Hakuna nia ya kuondoa umaskini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

ILI jambo lolote lifanikiwe linahitaji mambo matatu: nia, sababu na uwezo. Katika utekelezaji, likipungua moja kati ya mambo haya huwa hakuna mafanikio.

Lakini jambo kubwa zaidi katika haya ni nia. Katika misahafu ya Mwenyezi Mungu na mafunzo ya manabii tunausiwa kwamba kila amali ya mja huanza na nia. Hata wahenga wetu wanasema, “penye nia pana njia.”

Katika nia ndipo zilipo fikra na ubunifu, uwajibikaji na uadilifu, kujitolea na kuthamini utu.

Kwa mazingira ya Tanzania na tatizo la umaskini – sababu za kuondoa umaskini zipo; uwezo kuondoa umaskini upo; lakini nia ya kisiasa ya kuondoa umaskini inakosekana.

Kila mmoja anafahamu fika kwamba kiini cha umaskini wetu si uvivu wa wananchi  kama wenye dhamana wanavyosema, bali kiini ni watawala na watendaji walafi, wabadhirifu na mabingwa wa ufisadi.

Watawala hawa wanadhulumu na kunyonya haki za watu kwa mori kubwa, motisha kubwa na msukumo kubwa. Hawana uchungu na nchi.

Hawana huruma kwa wajane wanaohangaika kila siku kutafuta riziki za kuwalisha yatima. Hawana huruma kwa yatima wenye vipaji wanaokosa fursa ya kwenda shule kwa sababu mama hana pesa ya mchango wa dawati. Hawana huruma kwa wajawazito wanaojifungulia sakafuni katika hospitali zetu.

Hawana huruma kwa wajawazito wanaonyimwa huduma hadi kufa kwa sababu ya kukosa pesa kuchangia matibabu. Hawana huruma kwa wazee waliotumia nguvu zao za ujana kulijenga taifa lakini sasa hawapati pesa za kujikimu.

Hawana uchungu kwa wataalamu wetu ambao taifa liliwasomesha kwa pesa nyingi lakini sasa wameikimbia nchi kwa sababu hawaoni wakitendewa haki.

Hawana huruma kwa vijana wanaokosa ajira na nguvu kazi yao kupotea bure bila kuzalisha, jambo ambalo linatengeneza kizazi cha watu maskini wala hawana uchungu na raslimali za zinazochotwa tu bwerere kwa kisingizio cha uwekezaji na ukuzaji uchumi.

Uchumi gani huo unaokua bila kukua mifukoni mwa watu? Maana ya kukua kwa uchumi ni kuinuka kwa hali ya maisha ya watu. Ni uchumi upi mnauongelea? Labda uchumi wa mafisadi maana huo unakua kwa kasi zaidi. Tuhabarisheni.

Wananchi wanapewa ahadi hewa za kinafiki. Mnafiki akitoa ahadi hatimizi. Akisema anasema uongo. Na ukimwamini anaivunja imani.

Inabuniwa mipango mbalimbali ya kiuchumi ambayo malengo yake si kuhudimia umma bali kuuibia na kuumiza umma. Wenye dhamana wanauza raslimali za nchi kwa bei che, huku wakimegewa “ten pasenti”.

Hakuna anayewajibishwa. Juu ya hayo ni wafujaji wa kodi ya wakulima na wafanyakazi kwa matumizi makubwa ya anasa kana kwamba hawaujui umaskini uliokithiri, unaowazunguka wananchi.

Agustine Mrema akiwa Mwanza mwaka 2000 katika moja ya mikutano yake hadhara alisema “wanakula kwa mikono miwili tena bila kunawa.”

Ulaji huu wa kifisadi unaiangamiza Tanzania. Katu taifa haliwezi kukusanya mtaji wa kujenga viwanda vipya au kufufua viwanda alivyoacha Mwalimu Nyerere kwa sababu ya wizi wa waziwazi wa watawala na watendaji.

Taifa haliwezi kuwekeza katika elimu na utafiti. Baya zaidi hakuna nia ya kudhibiti ufujaji na wizi huu. Wanaachwa tu hivi hivi kwa kisingizio kwamba hakuna ushahidi. Je, hata ushahidi wa mazingira haupo?

Tunaufahamu mishahara ya mawaziri na watendaji na marupurupu waliyonayo lakini hawezi kuwa na pesa zaidi ya Sh. 1 bilioni katika kipindi cha miaka kumi ya utumishi wao hata kama wanajinyima kiasi gani.

Miaka miwili iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema ana akiba ya Sh. 25 milioni benki. Iangalie historia yake. Zaidi ya nusu ya maisha yake amekuwa serikalini tena katika ‘nafasi nyeti zenye mianya ya ulaji kwa mafisadi’ kisha ulinganishe na wenzake na walio chini yake utapata majibu.

Kwa ujanja upi na posho zipi wanazozipata za kumzidi Pinda? Hapo bila shaka ushahidi wa mazingira unatupa majibu sahihi kwamba upo ufisadi na dhuluma kubwa inayofanywa na watawala na watendaji wa ngazi mbalimbali serikalini.

Hivi kwa nini mali zilizozochumwa kifisadi zisitaifishwe kwa manufaa ya taifa? Kwa nini uozo huu unachwa uendelee kuota mizizi? Nini kinazuia hasa? Sheria? Mfumo? Woga? Kulindana? Fadhila? Jibu li wazi – Nia haipo.

Ukizingalia takwimu za ufisadi unaondelea nchini utaona wazi kwamba Tanzania inao uwezo wa kuondoa umaskini ila pesa inaibwa.

Ukiuangalia uzembe unaofanywa mfano katika suala la umeme, msongamano wa magari ya Dar es Salaam, kulegalega kwa usafirishaji wa reli, kufa kwa shirika la ndege, viwanda vyetu kutokuzalisha, mikataba mibovu ya madini na uwekezaji, utakubaliana nami kwamba Tanzania haipaswi kuwa ombaomba.

Bila nia njema ya kuutumikia umma wa wakulima na wafanyakazi wa Tanzania huwezi kuupunguza umaskini. Bila nia ya dhati huwezi kubuni mikakati ya kuondoa umaskini katika taifa kwa kuzalisha kwa wingi katika kilimo na viwanda.

Bila nia nzuri ya kuondoa umaskini huwezi kusimamia vema ukusanyaji kodi na kuondoa misamaha holela ya kodi. Bila nia ya kizalendo huwezi kuondoa umaskini kwa kuendelea kukumbatia ufisadi na uozo.

Bila nia yenye huruma huwezi kuondoa umaskini kwa ajira za uchuuzi. Bila nia thabiti huwezi kuondoa umaskini pasipo kutengeneza ajira zenye mafao ya uzeeni.

Yote haya yanategemea nia njema ambayo haipo.

Wakati umefika sasa tutambue kwamba kuendelea kukua kwa umaskini na kukua kwa ufisadi kunahatarisha amani ya nchi yetu.

Niliwahi kusema hapa kuwa jeshi la vijana wasio na ajira ni kubwa na huwezi kulidhibiti kwa bunduki, risasi na mabomu bali kwa ajira, huduma, matumaini ya maisha bora.

Viongozi, zisuteni nafsi zenu acheni kuiba mali ya umma. Acheni dhuluma na ufisadi, fanyeni kazi ya kuwatumikia Watanzania kwa nia safi yenye uadilifu na uaminifu. Juu ya hayo muongopeni Mwenyezi Mungu.

+447404486150
0
No votes yet