Gonjwa la wizi wa mitihani bado linatutafuna


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version
Uchambuzi

LILE gonjwa lililovuma kwa nguvu sana mwaka 1998 hadi kusababisha serikali kufuta mtihani wa taifa wa kumaliza kidato cha nne, mwaka huu limeibuka tena.

Juzi Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza kufuta mtihani wa Hisabati uliokuwa ufanyike Jumatatu baada ya kuvuja katika  maeneo mengi nchini.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba hali hii ya kuvuja kwa mitihani imejirudia, lakini kibaya zaidi imevuja wakati kukiwa na tuhuma nzito za kughushi kwa vyeti vya kidato cha nne kutoka Baraza la Mitihani pia.

Wiki iliyopita Baraza la Mitihani lilitangaza kufuta matokeo ya mitihani ya walimu zaidi ya 800 kutoka Chuo cha Ualimu cha Kange, mkoani Tanga.

Sababu kubwa iliyotolewa ni kwamba walimu hao walitumia vyeti kwa vya kughushi.

Aidha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefikisha mahakamani watumishi wake kadhaa kwa tuhuma za kuwa na vyeti vya kughushi kutoka Baraza la Mitihani.

Jamii yetu kila kukicha inazidi kutopea katika rushwa-ufisadi. Kila kitu kinatumbukia katika ufisadi. Ni jambo la hatari kwamba tamaa ya kupata fedha imetufikisha mahali ambapo hakuna anayejali tena.

Mtunga mtihani anatafuta jinsi ya kuondoka na karatasi moja ambayo ataitumia kujipatia kipato cha ziada.

Mkurugenzi wa serikali anatafuta semina na warsha kwa udi na uvumba ili aweze kujipatia kipato cha ziada bila kujali kama anathiri majukumu yake ya kikazi.

Halikadhalika kwa askari wa usalama barabarani anasaka kipato cha ziada kwa kupokea kitu kidogo kutoka kwa madereva.

Hakika, ugonjwa huu wa kutokujali maadili na maslahi ya taifa ndiyo sasa umetufisha mahali tumeamua kuweka elimu yetu rehani.

Jamii imefikia hatua ya kusadiki kwamba elimu ni kusaka cheti, iwe kwa kununua, au kwa kununua mtihani; hakuna kujali maarifa yoyote ambayo mtu anapata kichwani. Hali hii ndiyo inayotufanya  kuweka taifa rehani.

Taifa linawekwa rehani kwa sababu ya njaa ya watu wanaosaka fedha ya kununua mboga; taifa linahujumiwa kwa sababu kuna watu wameamua kwamba wao wanataka kula leo, hawataki kujenga tena taifa.

Swali la kujiuliza: Kama siku hizi watu wananunua vyeti, wanajipachika sifa za kuwa wasomi wa shahada za falsafa; wananunua shahada kwenye mtandao; taifa hili linakwenda wapi?

Kama watu hawataki tena kukaa darasani kuchemsha bongo ili kupata maarifa; bali wanatumia njia ya mkato kupata kile wanachopenda kuita, “mafanikio ya maisha” nini kitazuia kupigwa mnada kwa taifa hili? Nani atakuwa mwerevu?

Ugonjwa huu wa njia ya mkato ndio umetufanya Watanzania tukose maadili, tukose uzalendo na tukose hata hisia za woga juu ya vitu vinavyotutambulisha kama taifa.

Mtumishi wa serikali aliyeajiriwa leo anatamani kuishi maisha sawa na yule ambaye amekaa kazini miaka 10 iliyopita.

Mtoto wa shule anatamani aishi maisha kama vile anafanyakazi. Matamanio ya wote hawa ni mazuri kama wangekuwa wavumilivu ili wafikie mwisho huo kwa njia za haki na halali.

Lakini kwa bahati wengi wanaotaka kupata mema haya, wameamua kutafuta njia ya mkato. Hakuna kujali njia ya kutumia kufikia mema hayo, cha msingi ni kufikia mema.  

Ndiyo maana baada ya kusikia kwamba mtihani wa Hisabati wa kidato cha nne umevuja, mawazo yangu yalinipeleka kwenye kitu kimoja tu:

Ni dhahiri kwa uchanga wa taifa hili na changamoto za dunia ya sasa kama hatuwezi kuyafanya mataifa mengine yaamini mfumo wetu wa elimu, tunataka kujenga picha mbaya jwa wasomi wetu.

Je, hata baada ya juhudi za makusudi zinazofanywa na baadhi ya makampuni ya kuajiri watu kutoka nje kwa kisingizio cha kijinga kabisa cha kuzungumza Kiingereza safi, sasa tunawapa kisingizio kingine?

Kwamba mwisho wa yote hata mfumo wetu wa elimu haruhusu kupata watu wenye ujuzi unaolingana na vyeti walivyobeba, hivyo tunaruhusu kuwa manamba ndani ya taifa letu wenyewe!

Hakuna mtu anayeweza kubisha ukweli wa dhahiri kwamba uchi wa akili ni mbaya kuliko wa nyama.

Kwa maana hii basi, kama tumeamua sasa kuishi kwa kununua na kuuza mitihani ili kujenga taifa linalojidai linasomesha watu wake, basi tuwe na hakika kuwa taifa hili lina mwisho mbaya kuliko hata utumwa.

Taifa linapanda laana mbaya kwa kuruhusu mfumo wake wa elimu kuingiliwa na wizi wa mitihani.

Bila shaka taifa linastahili kutumia kila nguvu yake inayowezekana kuhakikisha wote wanaokuza au kusadia kwa njia yoyote ile kuvuja kwa mitihani wanakumbana na mkono mrefu wa dola.

Mwaka 1998 janga la kuvuja kwa mtihani lilipojitokea kwa kiwango cha juu kabisa, serikali hakujali kuwajibisha yeyote.

Hata hali hiyo ilijitokeza kidogo miaka ya 2000, pia haikuonekana kama ni jambo la kushtua. Wala mtihani wenyewe haukufutwa.

Safari hii Mtihani umefutwa, lakini hapana shaka wanaonufaika na biashara hii haramu wataendelea kupeta. Ni matumaini ya wananchi kwamba wahusika watashughulikiwa kikamilifu.

0
No votes yet