Hakuna vitisho vitakavyotusimamisha


editor's picture

Na editor - Imechapwa 22 July 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

NI jambo la kustaajabisha kwamba Polisi wamepata ujasiri wa kutumiwa ili kuvitisha vyombo vya habari. Ijumaa iliyopita Polisi walivamia na kupekua ofisi za gazeti la MwanaHALISI pamoja na nyumbani kwa Saed Kubenea , Mkurugenzi wa kampuni ya Hali Halisi Publishers (HHP) inayochapisha gazeti hili na lile la Mseto.

Tunasema ni jambo kustaajabisha kwa sababu kile walichokuwa wanasaka Polisi, eti ni nyaraka za wateja wa benki zinazodaiwa kuchukuliwa kwa mazingira wanayoyajua Polisi, ni kichekesho cha mwaka.

Kwa kutumiwa, Polisi wetu, ambao kwa kodi za wananchi sehemu yake tukiwa tunalipa sisi, walithubutu kufika kwenye ofisi za gazeti hili na kufanya upekuzi kwenye makabrasha na kompyuta kwa nia ya kutafuta taarifa 'nyeti' za benki.

Tunashangaa na kusikitika kwamba sasa Polisi na wote waliowatuma wametumbukia katika kina kirefu cha kutofikiri vema, kiasi cha kujiruhusu kutumwa kumfunga pingu mjumbe aliyewasilisha taarifa za kuwepo janga la kitaifa.

Gazeti hili bila ya kutafuna maneno lilichapisha orodha ya majina ya watuhumiwa wa ufisadi. Halikuishia hapo tu, lilibainisha ni akina nani wamenufaika na fedha za akaunti ya madeni ya nje (EPA) ambapo serikali hadi sasa imeshindwa kuwataja hadharani.

Halikutaja tu, lilisema nani walilipwa fedha hizo kupitia akaunti za Tangold na Meremeta, miongoni mwa makampuni kadhaa. Likataja jina moja baada ya jingine, lilifanya hivyo kwa nia moja: Kutimiza wajibu wake kama mdomo wa umma.

Kwa hivyo, MwanaHALISI ilipaza sauti kusema wale ambao serikali inaogopa kuwataja ndio hao. Likasema, hawa ndio waliochotewa mabilioni ya shilingi na serikali, wakazisambaza kwa maslahi yao.

Polisi waliostahili kutumia taarifa hizo kufanya uchunguzi wao ili kusaidia serikali kubaini waliko mafisadi, ilifumba macho isione na ikaziba masikio isikie. Ikabaki kama vile haina wajibu na jukumu.

Badala yake sasa, Polisi inakubali kutumiwa na wanasiasa kwa nia ya kueneza hofu kwa vyombo vya habari bila ya kujua kwamba kwa kufanya hivyo wanasaidia kupalilia uhalifu na kuwapa mafisadi nafasi ya kuendelea kutanua ndani ya nchi hii kama vile wapo juu ya sheria.

Pamoja na vitisho vya Polisi, sisi tunasema bado hatujateteleka na msimamo wetu unaotokana na sera na mwelekeo wa kuanzishwa kwetu kama taasisi ya habari ya karne ya 21. Hatujaogopa na wala hatuwezi kuogopa kutekeleza wajibu wetu kwa umma na taifa letu.

Tunafurahi kwamba tunajua fika kwa yale tunayoyashughulikia, tunalindwa na Katiba ya Jamahuri ya Muungano ambayo katika Ibara ya 27(1) kila raia anahimizwa kutimiza wajibu wake katika kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote milikiwa kwa pamoja na wananchi na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.

Tunasema hakuna cha kutusimamisha katika yale tunayoyaamini. Tunafanya kazi ya uandishi wa habari si kwa kubahatisha bali kwa akili timamu. Tunatafiti kwa mujibu wa sheria na tunaandika kulingana na maadili ya taaluma.

Kwa sababu hiyo, tunasema tunaangalia mbele. Kamwe hatuwezi kurudi nyuma kwa vitimbi vya Polisi na wale waliowatuma.

Hatutaki hata mara moja kuwa sehemu ya kulinda mafisadi na wahujumu uchumi na raslimali za taifa. Tutaendelea kufanya kazi tuliyoichagua pasina hofu na mtu yeyote, awe ni mwenye fedha au mamlaka makubwa kiasi gani katika taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: