Haki ya Dk. Ngunangwa ilipwe tu


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 21 January 2009

Printer-friendly version
Mwanasheria Mkuu hana mamlaka ya kuzuia mafao
Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika

ALIYEKUWA mbunge wa Njombe Kusini (1990-1995) kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ndembwela Ngunangwa, hajalipwa mafao yake yanayofikia Sh. 721 milioni mpaka sasa.

Mafao aliyopaswa kulipwa Dk. Ngunangwa miaka 13 iliyopita na Wizara ya Fedha, sasa yanashinikizwa kwa amri halali ya Mahakama Kuu. Lakini Wizara ya Fedha inasema eti lazima mafao hayo yaidhinishwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hii ni ajabu sana katika mfumo wa utawala wa sheria tulionao ambao hauruhusu maamuzi mengine zaidi ya yale yaliyotolewa na chombo cha utoaji haki, ambacho kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ni Mahakama.

Ni mahakama iliyotoa uamuzi kuhusu mafao ya Dk. Ngunangwa.

Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba ni kweli Dk. Ngunangwa alishinda kesi ya kuidai serikali mafao yake.

Msemaji huyo alisema mahakama iliagiza Dk. Ngunangwa alipwe mafao yake lakini suala hilo, anasema, lilikuwa limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuona alipweje na kwamba ni Mwanasheria Mkuu huyo mwenye mamlaka zaidi katika suala hilo kuliko mahakama.

Ingiahedi akamalizia kauli yake kwa kusema,“…hatuwezi kumlipa Dk. Ngunangwa bila idhini ya AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali).”

Siwezi kumlaumu ofisa huyu wa serikali kwa sababu si mwanasheria na inawezekana sana hata hiyo amri ya mahakama inayoamuru kulipwa mafao yake Dk. Ngunangwa, hajapata kuiona tangu ilipotolewa miaka 13 iliyopita.

Ili kuweka mambo sawa, ki-Katiba hakuna mamlaka yoyote iliyo juu ya Mahakama katika kutoa haki nchini petu; ndio maana Mwanasheria Mkuu naye huwa anashtaki mahakamani kwa niaba ya serikali kama alivyofanya wakati wa kuzuia migomo ya walimu mwaka jana.

Namsihi msemaji wa Wizara ya Fedha awe anapata maelezo ya kisheria kutoka kwa wanasheria wa wizara kama wapo au wale waliopo ofisi ya Mwanasheria Mkuu kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari hasa linapohusu suala lenye mtizamo wa kisheria.

Naona amepotosha umma kwani alichokisema ni kinyume cha Ibara ya 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kuhusu mamlaka iliyonayo mahakama katika kutenda haki.

Ninachofahamu ni kwamba mwanasheria mkuu anapaswa kulipa mafao hayo – yaliyoamriwa na Mahakama – bila ya kuyafanyia marekebisho ya aina yoyote. Kama Mwanasheria Mkuu hakukubaliana na uamuzi wa mahakama kuu alipaswa kukata rufaa katika muda uliotakiwa kisheria.

Kama alichosema Mduma ndicho kinachofanyika, basi hicho kitendo cha kudharau mahakama ambacho kwa mujibu wa sheria, ni kosa la jinai linalomstahili mkosaji kufungwa jela.

Sifahamu kwa nini Dk. Ngunangwa hajachukua hatua ya kufungua mashtaka mengine dhidi ya mwanasheria mkuu ambayo ni ya kudharau amri halali ya mahakama.

Kwa mujibu wa maelezo ya vyombo vya habari vilivyomnukuu Dk. Ngunangwa mwenyewe, wakili wake, Katibu wa Bunge, na Msemaji wa Wizara ya Fedha, mbunge mstaafu huyo amekuwa akidai mshahara na mafao anayostahili kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Watumishi Wastaafu wa Kisiasa ya Mwaka 1999 (iliyorekebishwa).

Tarehe 9 Mei 2005, aliishinda serikali katika kesi Na. 382 aliyoifungua Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mwaka 1996. Alimshitaki Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Dk. Ngunangwa anadai malimbikizo ya mshahara wake wa mwisho Sh. 2,436,690, pensheni ya miaka 10 (asilimia 40 ya mshahara wake wa kila mwaka) Sh. 518,527,632 pamoja na riba ya asilimia saba kwa kiwango cha mahakama baada ya hukumu (2006-2008) ambayo ni sawa na Sh. 78,324,963.

Madai mengine kwa mujibu wa mchanganuo wa Jaji Thomas Mihayo wa 14 Julai 2008 kufuatia Mwanasheria Mkuu kushindwa rufaa mara mbili, ni madai ya posho baada ya kumalizika muda wa ubunge ambayo ni Sh. 105,265,008 na riba ya asilimia saba ya Sh. 15,282,920.

Mafao mengine ni pensheni yake aliyopunjwa ya Sh. 2,500,000 kwa riba ya asilimia saba, fidia ya gharama za kesi ya Sh. milioni moja pamoja na riba yake ya asilimia saba ambayo ni Sh. 169,167.

Yote hayo, yanafanya stahili yake ya mafao kuwa ni jumla ya Sh. 721,472,606.

Kaimu Katibu wa Bunge, Kombe amekiri kuwa Dk. Ngunangwa anadai mafao hayo, lakini bunge halihusiki na deni hilo kwa kuwa sheria ya malipo ya mafao ya watumishi wastaafu wa kisiasa iko chini ya Wizara ya Fedha.

Wajibu wa bunge ni kuthibitisha tu kama Dk. Ngunangwa alikuwa mbunge au la na wajibu huo, alisema, Bunge lilishautekeleza kwa kuthibitisha Dk. Ngunangwa alikuwa mbunge. Taarifa ya Bunge kuhusu suala hilo ilitolewa 14 Juni 2006.

Dk. Ngunangwa alihama chama cha CCM kwenda NCCR-Mageuzi kushindana na mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Anna Makinda, ambaye ni Naibu Spika. Hata hivyo, Dk. Ngunangwa amerudi CCM.

Kwa msingi huu, imekuwa ikidaiwa nje ya mahakama kwamba Dk. Ngunangwa “anafanyiwa mizengwe ya kutolipwa mafao yake kutokana na sababu za kisiasa,” lakini hilo haliwezi kuingilia utekelezaji wa sheria kwa mujibu wa amri halali ya mahakama.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali anawajibika kuielekeza Wizara ya Fedha kwamba mbunge mstaafu huyo alipwe stahili yote ya mafao yake.

Dk. Ngunangwa aliwahi kuwa mtaalam mshauri wa Benki ya Dunia katika fani ya elimu ya uchumi na maendeleo, sayansi ya utawala, sera na utafiti. Kwa sasa ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ambako amefundisha kwa miaka minane sasa.

0
No votes yet