"Hakimu anayeng'ang'ania kesi hafai"


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 19 August 2008

Printer-friendly version

PALE Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliposema ujaji na uhakimu si katika kazi zinazopaswa kufanywa na mtu yeyote tu hata asiye na nidhamu, alikuwa anajenga msingi imara wa uadilifu miongoni mwa wanataaluma wa sheria.

“Kuna kazi katika jamii yetu ambazo zinaweza kufanywa na watu wasio na nidhamu. Watu ambao uadilifu wao unatia shaka. Kuwa Jaji au Hakimu si moja ya kazi hizi,” alisema Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1984 wakati akifungua mkutano mkuu wa majaji na mahakimu mkoani Arusha.

Mwalimu alikuwa anazungumzia uadilifu katika kazi ya uanasheria. Hata kanuni ya tabia ya maofisa wa Mahakama inaelekeza Jaji au Hakimu kufanya maamuzi akiwa huru na si vinginevyo.

Lakini uhuru wa mahakama ambao ni pamoja na uhuru wa jaji au hakimu mwenyewe, hauruhusu uendeshaji kesi kibabe au kwa kujiamini kupita kiasi hata kuamua kutosikiliza au kutonakili hoja za moja ya pande husika katika kesi.

Lazima ile imani ya kitaaluma kwamba haki haipaswi tu kutendeka bali ionekane inatendeka, ithibitike pasina shaka. Shaka yoyote (ikiwemo pingamizi lolote) ikitolewa, lazima ifanyiwe uamuzi kwa misingi ya sheria.
 
Mara nyingi walalamikaji au walalamikiwa au washtakiwa huomba hakimu fulani ajitoe katika kesi kwa hofu kuwa hatatenda haki kwa sababu mbalimbali kama za mgongano wa kimaslahi – labda kwa kuwa ana husiano wa karibu na mmoja wa pande za kesi au tu kwa shaka kuwa haonyeshi kuzingatia haki katika muendelezo wa kesi.

Ikitolewa hoja ya kuomba hakimu ajitoe, inampasa hakimu atoe uamuzi wa kukataa au kukubali. Hata hivyo makimu wengi wamekuwa wakikataa na kuamua kuendelea kusikiliza kesi bila kutambua kwamba mazingira ya mashaka ya kutenda haki yanakuwa yameshajitokeza.

Kuna wanaodhani kwamba kung’ang’ania kusikiliza kesi ambayo hakimu amekataliwa ni kudumisha uhuru wa mahakama. Eti mahakama haiwezi kuingiliwa au kuambiwa vinginevyo. Mahakimu hao hawakumbuki kuwa kukubali kujitoa ni kuipa mahakama fursa ya kutenda haki.

Mahakimu wanaong’ang’ania kesi hata wakishaombwa kujitoa, hawafai maana wanadhalilisha uhuru wa mahakama na kuzorotesha utawala wa sheria.

Ndio maana pale suala la hakimu kung’ang’ania kesi likifikishwa Mahakama Kuu, uamuzi huwa ni wa kumuondoa hakimu mhusika, kama alivyofanya hivi karibuni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Lawrence Mchome, alipokubali ombi la kumuondoa hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi ya tuhuma za wizi wa Sh. 230 milioni zilizoibwa Benki ya NMB.

Awali mawakili wa utetezi walikuwa wamemuomba Hakimu Mkazi Mfawidhi, Geni Dudu, ajitoe katika kesi hiyo na ampangie hakimu mwingine kwani walidai, alikuwa anaendesha kesi “kibabe” na kwa upendeleo. Hakimu Dudu alikataa ndipo washitakiwa walipoomba uamuzi wa Mahakama Kuu.

Washtakiwa walikuwa na hoja moja tu mbele ya Jaji Mchome: hakimu anapendelea. Anadaiwa kuwa akipendelea upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Juma Ramadhani. Alidaiwa kuwa alikuwa haandiki hoja za mawakili wa utetezi.

Jaji Mchome katika uamuzi wake juu ya rufaa ya washitakiwa, alisema hakuona sababu za Hakimu Dudu kung’ang’ania kesi wakati tayari upande mmoja umepoteza imani naye.

“Pale upande mmoja ukimkataa hakimu, lazima hakimu huyo awape faida ya mashaka wale wanaomkataa kwa kukubali kujitoa, ili kuihakikisha haki kwa kila upande katika kesi husika,” alisema.

Hivi kwa nini hakimu anakataa kujitoa katika kesi anayokataliwa na upande mmojawapo? Au inakuaje asijitoe mapema pale anapohisi hatatenda haki kutokana na mgongano wa kimaslahi au tu dhamira yake ikikataa kutokana na mazingira fulani?

Kwa mfano, ikiwa hakimu anachukia sana ulokole na kuipenda imani ya dhehebu lake tu la dini, ni vizuri akajiondoa katika kesi inayomhusu mtu anayeamini katika ulokole dhidi ya yule wa dhehebu lake. Au kama hakimu anachukia sana Wangoni au kabila lolote jingine, analazimika kujiondoa anapobaini mgongano wa kimaslahi.

Ni vizuri kwa maofisa hawa wa mahakama kuthibitisha uadilifu wao kikazi. Wanatakiwa kuondoa chembe ya shaka itakayotia shaka upande fulani katika kesi.

Hata enzi za Jaji Mkuu, Francis Nyalali, aliwahi kukumbusha mahakimu na majaji kwamba hawana sababu ya kushikilia kusikiliza kesi ambayo tayari wameombwa kujitoa.

Kesi ziko nyingi hivyo ni tatizo kwa hakimu au jaji kung’ang’ania moja hata pale anapoombwa kujitoa. Hakimu mwenye mtizamo wa kung’ang’ania kesi atambue anakiuka misingi ya uadilifu katika Mahakama.

0
No votes yet