Hakuna aliyebora ndani ya CCM


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 10 August 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

SASA Rais Jakaya Kikwete ametingwa. Marafiki zake ndani ya CCM ambao ama amekuwa akishirikiana nao au akitaniana nao hata kushikana ndevu wanakabiliwa na kashfa mbalimbali.

Kashfa kongwe zinamkabili aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa aliyejiuzulu baada kukumbwa katika kashfa ya Richmond. Swahiba na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz pia alikumbwa katika kashfa hiyo.

Mwanasheria mkuu wa serikali wa zamani na aliyekuja kuwa Waziri wa Miundiombinu, Andrew Chenge anahaha kupangua kashfa ya kujipatia vijisenti kutokana na ununuzi wa rada.

Kashfa mpya inamwandama Mzee wa Sera ya Uzawa Idd Simba, ambaye alipokuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika awamu ya tatu, Kikwete alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Idd Simba, ni mfanyabiashara na anakuwa kiongozi maarufu kukumbwa na kashfa nzito sawa na ile ya mwaka 2001.

Mwaka 2001, alilipuliwa bungeni kwa hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya kuhusu sakata la vibali vya sukari. Hatimaye, Simba ajiuzulu uwaziri.

Akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Simba ametajwa katika sakata la uuzaji kinyemela shirika hilo la umma.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zimepewa kazi ya kukagua hesabu za shirika na kuchunguza taratibu.

Hata kama sakata hili halimhusu Rais Kikwete moja kwa moja, ukweli unaihusu serikali yake na CCM. Kwa vyovyote, mkono wake utahitajika kunusuru hadhi ya serikali au CCM.

Simba hayuko peke yake. Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi anatajwa. Katika utetezi wake, Dk. Masaburi anasema yeye hahusiki lakini ni kweli fedha za mauzo ya UDA zimewekwa katika akaunti ya mtu binafsi.

Halafu Dk. Masaburi akawalipua wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Azzan Zungu na Abbas Mtemvu kwa kuwahusisha na kashfa nyingine ya uuzaji kifisadi mashamba ya Shirika la Maendeleo ya Uchumi Dar es Salaam (DDC) na matumizi mabaya ya fedha za ujenzi wa jengo la kibiashara la Machinga Complex, Ilala.

Kama kweli Zungu na Mtemvu wanahusika basi kuna tatizo zito katika uongozi wa nchi. Kwa nini Dk. Masaburi hakuweka wazi tuhuma hizi mapema? Bila ya yeye kutajwa katika kashfa ya UDA, tusingejua hayo mengine? Itakuwa kuna kashfa nyingi zimefunikwa.

Mei 2006, Dk. Mzindakaya alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu sakata la sukari mwaka 2001 alisema katika suala lile, kama Idi Simba angeelewa, lile jambo lisingetoka hadharani, kwani kabla ya kutolewa kashfa ile hadharani, Waziri aliandikiwa barua, aliambiwa, lakini aliendelea na msimamo wake wa kushikilia kosa lake.

Alisema jambo kubwa ni kukosoana na kurekebishana ndani kabla ya kutoa jambo hadharani tena ikitiliwa maanani wote ni CCM, lakini hatua hiyo ilifikiwa kutokana na mhusika (Waziri) 'kutosikia'.

“Unamwambia mhusika, hivi sivyo, lakini ingekuwa hivi ndivyo, yeye anashikilia msimamo wake, basi ndipo unapoamua kuweka mambo hadharani ili umma uweze kuelewa,” alisema.

Kauli hii ni ya kulindana, kwamba kumbe wanaotajwa hadharani kwa kashfa mbalimbali za ufisadi nchini ni wale walioshindikana kulindwa na mfumo wa CCM.

Aaaaaah! Kumbe hata sakata la uuzwaji wa ekari 800,000 Katumba, Mpanda linalindwa na mfumo huohuo sawa na wizi kupitia Kagoda, Meremeta, Richmond, EPA, Mwananchi Gold, Kiwira. Wengine wanakata posho za polisi.

Aaaaaah! Ndiyo maana maofisa waliotuhumiwa katika kashfa ya Richmond waliachwa wajiuzulu bila kushitakiwa. Na kadri itakavyopendeza, hata jamaa waliohonga wabunge ili bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ipitishwe watalindwa na mfumo huohuo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: