Giza Tanzania hadi lini?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KAMA hakuna kauli moja ya ufumbuzi wa tatizo la upungufu wa umeme nchini, kwanini tusiamini kuwa serikali imeshindwa uwajibikaji?

Kwa wiki kadhaa sasa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lililopewa mamlaka ya kuzalisha umeme na kuusambaza kwa wateja mbalimbali, linatoa umeme kwa mgao.

Mikoa 18 iliyounganishwa na Gridi ya Taifa inapata umeme kwa mgao kwa saa zisizo idadi muafaka. Wakati siku nyingine eneo lako linakosa umeme kuanzia saa 12 au 12.30 asubuhi, siku nyingine unakosa kuanzia saa 2 au 2.30 asubuhi.

Siku nyingine umeme utarudishwa saa 12 au 12.30 magharibi na siku nyingine mpaka saa 1.30 usiku ndipo unarudishwa. Usipozimwa asubuhi, utazimiwa kuanzia magharibi mpaka saa 5 au 6 usiku.

Lakini, inashangaza pia kwamba kwa siku tatu mfululizo, eneo lako linaweza kukosa umeme kuanzia saa 12.30 asubuhi mpaka saa 12.30 magharibi utakaporudishwa.

Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), mmikili na mchapishaji wa gazeti hili, pamoja na la Mseto, mahsusi kwa michezo na sanaa, zinajua vizuri machungu ya mgao wa umeme.

Ofisi zake zilizopo Kinondoni, Dar es Salaam, kwa siku tatu mfululizo – Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, zilikosa umeme kuanzia kati ya saa 12.30 na saa 2 asubuhi mpaka kati ya saa 12.30 na saa moja usiku. Jumatatu, 4 Julai 2011, umeme ulizimwa saa 2.30 asubuhi mpaka saa moja kasorobo usiku.

Utaratibu huu inawezekana ndio kawaida hata maeneo mengine ya mkoani Dar es Salaam na mikoa mingine nchini. Uzimaji na urudishaji umeme haupo kwa mpangilio.

Umeme wa mgao unaumiza wananchi kwa sababu unaathiri shughuli zao za uzalishaji mali na matumizi ya nyumbani. Unaathiri shughuli za uzalishaji ofisini na viwandani.Wiki iliyopita, maofisa watendaji wa viwanda na makampuni ya uzalishaji bidhaa na utoaji huduma, walilalamika athari za mgao wa umeme, ikiwemo kupunguza kiwango cha uzalishaji huku gharama zikipanda kwa kasi.

Katika tatizo hili kubwa, mbona viongozi wa serikali wanatofautiana kauli kuhusu njia za kulitatua? Iweje umma usielezwe kwa ufasaha ni lini tatizo litakwisha?

Je, serikali imeshindwa ufumbuzi au kuna njama za makusudi za kuhujumu uchumi na maisha ya watu? Sasa nani atathubutu kujibu maswali haya? Haiwezekani kitendawili kikose mteguzi!

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)