikalini. Nia ni kusakama mashujaa ambao hawajatunzwa kwa nyimbo wala kwa mapambo; wale ambao wamechoshwa na uzembe na wizi wa mali za umma na wameamua kuwafichua wahusika.

Wale waliofichua EPA wanatakiwa kupongezwa, wale waliofichua Meremeta, Kiwira, na mengine mengi ndio mashujaa ambao wanahitaji kushangiliwa Bungeni. Inashangaza kina Kaboyonga na Nyalandu wanataka kuwatisha mashujaa wetu.

Wabunge ambao wanaguswa na usiri na wanataka usiri wanaonesha ni jinsi gani wamepitwa na wakati kwani badala ya kuwaunga mkono mashujaa wao wanataka kuwakandamiza.

Wabunge wa aina hiyo ambao wako tayari kutetea usiri wa ufisadi na kuwatishia wananchi, wamekosa mwelekeo na sehemu yao, kama ile ya mafisadi, ni kizimbani na siyo katika Bunge letu.

Wabunge wanaohitajika Tanzania ni watetezi wa nchi na wasioogopa kuchukua upande wa haki, siyo wabunge wanaojaribu kujifanya wanatetea sheria kumbe wanataka kutetea wavunja sheria.

Hivyo, binafsi na kwa niaba ya wapambanaji wengine nawatia shime Watanzania wote ambao wanashiriki kikamilifu katika kufichua mbinu za kifisadi, njama za wizi na wale wanaohusika na mipango hiyo ya kuzimu.

Ninawatia shime watendaji serikalini na watumishi ambao wameona ni bora kupata “mateso na watu wa Mungu, kuliko kujifurahisha katika ufisadi kwa kitambo.”

Ujumbe wangu ni kuwa kina Ghasia na watendaji wengine serikalini wanaoogopa na kugwaya kuwa siri zao au za watu wao zitazidi kuibuliwa, wasiogope.

Wkifanya mambo kwa uwazi hawatavumilia wavunja sheria (kama wao wenyewe walivyofanya kwenye DECI na Kagoda) na hakutakuwa na haja ya kutafuta habari hizi.

Anayeficha uovu naye ni mwovu hata kama anatumia jina la serikali.

0
No votes yet